Wednesday, June 17, 2015

ZANZIBAR YADHIMISHA SIKU YA KUPAMBANA, USAFIRISHAJI NA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA DUNIANI

 Waandamanaji katika maadhimisho ya siku ya kupambana na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya Duniani wakipita mbele ya mgeni rasmi katika kiwanja cha Kombawapya. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
 Rais wa watoto Tanzania  Ameir Haji Khamis akitoa ujumbe wa watoto na dawa za kulevya kwenye sherehe za siku ya kupambana na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya Duniani katika kiwana cha Kombawapya.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej akitoa nasaha katika  maadhimisho ya siku ya kupambana na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya Duniani katika kiwanja Kombawapya Mjini Zanzibar.
 Baadhi ya vijana waliopata nafuu kutokana na utumiaji  wa madawa ya kulevya wakimsikiliza mgeni rasmi katika maadhimisho hayo. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
 Mgeni rasmi Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej katika picha ya pamoja na vijana waliopata nafuu.
 Naibu Waziri wa Afya akimkabidhi kombe la ushindi Nahodha wa Zanzibar Youth Forum (kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya Zanzibar Kheriyangu Mgeni Khamis.

Na Rahma Khamis Maelezo Zanzibar
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Mhe. Fatma Abdulhabib Fereji amesema dawa za kulevya ni janga  la Kidunia linalopigwa vita  na Mataifa yote Duniani.

Hayo ameyaeleza huko Kiwanja cha Kombawapya Zanzibar katika Maaadhimisho ya kupiga vita  Utumiaji na Usafirishaji pamoja na  Udhalililshaji wa Dawa za kulevya Duniani.

Amesema Zanzibar inakadiriwa kuwa na watumiaji wa dawa za kulevya zaidi ya 9000 idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na visiwa hivyo pamoja na idadi ya wakaazi wake jambo ambalo linahatarisha maisha ya vijana kujiingiza zaidi katika utumiaji huo
Aidha amesema Seikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za kulevya chini ya Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais huadhimisha siku hiyo kila Mwaka kwa lengo la kuitanabahisha Jamii kuwa Dawa  hizo ni janga la Kitaifa lisilovumilika hivyo linahitaji nguvu na maarifa ili kupambana na janga hilo.

 Hata hivyo Waziri huyo amesema kuwa  Zanzibar ni sehemu ya Dunia inayounga mkono juhudi za Mataifa na Jumuiya mbalimbali za Kimataifa katika kupiga vita Dawa hizo ambazo kwa asilimia kubwa zinaathiri nguvu kazi ya Taifa lolote Duniani hasa vijana wenye umri mdogo wakiwemo Wanafunzi.

Aidha amesema kuwa katika kuadhimisha siku hiyo jamii hupata fursa ya kuwakumbuka wale wote ambao kwa namna moja au nyengine wameathirika au kupoteza maisha kwa utumiaji ama  usafirishaji wa Dawa hizo haramu.

“Tunawajibu mkubwa wakutambua kwamba umuhimu wa siku hii ni wakipekee ambapo kila Mdau iwe Serikali ,Taasisi, Jamii au hata mtu mmoja mmoja lazima aguswe na maadhimisho hayo kwa namna moja au nyengine hasa ikizingatiwa kwamba tatizo la Dawa za kulevya tayari limeshaigusa kila Familia katika Nchi yetu”,amesema Waziri huyo.

Akielezea baadhi ya Mikakati ya kupambana na Dawa hizo amesema kuwa ni kuimarisha Viwanja vya Ndege na Bandari kwa kuweka Mitambo ya kisasa , kuendelea kuzipatia Ruzuku na Misaada mbali mbali Nyumba za upataji nafuu (Sober Houses)pamoja na kuwajengea uwezo wa kitaalamu Watendaji wa Tume Ofisi ya Mkemia Mkuu na Mamlaka ya kupambana na Rushwa.

Akifafanua zaidi kuhusu  mikakati hiyo amesema kuwa ni  kupambana na Dawa hizo Waziri ameeleza kuwa kuendelea na hatua za ukamilishaji na ujenzi wa Kituo cha Tiba na marekebisho ya tabia  kwa Vijana wanaowacha Dawa hizo (Treatment Rehabilitation Center) na kusimamia uendeshaji wa Kesi za Dawa za kulevya hadi kujua hatma ya kesi hizo ili kusiwe na ubabaishaji wowote katika Vyombo vya Sheria.

Nae Sandra Seif  Nyambu ambae ni Kijana aliyepata nafuu katika utumiaji wa Dawa za kulevya amesema kuwa Zanzibar bila ya Madawa ya kulevya inawezekana kwani yeye alikuwa mtumiaji wa Dawa hizo ambae sasa  yupo salama baada ya kujiunga na Nyumba za kurekebisha tabia (Sober Houses).

Hata hivyo Kijana huyo ameishukuru Sober House  pamoja na Familia yake kwa kumsaidia kuachana na Madawa hayo  kwani utumiaji wa Dawa hizo unapoteza Mawasiliano Kimwili na Kiakili.

“Nashukuru nimekuwa Kiongozi bora katika Familia na pia Mwanachama bora ambae najiamini kusimama popote na mtu yoyote akanisikiliza bila ya matatizo”, amesema Sandra.

Hata hivyo kijana huyo amewataka wale wote ambao waliojiingiza katika janga hilo waende kujiunga katika Nyumba za kurekebisha tabia ili waweze kupata nafuu na kuendelea kuwa viongozi wazuri katika familia na jamii kwa ujumla ambapo ujumbe wa mwaka huu ni IMARISHA AFYA EPUKA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA.

No comments: