Mke wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Lindi Mjini Mama Salma Kikwete akipokewa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Mwantumu Mahiza mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Lindi tarehe 15.3.2015 kuanza ziara ya kikazi ya siku 5 kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Mwantumu Mahiza akisisitiza jambo wakati akiwahutubia mamia ya wana CCM na wananchi wa Lindi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Mikumbi katika Manispaa ya Lindi tarehe 16.3.2015.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipokea kadi kutoka kwa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kata ya Tulieni Mjini Lindi wa Chama Cha Wananchi (CUF) Ndugu Shaibu Rajabu Matola (Kikaptura) aliyeamua kukihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi wakati wa mkutano mkubwa uliofanyika kwenye Kata ya Mikumbi tarehe 16.3.2015.
Mjumbe wa NEC Taifa ya CCM na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimkabidhi kadi ya CCM Ndugu Shaibu Rajabu Matola mara baada ya kujiunga na chama hicho. Ndugu Matola ni miongoni mwa vijana 200 waliojiunga na Chama Cha Mapinduzi na kukabidhiwa kadi katika mkutano huo.
Mjumbe wa NEC Taifa ya Chama Cha Mapinduzi na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwahutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Lindi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Mikumbi tarehe 16.3.2015.
Taswira mbalimbali za mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Mikumbi, Manispaa ya Lindi na kuhutubiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete tarehe 16.3.2015.
Mke wa Rais na Mjumbe wa NEC Taifa Mama Salma Kikwete akikabidhi bati 100 na vifaa vya bendi kwa uongozi wa Shule ya Sekondari Angaza iliyoko katika Manispaa ya Lindi tarehe 16.3.2015. Anayepokea kwa niaba ya shule hiyo ni Mkuu wa Shule Mwalimu Upendo Muro (wa tano kutoka kulia) akiwa pamoja na Ndugu Ashimun Mzava, Afisa Elimu Sekondar, Manispaa Lindi wa nne kutoka kulia) na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo. Aliyesimama wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Lindi Bwana Abdallah Ulega.
PICHA NA JOHN LUKUWI
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewaomba wananchi kuipigia kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa kwa kuwa ni bora na imezingatia mahitaji ya makundi yote ya jamii.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa ombi hilo jana wakati akiongea na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika tawi la Mikumbi Magharibi kata ya Wailes wilayani humo.
Alisema katiba inayopendekezwa ni ya watanzania wote na imegusa maeneo yote muhimu kwa ustawi wa wananchi, inazungumzia haki za wanawake, wazee, wavuvi, watoto na watu wenye mahitaji maalum.
“Katiba iliyopo sasa nayo ni bora, lakini hii inayopendekezwa ni bora zaidi kwani imezitaja haki za mwanamke, mtoto, kijana,mzee na watu wenye mahitaji maalum lakini katika katiba hii ya sasa makundi haya hayatajwi. Msipoteze nafasi, siku ikifika jitokezeni kwa wingi mkaipigie kura ya ndiyo”, Mama Kikwete alisema.
MNEC huyo pia aliwahimiza wananchi hao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kuipigia kura katiba inayopendekezwa na kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu wa kumchagua Diwani, Mbunge na Rais.
Alisisitiza, “Zoezi hili la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura ni jipya, hata kama unakitambulisho cha zamani ni lazima ukajiandikishe ili uweze kupata kitambulisho kipya kwakuwa hicho cha zamani hakitatumika tena”,.
Kuhusu maambuki ya Virusi Vya Ukimwi alisema ni tatizo na kuwasihi wananchi hao kujilinda na kutoruhusu ugonjwa huo usio na kinga wala tiba kuingia ndani ya nyumba zao.
“Hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika nchi yetu inazidi kupungua kutoka asilimia 7.8 kwa mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka 2014, hadi sasa jumla ya wananchi milioni 24 wamepima VVU kwa hiari.
“Kupima kwa hiari kutakusaidia kujua kama unamaambukizi au la, na ikiwa utakuwa na maambukizi utatumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa na kuchukua tahadhari ili usiwaambukize wengine na kama hauna maambukizi utajikinga”, Mama Kikwete alisema.
Akiwasalimia wananchi waliohudhuria mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza aliwasisitiza wazazi na walezi kuona umuhimu wa kusimamia elimu ya watoto wao kwani wakisoma wataweza kuzitumia fursa za kitaalam zinazopo mkoani humo.
Alisema hivi sasa shule za msingi na Sekondari ziko nyingi lakini cha kushangaza kuna baadhi ya wazazi hawataki kuwapeka watoto wao shule.
Mahiza alihimiza, “Kwa yeyote anayejijua ana mtoto nyumbani ambaye amefaulu mtihani wa darasa la saba na hataki kumpeleka shule ajiandae kwakuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, natoa angalizo ifikapo ijumaa ya wiki hii watoto hawa wawe shuleni kwani elimu ni mkombozi wa maisha yao”, .
Katika mkutano huo wanachama wapya 202 walijiunga na Chama Cha Mapinduzi kati ya hao wawili walitoka Chama cha Wananchi CUF.
Wakati huo huo MNEC Mama Kikwete alitembelea kwa nyakati tofauti matawi ya Mmongo, Majani Mapana na Mikumbi Magharibi na kuongea na viongozi wa Halmashauri kuu ya matawi mambo mbalimbali yahusuyo chama hicho .
Aliwataka wajumbe kuwahimiza wananchi wawe na utamaduni wa kufuga kuku wa asili (kienyeji) kwa kila kaya kwa kufanya hivyo itawasaidia kukuza uchumi wao na familia zao na hivyo kujikomboa kutoka maisha ya umaskini.
Mama Kikwete alisema ufugaji wa kuku wa asili hauna gharama kwani kuku mwenyewe anajitafutia chakula, mfugaji atakachompa ni mtama au pumba kidogo na maji ya kunywa pia nyama yake ni tamu na haina madhara kiafya ukilinganisha na kuku wa kisasa.
Alisema, “Ufugaji wa kuku una faida licha ya kuwa ni kitoweo bali pia ni biashara, hivi sasa kuku mmoja anauzwa shilingi 12000 hadi 15000, ukiuza mmoja ada ya shule itapatikana na mtoto atasoma na wewe mwenyewe utavaa. Jitahidini kila kaya iwe na kuku japo 20”,.
Kwa upande wa ardhi aliwasisitiza kutokubali kuuza maeneo yao kiholela kwani maeneo mengi yako karibu na Bahari ya Hindi na thamani yake ni kubwa hivyo basi wayatunze yatawasaidia katika siku zijazo .
Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za CCM ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment