Mwenyekiti wa UWT Mufindi na mjumbe wa NEC Taifa Bi Marcelina Mkini akiwapongeza wanawake kwa kuonyesha kumkubali
Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mufindi Bi Marcelina Mkini wa kwanza kushoto akiwa na mkuu wa wilaya ya Mufindi Mboni Mhita na mwenyekiti wa UWT mkoa wa Iringa Bi Zainabu Mwamwindi wakati wa kongamano la wanawake wilayani Mufindi.
WAKATI joto la uchaguzi mkuu likiendelea kushika kasi ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) kwa wanachama wake kujitokeza kutia nia ya kuwania urais ,ubunge na udiwani , umoja wa wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Mufindi umemuomba mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mufindi Marcelina Mkini kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Mufindi kusini .
Wakizungumza mara baada ya kumalizika kwa kongamano la UWT wilaya ya Mufindi wajumbe wa kongamano hilo walisema kuwa toka nchi ipate uhuru wake mwaka 1961 wilaya ya Mufindi mkoani Iringa haijapata kuwa na mbunge mwanamke hivyo kwa uchaguzi wa mwaka huu lazima wanawake wachukue nafasi ya kuongoza ubunge jimbo la Mufindi kusini ambalo kwa sasa linaongozwa na mbunge Mendrady Kigola (CCM).
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mjumbe wa UWT Mufindi Bi Anna Nyamba kutoka kijiji cha Nyololo alisema kuwa wamevutiwa na utendaji kazi wa mwenyekiti wao Bi Mkini na kuwa wamepata kuwa na wenyeviti wengi wa UWT ndani ya wilaya ya Mufindi ila hawakuweza kuifanya jumuiya hiyo kuwa hai kama ilivyo sasa .
Hivyo alisema kazi nzuri iliyoonyeshwa na mwenyekiti huyo ndani ya UWT kuna uwezekano mkubwa zaidi wananchi wa jimbo la Mufindi kusini iwapo watamchagua kuwa mbunge wa jimbo kasi ya maendeleo inaweza kuongezeka zaidi .
Bi Nyambo alisema kipimo cha utendaji wa mwenyekiti huyo ni katika nafasi yake ya ujumbe wa NEC Taifa akiwakilisha wilaya ya Mufindi japo kazi mbali mbali za kimaendeleo alizozifanya kwa kukiwezesha chama cha mapinduzi kuwa hai kupitia jumuiya hiyo ya UWT ni kielelezo tosha kuwa iwapo atakubali kugombea ubunge na kushinda nafasi hiyo sura mpya ya maendeleo itaonekana katika wilaya ya Mufindi.
"
Sisi kama UWT Mufindi tutamuunga mkono mwanamke mwenzetu ambae kazi
zake zimeonekana katika nafasi hii ya ubunge...leo jimbo letu halina
barabara za uhakika na tunaopata shinda ni wanawake na watoto huduma
za maji jimboni hakuna hivyo tunataka kuwapa wanawake watuongoze "
Bi Aida Kaduma mjumbe kutoka kijiji cha Lufuna kata ya Mtwango alisema kuwa uwezekano wa Marcelina kuwatumikia wananchi wa jimbo la Mufindi kusini ni mkubwa kwani tayari kuna kazi nyingi za kimaendeleo ambazo amepata kushirikiana na wananchi kuzitekeleza kama mwenyekiti wa UWT wilaya hiyo .
Alisema kwa upande wa kijiji chake shule ya msingi Lufuna ilikuwa haina nyumba ya mwalimu mkuu ila kwa jitihada zake aliweza kuchangia bati zote 40 za kuezekea nyumba hiyo na sasa nyumba hiyo imekamilika na mwalimu anaishi .
Pia alisema mbali ya kusaidia sekta ya elimu amepata kuchangia taasisi mbali mbali za kiserikali na dini katika jimbo la Mufindi ambako amepata kualikwa kama mgeni rasmi na kuwa matumaini ya wanawake Mufindi kusini ni kuona wanawake wanachukua nafasi ya ubunge .
Kwa upande wake mwenyekiti huyo Bi Mkini mbali ya kuwapongeza wajumbe hao kwa ushawishi wao huo bado alisema bado anatafakari juu ya maombi hayo.
Japo aliwataka wanawake kwa mwaka huu kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za udiwani na ubunge katika wilaya hiyo ya Mufindi ili kuongeza chachu ya maendeleo na kuondoa watu kujisahau katika nafasi zao.
Katika kinyang'anyiro cha kuomba kuteuliwa kugombea ubunge ndani ya CCM mwaka 2010 jimbo la Mufindi kusini lilikuwa na wanachama 11 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambayo Bw Mendrady Kigola alishinda
Wengine waliojitokeza ni Thomas Bangu ,Hassan Kalinga , aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Benitho Malangalila , Faustine Mhapa ,Michael Mlonganile ,Mstapher Msovela ,Mary Ngailo ,Dr Alex Sanga, Marehemu Sprian Tweve na Marcelina Mkini
katika kinyang'anyiro hicho nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Kigola wakati nafasi ya pili ilichukuliwa na marehemu Tweve na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Bi Mkini.
No comments:
Post a Comment