Na Bashir Yakub
Katika makala iliyopita nilisema kuwa vijana wengi wajasiriamali wanaofungua biashara za makampuni wanao uwezo mkubwa wa kufika mbali isipokuwa tatizo lao ni taarifa za mambo mbalimbali kuhusu uendeshaji wa kampuni hizo.
Mambo ya uendeshaji wa kampuni ni mepesi sana na yanawezwa na mtu yeyote isiopokuwa tatizo ni taarifa na elimu ya namna ya uendeshaji kisheria ili kampuni ionekane ni kampuni. Nilieleza namna kampuni inavyolipa kodi na taratibu za kikodi za kampuni.
Leo tuangalie kipengele kingine cha uendeshaji wa kampuni ambacho ni namna ya kupata leseni ya biashara.
1. KAMPUNI ULIYOSAJILI HAIWEZI KUANZA KAZI BILA LESENI YA BIASHARA.
Wajasiriamali wengi wanaofungua kampuni wanajua kuwa ukishapata usajili wa kampuni basi unakuwa umemaliza kila kitu na unaweza kuanza biashara. Wazo hili si la kweli kwakuwa baada ya kampuni kuwa imepata usajili na unataka kuanza biashara ni lazima uwe na leseni ya biashara (business licence). Kwa maana hii kumbe mchakato wa kuanza biashara na kampuni hauishii kwenye kupata usajili wa kampuni. Cheti cha kuzaliwa kwa kampuni yako ( certificate of incorporation) ni tofauti na leseni ya biashara.Na ili biashara ya kampuni ianze kisheria lazima uwe navyo vyote viwili.
2. LESENI YA BIASHARA HUTAFUTWA WAPI.
Leseni za biashara zote hupatikana manispaa. Kama wakati wa kusajili kampuni uliandika kuwa ofisi ya kampuni yako (Registered Office) itakuwa wilaya fulani basi leseni inatakiwa kufuatwa katika manispaa ya wilaya hiyo. Kwa mfano uliandika kuwa ofisi za kampuni zitakuwa Kinondoni, hii ina maana kuwa ukitaka leseni ya biashara lazima uifuate manispaa ya kinondoni na si kwingine.
3. MWENYE SIFA ZIPI ANARUHUSIWA KUPATA LESENI YA BIASHARA.
Sifa ya kwanza ni kuwa mtu yeyote raia wa Tanzania anayo haki ya kupatiwa leseni ya biashara. Pili Mtu huyo awe ametimiza umri wa miaka kumi na nane (18). Tatu awe na akili timamu. Nne awe na eneo la kufanyia biashara linalokubalika kisheria. Aidha utaratibu uko tofauti kidogo kwa mtu ambaye sio raia wa Tanzania. Mtu ambaye sio raia wa Tanzania hawezi kutafuta leseni ya biashara ikiwa hajapata kibali maalum kutoka idara ya uhamiaji. Kibali hicho lazima kiwe kinaonesha biashara aliyokuja kuifanya nchini na kazi hiyo hiyo iliyo kwenye kibali hicho ndiyo tu itakayotolewa leseni na manispaa.
4. KUPATA LESENI BILA USUMBUFU NENDA NA VIAMBATANISHO HIVI.
(i) Kama ni mtu binafsi nenda na jina la Biashara ulilochagua na kama ni kampuni nenda na (Certificate of Incorporation or Registration).
(ii) Pia kama ni kampuni nenda na Memorandum and Article of Association” .
(iii) Nenda na Kitambulisho cha mpiga kura, Cheti cha kuzaliwa au Hati ya kiapo kuonyesha kuwa ni Mtanzania na kama ni mgeni Hati ya kuishi nchini daraja la “A” (Residence Class “A”).
(iv) Usisahau hati ya kiuwakili (powers of attorney) kama wenye hisa wote wa Kampuni wapo nje ya nchi.
(v) Pia lazima uende na ushahidi wa kimaandishi kuonesha kuwa una mahali pa kufanyia biashara . Ushahidi wa kimaandishi waweza kuwa hati za nyumba za mahali utakapofanyia biashara , mkataba wa pango la sehemu uliyopanga kufanyia biashara, risiti za malipo ya kodi za majengo au ardhi za mahali utakapofanyia biashara.
(vi) Kumbuka kwenda na hati ya kujiandikisha kama mlipa kodi TRA (TIN) .
Ukiwa na vitu hivi hautapata usumbufu kupata leseni ya biashara na utakuwa umeepuka nenda rudi.
5. FOMU YA MAOMBI YA LESENI YA BIASHARA NI HII.
Maombi ya leseni ya biashara yana fomu maalum iitwayo 9TFN 2110 kwa jina la kitaalam. Hii ndiyo mwombaji anatakiwa kujaza na kuambatanisha viambatanisho nilivyoeleza hapo juu. Fomu hizi unazikuta kulekule manispaa. Bei ya fomu hizi ni Tshs 1 000/= ( Alfu Moja tu ). Tukutane tena katika uendeshaji wa kampuni.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
1 comment:
Hellow.
asante sana kwa elimu unayotupa kwa kutuelewesha kuhusu kufungua kampuni nk.
Naomba kitu kimoja,nahitaji kuelimishwa kujua jinsi kampuni inavyolipa kodi na taratibu za kikodi za kampuni.
Kwa maana kuna kampuni natarajia kupewa niisimamie mkoani Kilimanjaro.
Natanguliza shukurani.
Nitashukuru ukinitumia kwa email binafsi.
badvocalz@yahoo.com
Post a Comment