Wednesday, June 10, 2015

DKT. BILAL ASAINI MKATABA WA MAKUBALIANO YA SOKO LA PAMOJA, JIJIJINI SHARM EL SHEIKH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisaini mkataba wa makubaliano ya kuwa na soko la pamoja kwa Nchi za Wanachama wa Kanda ya tatu ya Nchi za Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na za Magharibi. Dkt.Bilal pamoja na Viongozi wa Nchi husika wamesaini mkataba huo leo katika Mkutano mkuu wa tatu wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la pamoja la Nchi za Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Sharm El Sheikh, nchini Misri.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza jambo na Waziri wa Afrika Mashariki, Dkt. Harrison Mwakyembe, akimpongeza baada ya kusaini mkataba huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipongezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima, baada ya kusaini mkataba huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa na baadhi ya Mawaziri wake katika mkutano mkuu wa tatu wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la pamoja la Nchi za Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika leo Juni 10, 2015 kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Sharm El Sheikh, nchini Misri. Picha na OMR.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo Jumatano Juni 10, 2015 amemuwakilisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali  unaolenga kuweka saini ya makubaliano ya kuwa na soko la pamoja kwa nchi wanachama wa kanda tatu za Afrika yaani Afrika Mashariki, Nchi za Kusini mwa Afrika na Nchi za Afrika Magharibi, katika mji wa Sharm El Sheikh nchini Misri.

Makamu wa Rais katika mkutano huu amemuwakilisha Rais Kikwete kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo alipata fursa ya kuhutubia kwa niaba ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wengine waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na Rais Robert Mugabe ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa SADC, Rais Abdel Fattah El-Sisi, Rais wa Misri pamoja na watendaji wa SADC akiwemo Dkt. Stargomena Tax na Balozi Richard Sezibera Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Pia mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa COMESA, Rais wa Benki ya Dunia pamoja na wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa yanayohusika na Biashara na Viwanda.

Mkutano huu unafanyika baada ya miaka takribani saba, ambapo wakuu wa nchi katika kanda hizi walipendekeza kuwepo mkakati wa kuwa na soko huru kwa nchi zote 26 na mkakati huu, sasa unasainiwa rasmi katika mkutano wa leo hapa Sharm el Sheikh. 

Katika hotuba yake kwa niaba ya Afrika Mashariki, Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema, nchi zilizopo Afrika Mashariki zimepokea mkakati huu na kwamba ziko tayari kupokea makubaliano kutokana na kubaini faida kubwa ya kuleta uhuru kwa nchi nyingi za Afrika pamoja na kupunguza mipaka ya kibiashara ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiathiri kukua kwa uchumi wa Afrika.

Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua kuwa, ili Afrika iendelee na ili iweze kukabiliana na vikwazo vya kimaendeleo ni lazima kuwepo fursa za kutanua uchumi na hasa kwa kuangalia rasilimali zilizopo Afrika ili ziweze kukuza uchumi wa ndani katika Bara hili. “Hatuwezi kufanikiwa kama kila mmoja atafanya mambo haya kivyake. Lazima kuwepo mtangamano kama huu kwa maslahi mapana ya Afrika,” Mheshimiwa Makiamu wa Rais alisema.

Awali akihutubia mkutano huo, Rais wa Misri Abdel Fattah El Sisi alisema, Misri inajivunia kushiriki katika hatua hii mjuhimu ya kufungua mipaka ya kibiashara katika Afrika na kwamba anatumia nafasi hiyo kuonesha namna nchi yake ilivyo tayari kuhakikisha makubaliano ya Sharm el Sheikh yanafanikiwa. “Nawakaribisha Misri na asanteni kwa kuja, sisi tuko tayari kuhakikisha kuwa nia hii njema ya nchi za kanda hizi tatu inafanikiwa,” alisema Rais Sisi.

Katika mkutano huu, viongozi mbalimbali wamehudhuria na baadhi yao ni Mfalme Mswati III wa Swaziland, Rais Omar al Bashir wa Sudan, Rais Arthur Peter Mutharika wa Malawi, Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemanrian Desalegn na Naibu Rais wa Kenya William Ruto. Viongozi hawa pamoja na wawakilishi wao, wamedhamiria kufungua njia za kuwa na masoko huru ikiwa ni mkakati kukabiliana na ukuzaji biashara na utanuaji wa teknolojia katika nchi za Afrika hasa sasa ambapo nchi katika mabara mengine zimekwisha fikia hatua hii, hali inayozineemesha huku Afrika ikibakia nyuma.

Hata hivyo, wajumbe wengi wa Mkutano huu wanapokea jitihada ya Misri kurejea kwa nguvu katika ukanda wa Afrika kuwa ni mpango maridhwa unaolenga kuongeza nguvu kwa Afrika kwani nchi tajiri za Afrika zinaongezeka na pia aina ya mahusiano inabadilika. Kubadilika huku kwa aina ya mahusiano kunaonesha faraja kwa nchi ambazo hazijatanuka sana kiuchumi na kiteknolojia na kwamba kutaongeza ushindani ndani ya Afrika pamoja na bidhaa za Afrika kupata masoko makubwa ya ndani na nje.

Mheshimiwa Makamu wa Rais yupo katika mkutano huu akiambatana na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Kigoda. Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na msafara wake wanatarajia kurejea nyumbani kesho mara baada ya mkutano huu kuisha jioni ya leo kwa sherehe rasmi ya kuweka saini makubaliano ya utangamano wa utatu wa kanda hizi.

Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Sharm el Sheikh, Misri
Jumatano Juni 10, 2015

No comments: