Aprili Mosi kila mwaka huwa ni siku ya kupanda miti kitaifa na mwaka huu 2015 mkoa wa Kagera
ulipewa heshima ya kuadhimisha siku hiyo ambapo iliadhimishwa katika Halmashauri ya Wilaya ya
Missenyi na kushirikisha wadau mbalimbali pamoja na wananchi wanaojihusisha na kupanda miti na
kutunza misitu.
Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Celestine Gesimba kutoka Wizara
ya Maliasili na Utalii ambapo maadhimisho hayo yalianzia katika Kijiji cha Bugolola eneo la Omukajunguti
kwa kupanda miti 2100 kwa kushirikisha washiriki wote na wananchi wa kijiji hicho.
Kauli mbiu ya siku hiyo ilikuwa ni “Misitu ni Mali Panda Miti.” Katika Hotuba yake Naibu Katibu Mkuu
Bw. Gesimba alisema wizara yake siyo kwamba inahamasisha wananchi kupanda miti ili kulinda
mazingira tu bali wananchi wapande miti ili kunufaika nayo kwani ni mali inayoingiza kipato kikubwa
kwa mwananchi mmoja mmoja.
Bw. Gesimba alisema wananchi wanatakiwa kupanda miti kwa wingi kwani miti isipopandwa
itasababisha maafa makubwa hapo mbeleni kama inavyoanza kuonekana kwa sasa mfano, ukosefu wa
mvua au mvua kutonyesha kwa wakati, joto jingi, kuyeyuka kwa theruji mlima Kilimanjaro.
Bw. Gesimba alimalizia hotuba yake kwa kusema kuwa kutotunza misitu kumesababisha baadhi ya
sehemu kuwa jangwa au kusababisha ugonjwa wa malaria mfano Lushoto mkoani Tanga ambako
hakukuwa na ugojwa huo miaka ya 1970 na 1990. Aidha alitahadhalisha misitu kutoweka kabisa kwani
kila baada ya dakika sita (6) nusu kiolmeta ya misitu hutoweka duniani.
Bwana Jaffari Omary Afisa Misitu katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa akitoa salaamu za mkoa wa Kagera
alisema mkoa wa Kagera una jumla ya misitu 17 yenye hekta 341,756.35 pia eneo la misitu na vichaka ni
kilometa za mraba 10,148 sawa na asilimia 35 ya nchi kavu ya mkoa mzima.
Mkoa wa Kagera una misimu miwili ya upandaji miti, msimu wa vuli ambapo wananchi hupanda miti
kwa wingi kutokana na msimu huo kuwa na mvua za kutosha pia na msimu wa masika ambapo nao
hutumika kupanda miti kwa wingi, alifafanua Bw. Jaffari Omary .
Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Kanda ya ziwa Bw. Haji Khatibu akitoa salaam za Kanda ya
Ziwa alisema kuwa kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2003 Kanda ya Ziwa ilionekana kuwa misitu
imebakia mapori tu kutokana na uchomaji moto ovyo, mifugo mingi na wananchi kutoshiriki kuitunza
misitu, uchomaji mkaa, kilimo na uvunaji wa mbao usiozingatia kanuni na taratibu.
Aidha Bw. Khatibu alisema uharibifu wa miti unachangiwa pia na sera mbalimbali kuingiliana na alitoa
mfano katika halmashauri za Wilaya kutoa maeneo ya hifadhi za misitu kwa wananchi kama viwanja vya
kuishi na kuendesha kilimo jambo ambalo linapelekea uharibifu mkubwa katika maeneo hayo ya hifadhi.
Ili kukabiliana na changamoto hizo na kuzipatia ufumbuzi Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea
kuwahasisha wananchi kushiriki katika kuilinda na kuitunza misitu kupita serikali zao za vijiji na vitongoji
pamoja na mwananchi mmoja mmoja kutoshiriki katika vitendo ovu vya kuharibu misitu.
Aidha serikali imekuwa ikiendesha doria katika maeneo ya hafadhi za taifa ili kukabiliana na uvamizi wa
maeneo hayo pia kukamata mazao ya misitu ambayo yanavunwa bila kuzingatia sheria, taratibu na
kanuni za uvunaji na kuwachukulia hatua kali wahusika wanaokamatwa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Missenyi William Katunzi akitoa shukrani zake kwa Wizara ya
Maliasili na Utalii kwa kuadhimisha siku ya kupanda miti kitaifa Wilayani missenyi alisema tayari kwa
mkoa wa Kagera wananchi wanajua nini maana ya kupanda miti kwa sasa, wapanda miti kibiashara ili
kujipatia kipato pia kulinda mazingira.
Takwimu za upandaji na utunzaji wa miti katika mkoa wa Kagera kwa miaka minne mfululizo; mwaka
2011/2012 lengo la kupanda lilikuwa miti 12,500,000 Miti iliyopandwa ni 13,100,875 sawa na asilimia
105, Miti iliyopona ni 11,220,328 sawa na asilimia 89.7. Mwaka 2012/2013 lengo la kupanda lilikuwa
miti 12,500,000 Miti iliyopandwa ni 12,755,042 sawa na asilimia 102, Miti iliyopona ni 11,081,519 sawa
na asilimia 88.
Aidha mwaka 2013/2014 lengo la kupanda lilikuwa miti 13,000,000 Miti iliyopandwa ni 13,767,022 sawa
na asilimia 85, Miti iliyopona ni 11,248,933 sawa na asilimia 88.4. Na mwaka 2014/2015 lengo la
kupanda lilikuwa miti 13,000,000 Miti iliyopandwa ni 12,278,125 sawa na asilimia 98.4, Miti iliyopona ni
11,153,627 sawa na asilimia 90.8
No comments:
Post a Comment