Sunday, January 11, 2015

UNAPONUNUA KIWANJA/NYUMBA HAKIKISHA MKE WA MNUNUZI ANASAINI DOCUMENT HII, USITAPELIWE.

Na   Bashir   Yakub
Wakati mwingine migogoro ya ardhi inasababishwa na kutojua. Wengi hawajui taratatibu na ndio maana hujikuta wanainga katika matatizo. Moja ya maeneo ambako watu wamekuwa wakipatia matatizo ni huu wakati wa kununua.  Yapo mambo mengi unapoununua ardhi, nyumba au kiwanja ambayo wewe kama mnunuzi unatakiwa kuyajua na kuyazingatia ili usiingie katika matatizo.  Nimefanya utafiti katika  kesi za  ardhi mahakamani na kugundua kuwa  moja ya eneo baya linalowaingiza watu mkenge ni hili la  mume kuuza nyumba au kiwanja  bila kupata ridhaa ya  mke wake . Ikumbukwe kuwa  suala la ridhaa hapa sio suala la hiyari isipokuwa ni suala la lazima na la kisheria ambalo kutolitekeleza kwake kunaweza kupelekea mnunuzi kupoteza kile alichokinunua. Ni hatari ndugu na umakini unahitajika.Mume anapouza nyumba/kiwanja kuna kitu huitwa ridhaa ya mwanandoa ambacho ni lazima akisaini, tutaona.
NINI   MAANA   YA  RIDHAA YA MWANANDOA.
Ridhaa ya mwanandoa(Spouses consent) ni ridhaa ambayo anapaswa kuitoa mwanandoa inapokuwa inauzwa mali( nyumba/kiwanja/shamba) ambayo mwanandoa naye ana maslahi au anaimiliki  kwa pamoja na  mme wake au mke wake. Ridhaa hii pia huweza kutolewa na  mume  iwapo anayeuza ni mke na huweza kutolewa na mke iwapo anayeuza ni mume. Ni hatua ya lazima unapokuwa unanunua nyumba , kiwanja au shamba.

KWANINI  MUHIMU  ZAIDI  MKE KUTOA  RIDHAA.
Hapo juu tumeona kuwa  pia mume anatakiwa kutoa ridhaa iwapo mke ndiye anayeuza halafu tukaona kuwa  pia mke anatakiwa kutoa ridhaa iwapo mme ndiye anauza. Lakini utashangaa katika makala yangu naongelea zaidi mke kutoa ridhaa mume anapouza. Ninamuongelea mke kutoa ridhaa zaidi kwakuwa  utafiti unaonesha kuwa migogoro mingi katika  hatua hii imetokea baada ya  mume kuuza bila ridhaa ya mke. Wanaume wengi ndio huwazunguka wake zao na kuuza.Hii ndio  maana hata kichwa cha mada hii kinaongelea zaidi  mume kuuza bila ridhaa ya mke kwakuwa hapa ndipo penye tatizo.
NI  NYUMBA/KIWANJA  GANI  AMBACHO LAZIMA  MUME  KUPATA  RIDHAA YA MKE.
Nyumba au kiwanja ambacho mume ni lazima kupata ridhaa ya mke  ni ile ambayo  wanaimiliki kwa pamoja. Wanayoimiliki kwa pamoja ni  ile ambayo wamejenga kama wanandoa au kununua  wakati wakiwa katika ndoa na  ile ambayo  mke wakati wa kuolewa amemkuta nayo mwanaume lakini wakati wakiwa wote katika ndoa kuna maendelezo yoyote  waliyofanya hata yawe kiduchu. Kununua pamoja si lazima iwe huyu analeta hela na huyu analeta hela hapana  hata kukaa nyumbani kupika, kufagia  halafu mwanaume akatafuta hela na kununua ni kuipata pamoja na haiwezi kuuzwa bila ridhaa ya mke.
JE  NYUMBA  IKIWA KATIKA  JINA   LA  MUME NI  LAZIMA  KUPATA  RIDHAA  YA  MKE.
Ndio hata  kama ipo katika jina la mume ni lazima kupata ridhaa ya mke. Nyumba au kiwanja kuwa katika jina la mume haiondoi matakwa ya sheria ya kuwa ni ya wote . Kuwa katika jina la mume ni  taratibu tu lakini  bado inakuwa ni ya familia au ya wote. Hapa wanaume huwalaghai wanunuzi kwa kuonesha majina yao kwenye hati ili wauze bila ridhaa ya wake. Mnunuzi usidanganywe na jina kwenye hati.
DOCUMENT  YA  RIDHAA  YA MWANANDOA   IWE  NA  VITU GANI.                                          
Document ambayo inaitwa ridhaa ya mwanandoa ambayo wakati unauziwa kiwanja au nyumba ni lazima mke aisaini inakuwa  na jina la mke wa muuzaji, ikieleza dini yake, anuani yake na ikiapa kuwa yeye ni mke halali wa muuzaji fulani fulani. Baada ya hapo  kutakuwa na kipengele  ambacho mwanamke ataapa kwa kutoa ridhaa yake  ya kumruhusu mume wake kuuza nyumba au kiwanja  na atakitaja hicho kiwanja/nyumba  namba zake(plot no) na eneo kilipo ikiwa ni pamoja na kiasi  cha mita kama ni kiwanja. Baada ya hapo atasaini kwa chini na kuandika jina lake na mume wake muuzaji ataandika jina lake naye atasaini.
NINI   KITATOKEA   MKE   ASIPOSAINI  DOCUMENT   YA   RIDHAA YA KUUZA NYUMBA/KIWANJA.
Ni rahisi tu kuwa  unaponunua nyumba ambayo iko katika mazingira kama niliyoeleza bila mwananke kusaini ridhaa ya mwanandoa wewe mnunuzi unakuwa umepoteza kwakuwa  ununuzi  huo ni batili na mda wowote mke akiamua  kurudisha ile nyumba anairudisha  na mnunuzi unapata  hasara.

UFANYE  NINI  MNUNUZI  ILI  KUEPUKA HILI.
Wanaume wengi ni wajanja na wanauza  nyumba viwanja  bila kujali hili   na matatizo utayapata mnunuzi baadae. Na si rahisi mume akwambie ukweli kuhusu hili akishafanya maamuzi ya kuuza na hivyo usitegemee kumuuliza ili upate ukweli. La kufanya ni kuwa hakikisha unapepeleza kama muuzaji mume ana mke na ukijua ana mke hakikisha mwanamke anasaini hiyo document bila kujali ile mali inayouzwa ni yao wote au ya mume peke yake ili kuwa upande salama zaidi. Wewe mnunuzi huwezi kujua imepatikanaje hayo ni yao wanan doa yatakuchanganya. Sasa ili kuweka mambo sawa iwe yao wote au  hapana we muombe tu muuzaji mke wake asaini nyaraka ya ridhaa kwakuwa kwa kufanya hivyo hapotezi lolote kama kweli hakuna jambo analoficha au kama hakuna utata. Narudia tena, usijaribu wala  usinunue  nymba au kiwanja  kwa mume bila mke wake kusaini  ridhaa ya mwanandoa utapata matatizo  sana  na ulichonunua ipo siku tu kitarudishwa na wewe utapoteza, ni hayo kwa leo.
MWANDISHI  WA  MAKALA  HAYA  NI MWANASHERIA  NA  MSHAURI  WA SHERIA  KUPITIA  GAZETI LA  SERIKALI  LA  HABARI  LEO  KILA  JUMANNE, GAZETI JAMHURI  KILA JUMANNE   NA  NIPASHE KILA  JUMATANO.

0784482959,  -0714047241 bashiryakub@ymail.com

2 comments:

Anonymous said...

Kwa kweli hapa mwanasheria umeongea jambo zuri sana, Wanaume wengi huwa tunachukua uamuzi bila kuwashirikisha wake zetu. Pia kuna usemi ambao sio rasmi kuwa mume ni kichwa hivyo mwanamke hana maamuzi yeyote yale.Hata ndugu husema inaonekana mwanaume huna sauti mbele ya mke wako au umekamatwa yaani umepewa limbwata kwa kupata ridhaa ya mke kwa jambo lolote lile.

Unknown said...

Shukrani sana