Saturday, December 6, 2014

WAZIRI MEMBE AANZISHA MFUKO KUSAIDIA WANAFUNZI ELIMU YA JUU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akitoa hotuba  wakati wa Mahafali ya Pili ya Chuo Kikuu cha Bagamoyo yaliyofanyika katika Viwanja vya Hoteli ya Kiromo iliyopo Bagamoyo. Wahitimu 99 katika fani mbalimbali walitunukiwa shahada zao. Pembeni yake ni Prof.  Costa Ricky Mahalu, Makamu Mkuu wa Chuo hicho. 
  =======================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ameanzisha Mfuko Maalum wa kuwasaidia Wanafunzi wenye Ulemavu na Mahitaji Maalum kwa Ngazi ya Elimu ya Juu ambao utajulikana kama The Bernard Membe Scholarship Fund.
Waziri Membe aliutangaza Mfuko huo wakati akihutubia katika Mahafali ya Pili ya Chuo Kikuu cha Bagamoyo yaliyofanyika katika Viwanja vya Hoteli ya Kiromo mjini Bagamoyo hivi karibuni.
Mhe. Membe alisema kuwa Mfuko huo ambao utakuwa chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo unalenga kuwasaidia Wanafunzi nchini kote wenye mahitaji maalum na wenye nia ya kufikia elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kifedha katika kutimiza malengo yao.
“Wakati umefika kwa Watanzania wenye uwezo kusaidia na kuchangia elimu nchini. Ni imani yangu kuwa kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali na pia kwa kutumia harambee mfuko huu utatunishwa na malengo yatatimia kama ilivyokusudiwa,” alisema Waziri Membe.
Aidha, Mhe. Membe alitumia fursa hiyo pia kuwaasa Wahitimu katika Kozi mbalimbali zinazotolewa na Chuo hicho kutumia vizuri elimu waliyoipata katika kudumisha amani, kufikia mafanikio na kuondoa umaskini katika jamii. Pia aliwaonya kujiepusha kabisa na vitendo vyovyote vya rushwa katika maisha yao na kuwataka kuwa raia wanaoishi kwa kufuata sheria za nchi.
Mhe. Membe ambaye pia alipata fursa ya kuwatunuku shahada mbalimbali Wahitimu hao kwa niaba ya Mkuu wa Chuo hicho, Askofu Mstaafu, Dkt. Elinaza Sendoro ambaye hakuweza kuhudhuria kwa sababu za kiafya, alizipongeza  jitihada za Chuo katika kutoa Taaluma mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinalenga kuwawezesha Wahitimu hao kujiajiri  na  kupata kazi sehemu yoyote duniani ikiwemo Mashirika ya Kikanda na Kimataifa.
“Ninaupongeza Uongozi wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo kwa kuweka mkazo katika  masomo ya Sayansi na Teknolojia, pia kwa ubunifu wa kuwafundisha vijana namna ya kutengeneza ajira na si kutafuta ajira ili kutoa suluhisho kwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu  nchini,” alisisitiza Mhe. Membe.
Awali akizungumza wakati wa mahafali hayo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Costa Ricky Mahalu alisema kuwa Chuo kimedhamiria kuwawezesha wanafunzi kuchangia Taifa katika vita dhidi ya maradhi, ujinga na umaskini na kutoa wataalam wenye uwezo wa hali ya juu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na utandawazi.
Chuo Kikuu cha Bagamoyo kilianzishwa mwaka 2011 kwa lengo la kutoa elimu ya juu kwa ngazi ya Shahada, Shahada ya Uzamili, Stashahada na Cheti katika kozi zinazohusu Sheria, Sayansi na Teknolojia,  Elimu, Utawala, Biashara, Usuluhishi wa Migogoro na Utunzaji wa Amani.
Sehemu ya Wahitimu hao wakifuatilia hotuba ya Mhe. Membe (hayupo pichani)
Baadhi ya wahitimu wa fani mbalimbali wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo wakiwa wamekaa kwa utulivu huku wakimsikiliza Mhe. Membe wakati wa sherehe za mahafali yao. 
Waziri Membe akiwatunuku  Shahada mbalimbali Wahitimu hao kwa niaba ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Askofu Mstaafu, Dkt. Elinaza Sendoro

Wahitimu wakiwa wamesimama kupokea shahada zao.
Wahitimu wa Stashahada

Sehemu ya Wageni Waalikwa
Waziri Membe akiendelea na hotuba
Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria mahafali hayo wakifuatilia hatua kwa hatua kile kinachoendelea katika sherehe hizo.
Meza Kuu wakiwa wamesimama kwa heshima ya  kumkumbuka Dkt.Edmund Senghondo Mvungi,  mmoja wa waanzilishi wa chuo hicho ambaye alifariki dunia mapema mwaka huu.
Waziri Membe akipokea zawadi kutoka kwa Bi. Happyness Katabazi kwa niaba ya Uongozi wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo wakati wa mahafali hayo.
 Waziri Membe akikata keki iliyoandaliwa na Wahitimu hao kama ishara ya kuwapongeza  huku akishirikiana na   Prof. Mahalu na mwakilishi wa Wahitimu hao Bi. Pamela Twalangeti 
waziri Membe na Prof. Mahalu kwapamoja wakifurahia burudani iliyokuwa ikitolewa na kikundi cha ngoma kutoka Chuo cha Utamaduni cha Bagamoyo (hakipo pichani)  
Kikundi cha ngoma kutoka Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo kikitumbuiza
Picha ya Pamoja na Wahitimu na Viongoiz wa Chuo

Waziri Membe akizungumza na Waandishi wa Habari

........................Matukio mengine kabla ya Mahafali kuanza

Msafara wa Waziri Membe ukiwasili
Akipokelewa na Prof. Mahalu
Akilakiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo hicho, Prof. Paramagamba Kabudi

Akisalimiana na Wakufunzi wa Chuo hicho

Maandamano kuelekea kwenye Mahafali
Brass band ikiwaongoza wahitimu kuelekea kwenye sherehe za mahafali. Picha na Reginald Philip

No comments: