Tuesday, April 14, 2015

BALOZI SEIF ALI IDDI AWAKUMBUSHA WANANCHI KUWAUNGA MKONO VIONGOZI WANAOWASIMAMIA HARAKATI ZA MAENDELEO YAO.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi msaada wa Vipaza sauti Amiri  wa Jumuiya ya Sherehe za Siku Kuu ya Iddi Matemwe Ustaadhi Kundi Choum Haji kutekeleza ahadi aliyoip[a Jumuiya hiyo wakati wa sherehe za siku kuu ya Iddi el Hajj iliyopita.
  Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman  Iddi akimkabidhi  mchango wa Shilingi 400,000/-  kwa kila kikundi miongoni mwa  vikundi 14 vya Ushirika wa Akina Mama vilivyomo ndani ya  Wilaya ya Kaskazini “ A “.
 Balozi Seif akikabidhi Seti moja ya Jezi na Mipira kwa kila Timu ya Soka miongoni mwa timu nne zilizomo ndani ya Jimbo la Matemwe.
 Balozi Seif akiangalia hodhi linalojengwa kwa ajili ya kuhifadhia maji kwenye Msikiti Mkuu wa Kijiji cha Mvuleni Kidoti Jimbo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif akiuagiza Uongozi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Kijiji cha Mvuleni kufanya Tathmini ya uenzi wa Vyoo ili uwahi kufunguliwa katika muda muwafaka uliopangwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Wananchi hasa akina Mama Nchini kuwaunga mkono Viongozi wenye muelekeo wa kuwasimamia vyema katika harakati zao za Maendeleo, kiuchumi na ustawi wa Jamii.

Alisema takwimu ya idadi ya watu  Nchini inaoonyesha wazi kwamba Wanawake ndio wenye uwezo wa kutumia kura zao katika kuchaguwa Viongozi watakaowafaa kwenye maeneo yao kutokana na wingi wao.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati akikabidhi Vipaza Sauti kwa ajili ya Jumuiya ya Kuhifadhi Quran pamoja na Sherehe za Siku Kuu ya Kiislamu  ya Kijiji cha Matemwe Wilaya ya Kaskazini “A”  Mkoa wa Kaskazini Unguja akitekeleza ahadi aliyoitowa wakati wa Siku Kuu ya Mfunguo Tatu uliopita akiwa mgeni rasmi. 

Balozi Seif alisema huu ni mwaka muhimu kwa Taifa la Tanzania ambapo Wananchi wanapaswa kuwa makini katika kufanya uamuzi  muafaka wa kura ya maoni pamoja na uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba.

Alisema uwamuzi wa Wananchi hao  endapo hautazingatia hatma yao ijayo ya miaka mitano kwa kuchaguwa viongozi makini na imara wasijetafuta visingizio vya lawama kwa  viongozi watakaowaweka madarakani.

Mapema Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akitekeleza ahadi  yake ya  kuviwezesha  Baadhi ya Vikundi vya Ushirika vya akina Mama wa  Wilaya ya Kaskazini “A “ alisisitiza umoja na mshikamano miongoni mwa Wananchi wa Wilaya hiyo.

Mama Asha alisema mshikamano huo ndio njia pekee itakayowawezesha wananchi hao kuendelea na shughuli zao za kujitafutia riziki katika hali ya amani na utulivu.

Alitanabahisha kwamba yapo Mataifa kadhaa duniani yakiwemo yale ya Bara la Afrika ambayo baadhi ya wananchi wake walijaribu kuichezea amani na hivi sasa tayari wameshatumbukia katika dimbwi la vurugu zilizozaa maafa  yaliyoacha  makovu yatayoendelea kukumbukwa milele na Mataifa hayo.

No comments: