Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Bibi Felista Tirutangwa (aliyesimama) akizungumza wakati wa kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo ya Taasisi Wadau wa Usimamizi wa Sheria Juu ya Ripoti ya Ukaguzi ya CAG na Jinsi ya Kuitafsiri yaliyofanyika katika Hoteli ya Den France, Dar es Salaam.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad (aliyesimama) akizungumza wakati wa Mafunzo ya Taasisi Wadau wa Usimamizi wa Sheria Juu ya Ripoti ya Ukaguzi ya CAG na Jinsi ya Kuitafsiri yaliyofanyika katika Hoteli ya Den France, Dar es Salaam.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad (aliyesimama) akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Taasisi Wadau wa Usimamizi wa Sheria na Ofisi yake katika kuimarisha matumizi bora ya rasilimali za nchi. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Bibi Felista Tirutangwa na Mchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Ofisi ya Rais, Bw. Stephene Likunga (Kulia).
Washiriki wa Mafunzo ya Taasisi Wadau wa Usimamizi wa Sheria Juu ya Ripoti ya Ukaguzi ya CAG na Jinsi ya Kuitafsiri wakimsikiliza kwa makini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad (aliyesimama). Mafunzo hayo yalifanyika katika Hoteli ya Den France, Dar es Salaam.
Muwakilishi wa washiriki wa Mafunzo ya Taasisi Wadau wa Usimamizi wa Sheria Juu ya Ripoti ya Ukaguzi ya CAG na Jinsi ya Kuitafsiri, Bw. Stephene Likunga (aliyesimama) akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo ya Taasisi Wadau wa Usimamizi wa Sheria Juu ya Ripoti ya Ukaguzi ya CAG na Jinsi ya Kuitafsiri.
PICHA NA SAIDI MKABAKULI - NAOT
Na Mwandishi wetu
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imeendesha mafunzo ya siku moja ya Taasisi Wadau wa Usimamizi wa Sheria juu ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na jinsi ya kuitafsiri yanayofanyika katika Hoteli ya Den France jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad alisema kuwa mafunzo yanalenga kuwapa ufahamu juu ya ripoti za ukaguzi ambazo Ofisi yake inazitoa, na jinsi ya kuzitafsiri na kushughulikia masuala ya maadili yanatokana na ripoti za ukaguzi.
Prof. Assad aliongeza kuwa mafunzo hayo yanafanyika kwa kuzingatia Kifungu cha 27 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma, 2008, kama ilivyofanyiwa mabadiliko na Sheria ya Fedha Na. 10 ya mwaka 2010.
Kwa mujibu wa kifungu hiki, kinawataka wakaguzi wanaofanya kazi kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mara tu wanapobaini kuwepo kwa viashiria vya ulaghai/kugushi au rushwa wanapokuwa wanafanya ukaguzi kutoa taarifa kwa CAG.
Kifungu kinaongeza kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akithibitisha kuwepo wa viashiria hivyo anapaswa mara moja kuvitaarifu vyombo vya dola vya uchunguzi na nakala ya taarifa hiyo kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashitaka.
“Kifungu hiki kinaeleza vyombo hivyo vya dola (DCI/PCCB) kufanya uchunguzi wa kitaalamu juu ya tuhuma hizo na kukamilisha zoezi la uchunguzi ndani ya siku 60 tangu siku ya kwanza. Mara baada ya kumaliza uchunguzi huu vinapaswa kuwasilisha ripoti yao kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kwa ajili ya maamuzi ya hatua za kisheria zinazopaswa kuchukuliwa.
Mkurugenzi wa Mashitaka anapaswa kwa mujibu wa kifungu hiki kumtaarifu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu juu ya hatua alizochukua,” Prof. Assad alifafanua.
Prof. Assad alisema kuwa utekelezaji wa kifungu hiki kwa sasa unaendelea ingawa wakuu wa Taasisi wadau waliona ni vyema kuwepo na mpango maalumu wa utekelezaji wake. Kwa mujibu wa CAG, mpango huu utaongeza ufanisi zaidi katika utekelezaji wa matakwa ya sheria ya ukaguzi.
Prof. Assad aliongeza kuwa licha ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kupongezwa kutokana na utendaji kazi wake, hata hivyo, kumekuwa na malalamiko kuwa hakuna hatua za kuridhisha zinazochukuliwa. “Kwa mujibu wa maoni ya wananchi wa kawaida, hakuna hatua stahiki zinazochukuliwa dhidi ya watu wanaobainika kufuja mali za umma au kutumia mamlaka yao vibaya kama ripoti hizo zinavyokuwa zinaonesha,” alisisitiza.
Prof. Assad aliongeza kwa kuzingatia maoni hayo, mafunzo hayo yanategemea kuboresha ufanisi katika utendaji kazi kwa washiriki wa mafunzo. Aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo wakiwa sehemu ya wadau katika maendeleo ya Tanzania hawana budi kusimamia uwajibikaji na kusimamia utawala bora ili kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi.
Prof. Assad aliongeza kuwa mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za mradi unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID) katika Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
“Naishukuru sana USAID kwa kufadhili mafunzo haya kwani yanachochea uelewa wa namna bora ya kutafsiri ripoti za ukaguzi na kushughulikia masuala ya maadili yanatokana na ripoti hizo,” aliongeza Prof. Assad.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Mchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Ofisi ya Rais, Bw. Stephene Likunga alimuomba CAG kuendelea kutoa mafunzo hayo kila wakati ili kuwaongezea uwezo wataalam wanaotumia Taarifa za Mkaguzi Mkuu.
“Tunaomba mafunzo haya kuwa endelevu ili kuwa tija katika kuchambua kwa kina taarifa zako kwa kina kwa faida ya umma,” alisema.
No comments:
Post a Comment