Mshambuliaji Hamis Tambwe amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuchukua
hatua stahiki dhidi ya wachezaji wa Ruvu Shooting kwa kitendo cha kumshambulia na kumtolea lugha
chafu uwanjani ikiwemo kumbagua kwa kumuita mkimbizi.
Akizungumza Makao Makuu ya klabu ya Yanga iliyopo mtaa wa Twiga na Jangwani leo, Tambwe
alisema kuwa kitendo alichofanyiwa ni cha kinyama na anakilaani kwa nguvu zote, na anataka aelezwe
wazi iwapo wachezaji kutoka mataifa mengine hawatakiwi kucheza Tanzania.
"Uwanja wa Taifa kuna kamera, matendo mengi sana mabaya tumekuwa tukifanyiwa wachezaji wa
kigeni, naamini baada ya mchezo TFF wanakaa kupitia mikanda ya mchezo wanaona kila kitu lakini
hakuna adhabu zinazochukuliwa tunavyodhalilishwa na kubaguliwa.
"Nimetukanwa, nimeitwa Mkimbizi, nipo nchini kihalali na nafanya kazi kwa kufuata sheria zote kwa
nini waniite mkimbizi, nipo tayari kusema matusi waliyonitukana kwa mabosi wangu na kwa TFF ili
hatua stahiki zichukuliwe, mpira sio vita, mpira ni burudani, mpira ni 'fair play', lakini hapa imekuwa ni
tofauti.
"Kitendo walichonifanyia ni sawa na kunishikia bastola, ni unyama wa hali ya juu walitaka kuniua, yani
wamenikaba nilikuwa naona roho yataka toka, hatukuwa vitani walitakiwa wacheze mpira wa
'profesional' hivi tutaogopa kucheza Tanzania."alisema kwa masikitiko.
"Hawakuja kucheza soka, walikuja kupigana, walinipiga kiwiko, wakanipiga ngumi na mwisho
walinikaba shingoni nikaona pumzi zinataka niishia.
Hii ni hatari, kuna mtu anaweza kuanguka akapoteza maisha siku moja. Wale wanajeshi hawaingii
uwanjani kucheza soka, wanakwenda kucheza na mwili wa wachezaji wenzao.
"Maneno makali waliyonitamkia yananiuma sana roho hadi sasa, wameniita mkimbizi, eti nimekimbia
vita nyumbani Burundi, vita hata hapa inaweza kutokea, hakuna anayependa mabaya kama hayo yatokee,
kumwambia mtu haujui kapoteza ndugu wangapi, si sahihi kabisa, cha kushangaza wale ni wanajeshi
lakini hawaonyeshi kuwa wanajua athari za vita.
Naye Ofisa habari wa Yanga Jerry Muro akizungumzia suala hilo aliitaka TFF kuweka adharani ripoti
ya kamisaa wa mchezo huo ulichezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na kumalizika kwa sare na
kuwachukulia hatua stahiki waamuzi, na kamisaa ikiwa ni pamoja na kocha wa Ruvu Shooting Tom
Olaba hatua kali za kinidhamu huku wakiitadharisha TFF kutowapanga waamuzi hao katika mechi zao
za Ligi zinazofuata ikiwemo ya kesho kutwa jumamosi dhidi ya Polisi Morogoro la sivyo watagoma
kucheza ligi.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa suluhu, Tambwe alichezewa rafu kadhaa na beki wa timu hiyo,
George Michael, hadi akachanika mdomoni lakini mwamuzi hakuchukua hatua yoyote.
Ofisa habari wa TFF Boniface Wambura alipoulizwa kuhusiana na suala hilo kwanza alionyesha
kushtushwa na taarifa za Tambwe kuitwa mkimbizi na kudai kuwa bado hawajapata malalamiko ya
mchezaji huyo wala viongozi wa Yanga na iwapo watapata watafanyia kazi na kudai kuwa ripoti ya
kamisaa haiwezi kuwekwa hadharani na kuwataka Yanga kuacha kujichanganya.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Yanga Jonasi Tiboroha amedai kuwa Yanga ipo kwenye harakati za
kujenga uwanja wa Jangwani kama ulivyo Azam Complex ambapo utakuwa na uwezo wa kuchukua
watu 6,000.
Tiboroha alisema kuwa mkataba wao wa awali dhidi ya Kampuni ya kichina ya Beljing Construction
Engineering ambao walikuwa wajenge uwanja wa watu 25,000 umekufa baada ya serikali kuwanyima
eneo la nyongeza na sasa wanaelekeza nguvu kujenga uwanja wa mazoezi na kurekebisha Jengo lao
ikiwa ni hosteli za wachezaji na ofisi za utawala.
No comments:
Post a Comment