Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei nchini kwa mwezi Februari, 2015. Kulia kwake ni Kaimu Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa kazini wakati Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu akizungumza nao leo jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa ya kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei nchini kwa mwezi Februari, 2015. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO).
Na Veronica Kazimoto,
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Februari, 2015 umeongezeka kwa asilimia 4.2 kutoka asilimia 4.0 mwezi Januari mwaka 2015.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambapo amesema kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, 2015 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2015.
“Kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari, 2015 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Februari, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014, amesema Kwesigabo”.
Bidhaa za vyakula zilizoonyesha kuongezeka mwezi Februari, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014 ni pamoja na bei za mchele (asilimia 18.5), unga wa mihogo (asilimia 9.3), nyama (asilimia 8.9), samaki (asilimia 12.4) na maharagwe kwa asilimia 7.1.
Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoonyesha kuongezeka mwezi Februari, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014 ni pamoja na bei za mavazi ya wanaume (asilimia 4.7), mavazi ya wanawake (asilimia 3.3), mkaa (asilimia 5.1), mashuka (asilimia 3.1) na gharama za kumuona daktari kwa asilimia 11.2.
Akizungumzia kuhusu Mfumuko wa Bei kwa kipimo cha mwezi Mkurugenzi Kwesigabo amesema kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari, 2015 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 1.6 ukilinganisha na ongezeko la asilimia 1.0 mwezi Januari, 2015.
Aidha, Kwesigabo amesisitiza kuwa Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi kufikia 154.83 mwezi Februari, 2015 kutoka 152.43 mwezi Januari, 2015 ambapo kuongezeka kwa fahirisi kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.
Kwa upande wa thamani ya shilingi, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo amesema uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 64 na senti 59 mwezi Februari, 2015 kutoka mwezi Septemba, 2010 ikilinganishwa na Shilingi 65 na senti 60 ilivyokuwa mwezi Januari, 2015.
Hata hivyo, Mfumuko wa Bei nchini Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari, 2015 nchini Uganda umeongezeka hadi asilimia 1.4 kutoka asilimia 1.3 mwezi Januari, 2015; na nchini Kenya, Mfumuko wa Bei wa Mwezi Februari, 2015 umeongezeka hadi asilimia 5.61 kutoka asilimia 5.53 mwezi Januari, 2015.
No comments:
Post a Comment