Monday, July 20, 2015

KAMPUNI YA SIMU YA TTCL YATOA BATI 100 KWA SHULE MBALIMBALI MKOANI NJOMBE

Naibu waziri wa maendeleo ya jamii jinsia na watoto Dkt Shirika la mawasiliano la TTCL Tanzania limekabidhi jumla ya bati 100 zenye thamani ya shilingi Milioni mbili kwa Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Njombe Dokta Pindi Hazara Chana ambaye pia ni Naibu waziri wa maendeleo ya Jamii  Wanawake jinsia na watoto kwa ajili ya sekta ya elimu mkoani Njombe.

Akikabidhi bati hizo  kwa niaba ya mkurugenzi kuu wa TTCL Tanzania, Kaimu mkurugenzi kanda ya nyanda za Juu kusini bwana James Mlaguzi amesema kwa kuwa shirika hilo limekuwa likifanya kazi za kijamii kupitia mapato yake hivyo limeamua kuchangia sekta ya Elimu mkoa wa Njombe kupitia Mbunge Chana kwa kutoa bati hizo.

Amesema katika mkoa wa Njombe wametoa jumla ya bati 100 ambazo zitasaidia kupunguza changamoto katika ujenzi wa madarasa na maabara katika shule mbalimbali.

Aidha mara baada ya kukabidhiwa bati hizo, Naibu waziri Chana na msafara wake pamoja na TTCL wameelekea katika shule ya Sekondari Mbeyela ambako amekabidhi bati 20 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Taarifa  fupi ya shule ya Mbeyela Sekondari iliyosomwa na mkuu wa shule hiyo Mwalimu Emphraim Ngimba imeeleza kuwa shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 500 na walimu zaidi ya 50 zitasaidia kupunguza adha ya ukarabati wa madarasa kutokana na madarasa mengi kutokamilika.
Akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo wakati wa kukabidhi bati hizo 20 Mbunge Pindi Chana ametumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi hao kujikita zaidi katika masomo ili waje kuwa viongozi makini katika Taifa la Tanzania.


Amesema serikali ya Jamhuri ya muungano imekuwa ikijali sana elimu kwa watoto jambo lililopelekea kutolewa kwa bati hizo ikiwa ni pamoja na kufuta karo kwa shule za msingi.


Kwa upande wake Afisa elimu taaluma mkoa wa Njombe Walimu Hansi Mgaya akizungumza kwa Niaba ya afisa elimu mkoa amesema kutolewa kwa bati 100 na shirika la TTCL Tanzania kutasaidia kukamilisha baadhi ya madarasa na maabara katika shule za sekondari mkoa wa Njombe.

Hata hivyo amesema kwa kuwa serikali imekuwa ikizitumia sekta binafsi pamoja na mashirika ya umma katika kukuza maendeleo ya Taifa basi mpango wa matokeo makubwa sasa katika sekta ya elimu kufanikiwa zaidi kwa kushirikiana na wadau Mbalimbali wa elimu.

No comments: