Thursday, June 11, 2015

MSUMBIJI YAJA KUJIFUNZA UTEKELEZAJI WA BRN TANZANIA

Ujumbe kutoka Msumbiji umetembelea Makao Makuu yaWizara ya Maji, Ubungo Maji leo kwa nia ya kujifunza na kuelewa utekelezaji wa miradi ya maji kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) nchini.

Lengo kuu la ziara hiyo hapa nchini ni kujifunza namna  Mpango wa BRN unavyotekelezwa nchini Tanzania, hasa mfumo na mbinu katika kufanikisha mpango huo.

Kwa upande wa Sekta ya Maji, ujumbe huo ulikutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Mbogo Futakamba pamoja na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Wizara na kujionea jinsi Wizara hiyo inavyotekeleza mpango huo tangu ulipoanza.
“Wizara ya Maji inafanya bidii kuhakikisha BRN inatekelezwa na Idara na Vitengo vyote Wizarani na sio watu wachache tu, na katika kufanikisha hilo uwezo wa kufanya kazi na kujituma ni muhimu sana kwa kila mtumishi na hili nalisisitiza siku zote”, alisema Katibu Mkuu, Inj. Mbogo Futakamba.

“Pamoja na changamoto za fedha na nyinginezo  hatuna budi kufikia malengo ya BRN, huku tukiweka uwiano mzuri katika upatikanaji wa maji safi na salama na ujenzi wa mifumo mizuri ya maji taka ambayo viko sanjari katika mpango huu”, aliongeza Inj. Futakamba.

Katibu Mkuu aliendelea kusema kuwa ni matumaini yake makubwa ndugu zetu wa Msumbiji watajifunza mengi yenye tija na manufaa makubwa  kwa maendeleo ya Sekta ya Maji na taifa lao kwa ujumla kutoka Tanzania.

Aidha, kiongozi wa msafara wa ujumbe huo kutoka Msumbiji, Christina Matusse, Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango wa Wizara ya Uchumi na Fedha alisema kuwa nchi ya Msumbiji iliyopata Serikali Mpya hivi karibuni, imekuja kujifunza kutoka Tanzania ili nao waweze kutekeleza miradi ya maendeleo nchini mwao.

Huku akisisitiza Tanzania ni mfano mzuri kwa nchi yao katika kujifunza kutokana na kuwa na mipango mizuri na hatua waliyopiga, itaisaidia nchi yao kimaendeleo.

Mpaka sasa BRN imefanikiwa kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi takribani milioni 21.07 waliopo vijijini sawa na asilimia 56.2 na vichoteo vya maji vipya 18,603 vikiwa vimetengenezwa hadi kufikia tarehe 31Mei, 2015.

Ujumbe huo wa Wizara ya Uchumi na Fedha ya Msumbiji, uliowasili jana  unajumuisha Christina Matusse, Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango, Augusta Pechisso, Mkurugenzi wa Sera, Constantino Gode, Mshauri wa Uchumi wa Waziri Mkuu, Elton Cavadias, Msaidizi wa Waziri na Vanessa Mendonca, Msaidizi wa Naibu Waziri, na unategemewa kumaliza ziara yake tarehe 12, Juni.
Ujumbe kutoka Msumbiji (kushoto) na Wakurugenzi wa Wizara ya Maji katika kikao cha pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Mbogo Futakamba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Mbogo Futakamba (katikati), pamoja na Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti wa Presidential Delivery Bureau (PDB), Mugisha Kamugisha (kushoto) na Mkurugenzi wa Maji Vijijini, Frida Rweyemamu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Mbogo Futakamba akizungumza na Ujumbe kutoka kutoka Msumbiji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Mbogo Futakamba akiwa pamoja na Ujumbe wa Msumbiji, Watumishi wa PDB na Wizara ya Maji.

No comments: