WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itawasilisha Bungeni
Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wenye sehemu 14 likiwemo
suala la Mahakama ya Kadhi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Magogoni jijini Dar
es Salaam, jana jioni (Jumatano, Machi 11, 2015) Waziri Mkuu alisema
Serikali inakusudia kuwasilisha muswada huo kwenye mkutano ujao wa
Bunge unaotarajiwa kuanza Jumanne ijayo, (Machi 17).
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasihi Watanzania waondoe hofu iliyoenezwa
na tetesi kwamba muswada huo una lengo la kuiingiza mahakama hiyo
kwenye Katiba Inayopendekezwa na kuwataka wazipuuze tetesi hizo.
“Hakuna ukweli wowote kwenye jambo hilo kwa sababu Bunge la Katiba
lilikwishavunjwa na Bunge lijalo halina mamlaka ya kufanya hivyo. Hili
ni Bunge la sasa haliwezi kubadili maamuzi ya awali… Jambo hili halina
ujanjaujanja au njama zozote za kuliingiza Kwenye Katiba
Inayopendekezwa,” alisema.
“Hizo ni hofu za kweli zilizosambaa na inategemea jinsi mtu
alivyoelewa suala zima. Kikubwa ni kutambua kwamba Mahakama ya Kadhi
zimekuwa zinafanya kazi hapa nchini tangu mwaka 2012 lakini kwa
kuendeshwa na wao wenyewe na siyo Serikali,” alisema.
Alisema kinachoombwa kwenye marekebisho hayo ya sheria ni kutambuliwa
kwa maamuzi yanatolewa na Mahakama ya Kadhi pindi yanapofikishwa
kwenye vyombo vya umma au taasisi za Serikali. “Sehemu ya tano ya
muswada huo ndiyo inaongelea Mahakama ya Kadhi. Na mapendekezo yao
yanaomba maamuzi yanayotolewa kuhusu ndoa, mirathi au talaka
yanapokuja kwenye taasisi nyingine yaheshimiwe,” alifafanua Waziri
Mkuu.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema: “Kuna mama mmoja alipewa talaka na
katika maamuzi ya talaka ile, alipaswa kupewa nyumba. Alipokwenda kwa
Kamishna wa Ardhi ili abadilishe jina kutoka majina ya awali na kuwa
la huyo mama akaulizwa haya maamuzi yametolewa wapi, sisi
hatuyatambui… hili lilileta usumbufu mkubwa kwa wahusika.”
Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu alisema kwa mara ya kwanza, suala la
Mahakama ya Kadhi liliibuliwa mwaka 1998 na Bw. Augustine Lyatonga
Mrema na Bw. Yusuph Ramia (marehemu) ambao walitaka Bunge lijadili
hoja yao ya kutaka Serikali ianzishe mahakama hiyo.
“Bunge liliunda Kamati iliyoongozwa na Bw. Arcado Ntagazwa na baada ya
mjadala mrefu halikufikia tamati. Serikali ikalifuatilia lakini pia
haikufikia mwisho. Mwaka 2005 likaingizwa kwenye Ilani ya Chama cha
Mapinduzi na Chama kikaitaka Serikali ifuatilie kuona tatizo ni nini.”
“Kwenye mkutano wa Bunge la Bajeti, tarehe 30 Juni 2009, Waziri wa
Katiba na Sheria ndiye alikuja na hiyo hoja na kuahidi kuifuatilia
Reinstatement Act ya mwaka 1964 sura ya 375 na kuona Serikali itafanya
nini katika suala hilo.”
“Wakati huo ndiyo nilikuwa nimeteuliwa Uwaziri Mkuu kwa hiyo nikaanza
nalo kwa kuunda timu ya viongozi wa dini ili tulijadili kwa kina suala
hili kwani kama Serikali kuna masuala ambayo inaamini ni lazima
iendelee kuyasimamia na kubwa likiwa ni amani na utulivu wa nchi
yetu,” alisema.
Alisema katika vikao hivyo walikubaliana kwamba kuendelea kudai suala
hilo liingizwe kwenye Katiba haikuwa sahihi kwa sababu ni suala la
imani zaidi na kwa msingi huohuo, walikubaliana kwamba zianzishwe na
wao wenyewe na kisha wazipangie majukumu ni nini zitafanya.
“Tulikubaliana kwamba mahakama hizo zisiguse masuala ya jinai bali
zihusu masuala ya binafsi tu ambayo ni ndoa, talaka, mirathi, malezi
ya watoto na wakfu. Tulisema jambo hili liwe ni la hiari na lisiwe la
lazima,” alisema.
“Msingi wa mjadala ulikuwa mahakama hizi zisiwe kama Mahakama ya Ardhi
au Mahakama ya Biashara kwamba mishahara na ofisi zao vigharimiwe na
Serikali, hapana… kwa hiyo fikra kwamba Serikali ilikuwa inakataa
kuzianzisha hazikuwa sahihi. Ndiyo maana Waislamu walikubali
kuziansisha kwa hiari yao wenyewe na kwa gharama zao wenyewe,”
alisema.
“Nimeongea na Kadhi Mkuu hivi majuzi akaniambia kwamba hadi sasa
mahakama hizo zimekwishaamua kesi zisizopungua 2,000 na zisizozidi
3,000.”
Akielezea juhudi za kukutana na wadau wa pande zote mbili, Waziri Mkuu
alisema Februari 3, mwaka huu alikutana na Kamati ya Amani ya Mkoa wa
Dar es Salaam yenye wajumbe 25 ambao ni Waislamu na wajumbe 25 ni
Wakristo lakini katika kikao hicho walihudhuria wajumbe 55.
“Wao walijadiliana peke yao, kisha wakakutanisha pamoja na mimi
nikapewa majumuisho ya mkutano huo. Lakini wakashauri kwamba uitishwe
mkutano mkubwa zaidi wenye wadau kutoka nchini nzima ili nao wajadili
suala hili. Ndipo Machi 3, mwaka huu nikakutana na Kamati ya Maadili
na Haki za Binadamu iliyokuwa na wajumbe 55 wa taasisi tofauti za
Kiislamu na wajumbe 34 wa Madhehebu ya Dini ya Kikristo.”
“Mkutano ulikuwa mkali na ubishani mwingi wengine wakidhani kwamba
wameitwa kushiriki kikao hicho ili kubariki suala la Makahama ya Kadhi
liingizwe kwenye Katiba inayopendekezwa lakini hatimaye, tulielewana
na kufikia muafaka juu ya marekebisho yanayotarajiwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment