Mchungaji wa mifugo akinywesha maji mifugo yake kwenye eneo lenye maji ambalo Waizri Prof.
Maghembe amepiga marufuku kunywesha kwenye eneo hilo.
Na Hussein Makame-MAELEZO, Musoma
WAZIRI wa Maji Profesa Jumanne Maghembe amewaonya
wananchi wanaoharibu vyanzo vya maji kwamba kufanya hivyo
kunahatarisha uhai wa vyanzo hivyo.
Ametoa onyo hilo kwa nyakati tofauti wakati akiwa kwenye
shughuli za kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maji
kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya ya Serengeti mkoani
Mara ambako Maadhimisho ya Wiki ya Maji kitaifa yanafanyika.
Akiwa katika kijiji cha Rung’abure, Waziri alishuhudia baadhi ya
wafugaji wakinywesha mifugo yao kwenye maeneo ya vyanzo
vya maji huku baadhi wakilima karibu na chanzo cha maji.
“Jamani mradi huu ni wa kwenu, lakini nilichokiona pale
kwenye chanzo cha maji, nilina ng’ombe kwenye eneo
chepechepe” alisema Waziri Prof. Maghembe na kungeza:
“Jamani fanyeni juhudi au lolote mnalofanya lakini msiingizi
ngombe mule kama mkiingiza basi maisha ya mradi yatakuwa
mafupi na hakuna mtu wa kumlaumu kwa sababu ni nyinyi
wenyewe mmekuwa kama mtu anayekata tawi la mti alilokalia”
Aliongeza kuwa katika eneo la mradi wa Rung’abure kuna
mkulima analima kwenye msitu ulioko karibu na chanzo cha
maji cha mradi wa kijiji hicho, hivyo anahatarisha chanzo hicho.
“Mtu yule tunamuomba mwaka huu avune mazao yake lakini
mwaka kesho asipande pale.Mwenyekiti naomba mumpe
shamba lingine kwa sababi akiendelea kulima hakuna maji
pale” alisema Waziri Prof. Maghembe.
Alifafanua kuwa suala la kuondoka si hiyari kwani hairuhusiwi
kisheria kulima mita 60 kutoka chanzo cha maji, hivyo mkulima
huyo ni lazima aondoke mwakani.
“Hili jambo ninalosema si hiari ni suala la kisheria hairuhusiwa
kulima kwenye chanzo cha maji kwa umbali wa mita 60 na hilo
sio jambo la kumuomba mtu ni jambo la kutekeleza sheria”
alisema na kuongeza:
“Ninachosema yule aliyelima pale mwaka huu avune mazoa
yake mi sina tatizo kabisa baada ya hapo tunamuoba aondoke
pale sheria hii sio ya mwaka huu, wala mwaka jana wala mwaka
juzi na hilo ni sheria imetungwa mwaka ya 2006”
Aliitaka Serikali ya kijiji hicho pia wanasimamia kuhakikisha
ng’ombe hawapelekwi kunywa maji kwenye eneo la chanzo
cha maji badala yake wakanywe maji kwenye mabirika
yaliyojengwa.
Akiwa mjini Mugumu wilayani Serengeti, ambako alitembelea
ujenzi wa chujio la maji ya bwawa la Manchira na baada ya
ukaguzi huo alizungumza na wananchi wa mji huo.
Alisema chujio hilo litachuja maji na kuweka dawa kwenye
maji yanayokwenda mjini na kutatua tatizo la uchafu wa maji
ambalo linawakabili wananchi wa Mugumu.
“Lakini pia niwaombe sana ndugu zangu mtunze sana
mazingira kwani tumeona rasilimali za maji zinapungua sana
ninawaomba mtunze sana vyanzo vya maji mtunze na bwawa
letu la Manchira” alisema Waziri Prof. Maghembe.
Hivyo alisisitiza kuwa ili kuhakikisha bwawa hilo na linaendelea
kutumika kwa kipindi kirefu, kitu kikubwa ni kutunza sana
mazingira ili kiasi cha rasilimali kilichopo kisiendelee kupungua.
Akiwa katika vijiji vya Ligamba A na Mumagunga vilivyoko
wilayani Bunda mkoani Mara, Waziri aliwataka wananchi
wapande miti ili kulinda vyanzo vya maji kwenye maeneo yao.
Alisema utunzaji wa vyanzo vya maji ni jambo muhimu ili
kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji havikauki na kujharibiwa
kwani kufanya hivyo kutahatarisha upatiakanaji wa maji.
Waziri Prof. Maghembe anaendelea na ziara ya kukagua na
kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maji katika vijiji
mbalimbali vya wilaya za mkoa wa Mara ikiwa ni sehemu ya
Maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa.
No comments:
Post a Comment