Thursday, June 18, 2015

SHIRIKA LA OXFAM LAKABIDHI VITUO VYA KUSINDIKA NA KUHIFADHI MAZIWA KWA WANAWAKE WA VIJIJI VINNE VYA WILAYA YA NGORONGORO

Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro John Kulwa Mgalula akikata utepe kama ishara ya kuzindua  rasmi kituo cha kuhifadhia na kusindika maziwa.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro John Kulwa Mgalula akijalibisha Jokofu linalotumia umeme wa jua wakati wa uzinduzi huo.
  Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro John Kulwa Mgalula wa kwanza kushoto akioneshwa baadhi ya vifaa ambavyo walikabidhiwa vituo hivyo na Shirika la Oxfam Tanzania.
Baadhi ya Wanakikundi cha NOSOTWA kutoka kijiji cha Engaresero.
Stellah Julius kutoka Oxfam akizungumza  na wanakikundi cha NOSOTWA kutoka kijiji cha Engaresero.
 Mwenyekiti wa kikundi cha NAPONU akishukuru Oxfam kwakujengewa kituo cha kisasa cha kuhifadhi na kusindika Maziwa.
 Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro John Kulwa Mgalula Wanakikundi cha NOSOTWA kutoka kijiji cha Engaresero.
 Miriam Lembilika akishukuru kwa kuletewa vituo hivyo kijijini kwao.
Wanakikundi cha NYUWAT kutoka kijiji cha MALAMBO wakifurahia jambo.
  Afya imezingatiwa hiki ni moja ya vyoo ambavyo vipo katika vituo hivyo.
Wanakikundi cha NAPONU kutoka kijiji cha PINYINYI.
 Picha ya pamoja na wanakikundi wa NYUWAT kutoka kijiji cha MALAMBO.

Shirika lisilo la Kiserikali la Oxfam hapo jana lilikabidhi vituo vya kusindika maziwa kwa wanawake wa vikundi vinne kutoka vijiji vya Engaresero, Pinyinyi, Malambo na Piyaya vilivyoko katika wilaya ya Ngorongoro.

Akipokea vituo hivyo kwa niaba ya wanavikundi hao, Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro John Kulwa Mgalula, alisema ana imani vituo hivi vitawasaidia wanawake kukua kiuchumi na kuepuka kuwa tegemezi kwani wanawake wengi wamekuwa na sifa ya uvumilivu, uangalifu wa hali ya juu na kwamba mara nyingi wao hufanya vitu kwa uaminifu.

Mkurugenzi aliyashukuru mashirika ya Oxfam waliofadhili ujenzi wa vituo hivi pamoja na PALISEP waliotekeleza mradi huu kwa jitihada mbalimbali ambazo yamekuwa yakifanya katika wilaya ya Ngorongoro ili kuwakuza wanawake kiuchumi huku akitaja miradi mingine iliyofadhiliwa na Oxfam kuwa ni pamoja na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula, ujenzi wa majosho, pamoja na ujenzi wa vyanzo vya maji.

Akikabidhi vituo hivyo, Stellah Julius kutoka Oxfam alisema, “Baada ya kufanya utafiti uliowashirikisha wanawake wa vijiji hivi vinne walituambia kwamba wanahitaji vituo vya kusindika na kuhifadhia maziwa. Tumewajengea vituo hivi mvitumie kwa maendeleo yenu.” Stellah pia aliipongeza serikali na wadau mbalimbali kwa kutoa ushirikano mkubwa uliopelekea kufanikisha ujenzi wa vituo hivyo ikiwemo kutoa maeneo ya ardhi ya vijiji hivyo vinne.

Aidha Stellah aliwataka wanavikundi hao kuwa wabunifu wa namna ya kujiendeleza kibiashara na kuepuka kutegemea mashirika na taasisi ambazo zipo kwa muda tu.

Naye Mkurugenzi wa shirika la PALISEP Robert Kamakia alisema shirika lake limewajengea uwezo wana vikundi hao kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali na mbinu mbalimbali za kibiashara pamoja na kuwafundisha namna za kutunza maziwa kwa usafi.

Kwa upande wake Thomas Nade, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ngorongoro aliwataka wanavikundi hao kusajili vikundi vyao mapema ili vitambulike kisheria na waweze kunufaika kwa namna mbalimbali ikiwemo kupatiwa mikopo na kufungua akaunti ya benki.


Wanawake kutoka vijiji hivi vinne wanatarajia kunufaika kwa kujipatia kipato kutokana na kuuza maziwa na siagi.

Akionyesha furaha yake, Mariam Lembilika kutoka kijiji cha Malambo alisema, “Mimi kama mwanamke ambaye nina watoto watano na sina mume natarajia kutumia kipato kutokana na biashara hii kusomesha watoto.”

Naye Mary Saigulan kutoka kijiji cha Engaresero alisema, “Tutauza maziwa na siagi na kujipatia fedha nyingi ambazo zitatusaidia kuanzisha miradi mingine na kutuwezesha kujitegemea“

Ujenzi wa vituo hivi vinne umegharimu takribani shilingi za kitanzania milioni 120 na kila kimoja kina jokofu linalotumia umeme wa jua, mashine za  kusindika maziwa, madumu ya kuhifadhia maziwa, vipima joto, vipimo vya kupimia ubora wa maziwa, tenki la maji pamoja na mashimo mawili ya vyoo na bafu.

Vikundi hivyo vya NOSOTWA (Engaresero), NAPONU (Pinyinyi), NYUWAT (Malambo) na NASERIYAN (Piyaya) vina wana kikundi wapatao 30 kila kimoja.

No comments: