Na Abou Shatry Washington DC
Watanzania walioko nchini Marekani, wamechangisha zaidi ya Dola 3,550 kwa ajili ya kumsaidia ndugu Moh'd Said Moh'd anayehitaji kwenda nchini India kwa matibabu.
Bi Moza Moh'd Khamis akitoa maelezo machache, Maryam Shaaban kulia, pamoja na Bi Asha Haris, Picha zote na (swahilivilla.blogspot.com)
Akifungua shughuli hiyo iliyofanyika May 17, katika Jimbo la Meryland nchini Marekani na kuzijumuisha jumuiya mbali mbali za Kitanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazanzibari nchini humo (ZADIA) Bwana Omar Haji Ali, alisema kwamba mkusanyiko huo ni kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Katika maelzo yake ya ufunguzi yaliyokamilishwa na dua, Bwana Omar alisisitiza kuwa harambee hiyo iliyofanykika nchini Marekani kwa ajili ya kumsaidia kijana aliyeko Zanzibar, ni uthibitisho kuwa jumuiya za Kitanzania nchini humo zina azma ya kuchangia kidhati katika ustawi wa Tanzania na watu wake.
Mwenyekiti wa Zanzibar Diaspora Association (ZADIA) ndugu Omar Haji Ally akifungua harambee kwa dua.
Mbali na fedha taslimu, baadhi ya wasamaria wema, walichangia vitu vya aina mbalimbali vya Kitanzania ambavyo viliuzwa kwa mnada na kuweka nyongeza kwenye fungu hilo.
Miongoni mwa vitu hivyo ni pamoja na mavazi kama vile kanga, vikoi, kanzu na vyenginevyo, ambavyo vilisasambuliwa chini ya MC Mayor Mlima, Abou Shatry, pamoja na washika fedha katika harambe hiyo Bi Asha Haris na Bi Sarah Towa.
Akizungmza katika shughuli hiyo, mama mzazi wa Moh'd, Bi Moza Moh'd Khamis alielezea shukurani zake za dhati kwa wale wote walioitikia wito wa harambee hiyo. "Nawashukuru ndugu zangu muliokuja hapa kuniunga mkono juu ya swala la huyu mtoto", alisema Bi Moza katika sauti iliyochanganyika na kilio na huzuni za uchungu wa uzazi.
Bi Moza Moh'd Khamis na mumewe Sarai Mfaume Sarai, walipoungana na waTanzania wa DMV katika harambee ya kumsaidia Moh'd Said Moh'd anayehitaji kwenda nchini India kwa matibabu.
Aliendelea kusema kuwa, mtoto wake amekuwa akisumbuliwa na maradhi tangu akiwa na umri wa miaka mitano, na hivi sasa akiwa na umri wa miaka 25, imebainika kuwa mafigo yake yameharibika. Kutokana na hali hiyo, Moh'd aliyeko hospitalini nchini Tanzania, anahitaji kwenda nchini India kwa ajili ya upandikizaji wa figo.
Naye babu wa kijana Moh'd mzee Shaaban Kassim Said, alielezea shukurani zake kwa wale wote walijitokeza katika mkusanyiko huo. Katika dua aliyoitoa ufungaji wa shughuli hiyo, mzee Shaaban alisema kuwa, kamwe hawezi kuwalipa wale wote waliochangia, na kwamba malipo yao yako kwa Mungu.
Mbali na michango iliyokusanywa hapo, Katibu mkuu wa ZADIA Shamis Al Khatry amesema kuwa, bado michango inaendelea kupokelewa, na kwamba wale wote wanaotaka kufanya hivyo wanaweza kuchangia ama kwa fedha taslimu au kwa kupiti gofundme.com
Mzee Shaaban Kassim Said akisoma dua pamoja na shukuran
Katibu mkuu wa ZADIA Shamis Al Khatry akipongeza wanakamati pamoja na kusisitiza michango
Bi Asha Haris pamoja na Bi Sarah Towa wakifanya hesabu za michango
No comments:
Post a Comment