Na Bashir Yakub
Mara
nyingi nimekuwa nikiandika kuhusu masuala muhimu kuhusu ardhi hasa namna ya kuandika mikataba mtu anapokuwa ananunua nyumba/kiwanja , hadhi
ya mikataba hiyo kisheria, na ubora wake.
Pia nimeandika mambo mbalmbali kuhusu
namna ya kununua nyumba au kiwanja kwa usalama ili watu wasitapeliwe. Nikasema
suala si tu kununua kile unachokipenda na kuondoka isipokuwa ni kununua na
kuwa salama na ulichonunua bila hatari ya kukumbana na mgogoro mbeleni.
Lengo la haya yote ni katika kuhakikisha watu hawatapeliwi na hivyo
kupoteza fedha walizochuma kwa
jasho.Lengo lingine ni kuwaepusha wanunuzi
na hatari ya kuingia mahakamani ambako kuna usumbufu mkubwa na panapoteza fedha na muda
sana tena sana, naongea hili kwa uzoefu.
Leo pia nasisitiza tena kuwa ili ununue kiwanja au nyumba na uepuke kabisa kupata mgogoro
hakikisha unafuata taratibu zote za
msingi na za kisheria ikiwemo kuhakikisha
unaandaa mkataba wenye hadhi ambao
hata likitokea tatizo basi mkataba uwe ndio mlinzi wako. Aidha leo naongelea tatizo lingine tena katika masuala hayahaya ya manunuzi ya viwanja na nyumba. Naongelea
fedha ambayo serikali za mitaa wamekuwa wakiichukua kutoka kwa watu wanaouziana ardhi.
Hatua
hii ya serikali za mitaa
kuchukua fedha kutoka kwa
wanaouziana viwanja au nyumba
limekuwa la kawaida sana. Kitu hiki kipo muda mrefu sasa lakini hakuna anayekemea
au hata kusema.
Watu
wanauziana kiwanja au nyumba serikali za
mitaa wanawaambia kuwa mnatakiwa kulipa
asilimia kumi kama ada ya mauziano .Asilimia kumi ni hela nyingi sana kwakuwa kama nyumba imeuzwa
milioni mianne asilimia kumi ni sawa na milioni arobaini.
Zipo serikali za mitaa nyingine ambazo wakati
mwingine hudai chini ya hizo lakini mara
kwa mara asilimia kumi ndio huwa
inaombwa. Kinachouma zaidi hawa jamaa wa serikali za mitaa huwa
wanalazimisha kutolewa kwa fedha hizo.
Hufikia hadi hatua ya kutoa vitisho na ikitokea kuwa mtu ameuza bila kuwa
taarifu ili wachukue hela basi
wanamjengea uadui na hata yule
aliyenunua naye anajengewa uadui.
( 2 ) ASILIMIA KUMI YA SERIKALI ZA MITAA
HAIPO KISHERIA.
Ni jambo la kushangaza sana. Hakuna sheria yoyote katika nchi hii
ambayo inatambua asilimia kumi. Hili ni jambo la kuzuka tu na limeanzishwa kwa matamanio(tamaa) ya watu.
Narudia tena hakuna katika sheria yoyote
ya nchi hii inayosema kuwa watu wanapouziana kiwanja au nymba inatakiwa muuzaji au mnunuzi alipe asilimia kumi
serikali za mitaa.Asilimia kumi ni mradi
wa watu tu ambao wamekubaliana ili kujipatia kipato.
Ni mradi ambao umeanzishwa kwa muda sasa na umekuwa
ukirithishwa kizazi hadi kizazi. Natoa
changamoto( challenge) ukimuona kiongozi yoyote wa serikali za mitaa kwa
nia njema tu muulize asilimia kumi wanayotoza
au gharama yoyote ile wanayotoza wakati wa mauzo ya viwanja na nyumba inapatikana katika sheria ipi. Namba yangu ya
simu iko chini hapa akikupatia sheria hiyo nijulishe. Kwa uhakika hatopata kitu
kama hicho kwa kuwa ni kitu ambacho
hakipo.
( 3 ) KAMA ASILIMIA
KUMI HAIPOI KISHERIA BASI NININI ?.
Jibu
ni rahisi kuwa asilimia kumi au malipo
yoyote unayoyatoa serikali za mitaa
wakati wa ununuzi wa nyumba/kiwanja ni
rushwa. Ni rushwa na ni ufisadi. Ifahamike wazi kuwa viongozi wa serikali za
mitaa ni watumishi wa serikali. Fedha yoyote
ambayo hulipwa serikalini ni lazima iwe imeainishwa katika sheria fulani.
Hakuna malipo yoyote
kwa serikali ambayo hutolewa bila ya kuwa
yameainishwa pahala fulani. Pili fedha
yoyote halali inayolipwa kihalali katika mamlaka yoyote ya serikali ni lazima itolewe risiti ya serikali.
Inatolewa risiti ya serikali ikiwa na
maana kuwa inatambuliwa na serikali , itakwenda serikalini na matumizi yake yatakaguliwa na serikali. Fedha yoyote inayotolewa kwa serikali bila aliyetoa
kupewa risiti ni fedha ambayo ina ufisadi ndani yake.
Na katika maana hiyo ni kuwa
unapolipa fedha serikali za mitaa
kwasababu yoyote ile kuhusu kufanyika kwa
mkataba wa manunuzi ya kiwanja/nyumba
unakuwa umetoa rushwa ndugu na
kama utachukuliwa hatua utatakiwa kujibu mashtaka ya kutoa rushwa. Kutoa
rushwa nako ni kosa si kupokea tu ndio kosa.
Kiongozi wa serikali za mitaa anayeomba
na kupokea fedha hizo anakuwa ameomba na
kupokea rushwa. Na ndio maana fedha hizi
hazitolewi risiti. Kama kuna mtu aliwahi
kunua ardhi na akalipa fedha serikali za mitaa na akapewa risiti atanipigia
simu aniambie. Hakika hakuna na kama ulipewa
ilikuwa ya kuzuga tu kwa kuwa hakuna risiti ya malipo hayo.
( 4 ) UNAPONUNUA KIWANJA/NYUMBA
SI LAZIMA KUWASHIRIKISHA SERIKALI ZA
MITAA.
Kisheria
unaponunua kiwanja au nyumba pahala fulani suala la kuwashirikisha serikali za mitaa ni hiyari
yako. Mtu asikulazimishe eti ni lazima serikali za mitaa wawepo. Na hata
wakiwepo uzito wao kama itatokea mgogoro
ni sawa na uzito wa shahidi mwingine yoyote ambaye ungeenda naye katika
mauziano.
Mahakamani serikali za mitaa ni shahidi sawa na shahidi ambaye si kiongozi
wa serikali za mitaa kama itatokea mgogoro. Ieleweke kuwa wanaouziana wanao
uhuru kisheria kabisa kuwashirikisha serikali za mitaa au kutowashirikisha. Serikali
za mitaa hulazimisha kuingia katika manunuzi
ili wapate chao.
Basi wanunuzi mjue kuwa kutowashirikisha serikali za
mitaa katika kununua haiondoi uhalali wa
ulichonunua na wala haikipunguzii hadhi hata chembe kisheria ulichonunua.Hapa
naongelea sheria na hivi ndivyo ilivyo.Wasikulazimishe kuwashirikisha au kutoa hela.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA
NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA
SERIKALI LA HABARI LEO KILA
JUMANNE, GAZETI JAMHURI JUMANNE, NA GAZETI NIPASHE JUMATANO.
0784482959
0714047241
bashiryakub@ymail.com
1 comment:
afadhaki umetuelimisha mwanasheria maana tulikuwa tunapigwa kweli na hawa watendaji, naomba uendelee na moyo wako wa kizalendo kuelimisha watanzania juu ya haki zao za msingi, may God bless u..
Post a Comment