Mheshimiwa
Hailemariam Desalegm, Waziri Mkuu wa Ethiopia;
Mheshimiwa
Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Dkt. Abdala Kigoda, Waziri wa Viwanda na
Biashara;
Mheshimiwa Dkt. Kebwe Stephen Kebwe, Naibu Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Ndugu Lobani Gutieres Ravelo, Naibu Mkurugenzi Mkuu
wa Kampuni ya LABIOFAM, Cuba;
Ndugu
Joyce Phumaphi, Katibu Mtendaji wa ALMA;
Mheshimiwa
Lorge Luis Lopez Tarmo, Balozi wa Cuba nchini Tanzania;
Mheshimiwa Evarist Ndikilo, Mkuu
wa Mkoa wa Pwani;
Waheshimiwa
Mabalozi wa Nchi za Nje na
Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa;
Wageni Waalikwa;
Wanahabari;
Mabibi na Mabwana;
Ni furaha iliyoje kwangu kuwepo hapa
leo, kushuhudia uzinduzi wa Kiwanda cha
Kutengeneza Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi wa Mbu. Furaha yangu inaongezeka zaidi kwa kuwepo ugeni
mkubwa wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Desalegn. Yeye ndiye
Mwenyekiti wa Umoja wa Viongozi wa Afrika walio mstari wa mbele katika
Mapambano Dhidi ya Malaria katika Bara la Afrika (ALMA). Kwa niaba ya Watanzania
wenzangu wote namshukuru sana mgeni wetu kwa kutenga muda wake na kusafiri
kutoka Ethiopia kuungana nasi siku ya leo. Ujio wako unaweka uzito mkubwa
kwenye azma yetu hii ya kutokomeza Malaria katika Bara letu.
Pamoja nasi, napenda pia kuwakaribisha
watu wafuatao; kwanza, Ndugu Alfred
Romberto Corta, Rais wa Kampuni ya LABIOFAM ya Cuba waliotuuzia teknolojia ya
kutengeneza dawa hizo. Wa pili, ni
Bibi Joy Pumaphi, Katibu Mtendaji wa ALMA. Mwisho, ingawaje siyo mwisho kwa
umuhimu wageni wote wengine waliopo hapa leo.
Chimbuko la Kiwanda
Wageni waalikwa;
Chimbuko la ujenzi wa kiwanda hiki ni
ziara yangu niliyoifanya nchini Cuba mwezi Desemba, 2009. Katika ziara ile,
mwenyeji wangu Rais Raul Castro alinipangia ratiba ya kutembelea Kiwanda cha LABIOFAM
kinachomilikiwa na Serikali ya Cuba na kinachozalisha dawa za viluwiluwi vya mbu
wanaosababisha malaria. Baada ya
kuvutiwa na maelezo na teknolojia ile na kuhakikishiwa kuwa haina athari kwa
mazingira na afya ya binadamu niliagiza mambo mawili yafanyike. Kwanza, Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii iagize dawa hizo kutoka Cuba zitumike nchini; na Pili, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lianzishe ushirikiano na Kampuni
ya LABIOFAM kwa lengo la kujenga kiwanda cha aina hiyo hapa nchini.
Shukurani kwa
Serikali ya Cuba
Mabibi na Mabwana;
Shukrani zangu za pekee zimuendee
Mheshimiwa Raul Castro, Rais wa Jamhuri ya Kisoshalist ya Cuba, na rafiki mkubwa
wa Tanzania, kwa kukubali kutuuzia teknolojia hii. Wenzetu wa Cuba wametufaa
sana kwani “hawajatupa tu samaki, bali
wametupa ndoano ya kuvua samaki”.
Wangeliweza kabisa kwa tamaa kukataa kutuuzia teknolojia na ujuzi wao na kutaka kutuuzia dawa. Pamoja na kuwa wao si nchi tajiri hawakufanya
hivyo. Wameshirikiana nasi katika ujenzi na kukubali kutupa wataaalam ambao
watabakia nchini kwa miaka mitano kufundisha watu wetu na kutusaidia kwa
masuala ya kiufundi na kitaalam. Tunaye
pamoja nasi kiongozi na Mhandisi Mkuu aliyesimamia ujenzi huu Ndugu Alfredo R.
Drespo Dorta ambaye amesafiri toka Cuba kuja kushuhudia ufunguzi wa kiwanda
hiki. Huu ndio urafiki wa kweli na udugu.
Nakuomba Mheshimiwa Balozi wa Cuba unifikishie shukrani zangu za dhati
na za Watanzania wenzangu kwa Rais Raul Castro na kwa ndugu zetu wananchi wa
Cuba.
Vita Dhidi ya Malaria
Mabibi na Mabwana;
Leo tunapiga hatua kubwa na ya aina yake
katika vita yetu dhidi ya malaria hapa nchini na katika Bara la Afrika hasa
nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Katika Ripoti ya Malaria Duniani ya mwaka 2014
iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa, mwaka 2013,
malaria ilisababisha vifo vya watu 584,000.
Kati ya vifo hivyo asilimia 90 vilitokea
barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Bahati mbaya sana waathirika wakubwa
walikuwa ni wanawake na watoto chini ya umri wa miaka 5. Inakadiriwa pia kwamba malaria inazigharimu
nchi wastani wa asilimia 40 ya fedha
zao za bajeti ya afya na kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wa baadhi ya nchi
za Afrika kwa asilimia 1.3.
Kinachosikitisha
zaidi ni ule ukweli kwamba, upo uhusiano mkubwa kati ya malaria na
umasikini. Bahati nzuri ugonjwa huu
unazuilika na kutibika maana uliwahi kuwa tishio kubwa duniani lakini leo ni tishio zaidi Afrika. uzoefu wa nchi nyingine duniani waliofanikiwa
kuzuia na kutokomeza. Unatupa matumaini kuwa na sisi tukiiga mifano yao
tunaweza kuwa kama wao. Kuwekeza katika kiwanda cha aina hii kutatuwezesha kutokomeza
malaria.
Hali ya Malaria
Nchini
Mabibi na Mabwana;
Tangu mwanzoni mwa uongozi wangu
kupambana na malaria tuliupa kipaumbele cha juu. Ndicho chanzo cha wagonjwa
wengi na vifo vingi nchini. Tumekuwa tunafanya mambo makuu matatu katika
kupambana na malaria; kwanza,
kutumia dawa mseto kutibu wagonjwa wa malaria. Pili, kuhamasisha matumizi
ya vyandarua vilivyopuliziwa dawa na tatu,
kupulizia dawa inayoua mbu ndani ya nyumba. Kwa kufanya hivyo tumefanikiwa kwa
kiasi kikubwa kupunguza wagonjwa na vifo
vitokanavyo na malaria. Kiwango cha maambukizi nacho kimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi asilimia 10 mwaka 2012. Vifo
vitokanavyo na malaria kwa uzazi vimekupungua kutoka 41 kwa vizazi hai 100,000
mwaka 2004 hadi 12 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2014. Idadi ya wagonjwa chini ya miaka 5 imepungua
kutoka wagonjwa milioni 5,372,569 mwaka 2004 hadi wagonjwa milioni 3,486,326 mwaka 2014 na vifo vya watoto wa miaka 5 kwenda chini
vimepungua kutoka 7,907 mwaka 2004
hadi 4,008 mwaka 2014. Kwa ujumla idadi ya wagonjwa wote imepungua
kwa asilimia 51 na vifo kwa asilimia 71
kati ya 2004 na 2014.
Kwa upande wa matumizi ya vyandarua
vilivyotiwa dawa, Serikali imesambaza vyandarua 26,371,329 nchi nzima, yaani vyandarua viwili kwa kaya, kwa watoto
wa umri wa chini ya miaka 5 na kina mama wajawazito. Matokeo yake, idadi ya matumizi ya vyandarua vilivyotiwa
dawa imeongezeka kutoka asilimia 23
mwaka 2004 hadi asilimia 92 mwaka
2012. Kwa upande wa wajawazito kutoka asilimia 27 mwaka 2004 hadi asilimia 75. mwaka 2014. Kwa upande wa watoto wa miaka 5, idadi
imeongezeka kutoka asilimia 26 mwaka
2004 hadi asilimia 72 mwaka 2014.
Mafanikio zaidi makubwa na ya
kujivunia yamepatikana Zanzibar. Kiwango cha maambukizi ya malaria kimeshuka na
kufikia asilimia 0.2 hivi sasa.
Pamoja na kufanya yale mambo matatu ndugu zetu wa Zanzibar walipulizia na kuua viluwiluwi vya mbu waenezao
malaria. Kama imewezekana Zanzibar inatufanya
tuamini kuwa itawezekana na huku Bara pamoja na ukubwa wa eneo na wingi wa watu. Ni kwa sababu hiyo, tulichukulia uwekezaji
huu wa kiwanda cha kuzalisha viuatilifu kuwa uwekezaji wa kimkakati katika vita
dhidi ya malaria. Kwa kuwa sasa dawa
hizi zitakuwa zikizalishwa nchini kwa wingi na gharama nafuu, jukumu letu sasa
ni kuanzisha kampeni nchi nzima ya kupulizia maeneo yote ili kuua viluwiluwi
vya mbu pale wanapozaliwa. Sasa tunatangaza vita si tu na mbu bali na
viluwiluwi vyake.
Maelekezo Mahsusi
Mabibi na Mabwana;
Natoa pongezi kwa Bodi ya Shirika la
Taifa la Maendeleo (NDC) kwa kusimamia vizuri ujenzi wa kiwanda hiki. Jukumu kubwa na lililo mbele yenu sasa ni kuhakikisha kiwanda hiki
kinazalisha na kujiendesha kibiashara.
Hatutarajii kiwanda hiki kiijiendeshe kwa hasara maana biashara yenyewe
ni ya uhakika ndani na nje ya nchi yetu.
Kama nilivyokwishasema hapo awali, Tanzania ni mwanachama, tena mwanachama
mwanzilishi wa Umoja wa Marais wa Afrika walio katika Mapambano Dhidi ya
Malaria (ALMA). Umoja huu una nchi 49 Sote kwa pamoja, tunayo dhamira ya
kuondokana na malaria katika nchi zetu na tumejiwekea malengo. Uwepo hapa wa
Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Ethiopia ni ushahidi huo.
Shirikianeni na Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa na Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii kutangaza bidhaa za kiwanda
hiki. Tafuteni masoko barani Afrika, maana, kutokomeza malaria hakutegemei
mafanikio katika nchi yetu tu, bali pia na kwa nchi nyingine katika Bara letu.
Naelekeza pia ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kukitumia kiwanda hiki katika mipango yake
ya kutokomeza malaria katika Halmashauri zetu.
Halmashauri zihamasishe watu wetu na kaya zilizo kwenye maneo yao ya utawala
kutumia dawa zinazozalishwa na kiwanda hiki.
Angalieni namna bora ya kuwezesha hilo kufanyika. Kwa kupulizia dawa hizi na kutokomeza
viluwiluwi wa mbu kutang’oa mzizi wa fitina unaosababisha maambukizi na vifo
vya malaria.
Hitimisho
Mabibi na Mabwana;
Kama nilivyosema awali, leo ni siku ya
furaha sana kwangu kwa kukamilika kiwanda hiki na kupata fursa ya kushuhudia
ufunguzi wake. Mafanikio tuliyoyapata katika kutibu malaria ni makubwa na ya
kutia moyo. Hata hivyo, mafanikio hayo
yasingekuwa endelelevu iwapo tusingeongeza nguvu na mkazo katika kukinga na
kuzuia maambukizi. Kiwanda hiki tunachokifungua
leo kitaimarisha uwezo wetu wa kukinga na kuzuia maambukizi ya malaria. Wahenga wamesema daima “kinga ni bora kuliko tiba”. Sasa
tuna uhakika kuwa mapambano yetu dhidi ya malaria tumeyafikisha mahali pazuri. Nafurahi kuona leo tunatamka kwa vitendo kuwa
“Malaria Haikubaliki”. Sasa natangaza kuwa kiwanda cha Kuzalisha
Viuadudu vya Viluwiluwi vya Mbu kijulikanacho kama Tanzania Biotech Products Limited kimefunguliwa rasmi.
Asanteni kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment