Warsha ya wataalam wa misitu imeazimia kuwa kitajengwa Kituo cha Kuendeleza Misitu katika Nyanda za Juu Kusini ili kutoa mafunzo ya ngazi ya VETA kuhusu uendelezaji wa mashamba na viwanda vya misitu. Kituo hicho kitatoa mafunzo ya darasani pamoja na nje ya darasa kwenye misitu na viwanda.
Azimio hilo linasisitiza zaidi kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Programu ya Panda Miti Kibiashara, itahakikisha kuuundwa kwa Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) kwa manufaa ya kituo hicho, na kuwa Umoja huo utamwajiri Mratibu ambaye ataongoza kituo hicho.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Bi Gladness Mkamba, mwishoni mwa Warsha ambayo ilifanyika Iringa katika kituo cha VETA tarehe 10 Machi 2015.
Warsha hiyo ambayo iliandaliwa na Programu ya Panda Miti Kibiashara ili kupokea na kuidhinisha taarifa ya mtaalam mwelekezi Bw Peter Shepherd kutoka Australia, kuhusu kukifufufa upya kituo cha Wafanyakazi wa Misitu kilichoko Sao Hill mkoani Iringa.
Kituo hicho kilijengwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 1992 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wanfanya kazi wa misitu, mafunzo ambayo yalitolewa kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Sweden (kupitia Shirika la SIDA). Hata hivyo kituo hicho kilifungwa mwaka 2002 kutokana na uhaba wa fedha za kukiendesha.
Awali, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, ambaye pia ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Warsha hiyo, alisema kupitia hotuba ya ufunguzi ambayo aliisoma kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utali, kuwa mafunzo ya ngazi ya VETA yanahitajika zaidi sasa kwa kuwa shughuli za kupanda miti na kuchakata mazao ya misitu viwandani zimeongezeka zaidi, hususan katika Nyanda za Juu Kusini.
Vilevile, katika hotuba ya ufunguzi Bi Mkamba alisema kuwa utafiti kuhusu ufufuaji wa Kituo cha Sao Hill unaenda sambamba na matakwa ya Sera ya Taifa ya Misitu. Aliwakumbusha washiriki wa Warsha kuhusu vifungu vya 33 na 34 vya Sera hiyo ambavyo vinasisitiza kuhusu mafumzo ya misitu na uendelezaji wa raslimaliwatu katika Sekta ya Misitu.
Mkurugenzi alisisitiza kuwa ‘utafiti uliofanyika pamoja na warsha hii ni sehemu ya hatua za utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Misitu ambao ulikuwa unasubiriwa sana’.
Lifuatalo ni Azimio kamili la Warsha:
i. Kituo cha Kuendeleza Misitu kitajengwa katika Nyanda za Juu Kusini ili kutoa mafunzo ya kuendeleza misitu na kuchakata mazao misitu katika ngazi ya VETA 1, 2, 3 .
ii. Mafunzo hayo yatafanyika darasani na nje kwenye misitu na viwanda vya misitu.
iii. Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) utaundwa ambao utajumuisha viwanda, wakulima wa miti, wafadhili, na serikali ili kuwezesha mafunzo ya kuendeleza misitu na kuchakata mazao misitu katika ngazi ya VETA 1, 2, 3 .
iv. Ushirikiano wa PPP utaongozwa na Bodi ya Wakurugenzi ambayo itakuwa na wawakilishi kutoka serikalini na wadau wengine.
v. Mafunzo yataandaliwa kwa ushirikiano na Chuo cha Misitu Olmotomnyi (FTI), Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) na wadau wengine wanaohusika na mafunzo.
vi. Kituo kitaongozwa na Mratibu ambaye ataajiriwa na PPP na sehemuyake ya kazi itakuwa katika Nyanda za Juu Kusini.
vii. Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Programu ya Panda Miti Kibiashara, itahakikisha na kuwezesha kuuundwa kwa Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) kwa manufaa ya kituo hicho.
PROGRAMU YA PANDA MITI KIBIASHARA
No comments:
Post a Comment