Tuesday, December 9, 2014

MSICHANGIE SHEREHE PEKEE CHANGIENI NA MATIBABU - DC SIKONGE

Mkuu wa wilaya ya Sikonge Bi.Hanifa Selengu akimkabidhi kadi ya kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii  CHF mmoja kati ya wakulima wa tumbaku katika kijiji cha Kisanga wilayani humo wakati wa kampeni ya Uzinduzi wa mfuko huo. 
Mkuu wa wilaya ya Sikonge akikabidhi kadi ya CHF kwa mkazi wa kijiji cha Kisanga wilayani humo
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kisanga waliohudhuria uzinduzi wa kampeni hiyo ya uhamasishaji kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii CHF wilayani Sikonge.

Wananchi  wakiwa wamekaa  chini ya mti wa Mwembe wakisiliza kwa makini maelezo kuhusu faida za kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii CHF,wakati wa uhamasishaji mfuko huo.
Meneja wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF kanda ya Magharibi Bw.Emmanuel Adina akigawa vipeperushi kwa wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii CHF katika kijiji cha Kisanga.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima Afya NHIF kanda ya Magharibi Bw.Emmanuel Adina akitoa ufafanuzi kuhusu kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii.

 JAMII imeshauri kubadilika na kujenga tabia ya kuchangia matibabu kupitia mifuko ya (NIHF) na (CHF) na kuachana na tabia ya kupenda kuchangia sherehe pekee badala yake wajitoe kuchangia na matibabu.

Meneja wa mfuko wa taifa wa bima ya afya (NIHF) kanda ya magharibi Emmanuel Adina alisema hayo wakati akiongea na wananchi wa kata ya Kisanga wilaya ya Sikonge mkoani Tabora siku ya uzinduzi wa mfuko wa afya ya jamii (CHF).

Adina alisema jamii imejenga tabia ya kupenda kuchangia harusi na sherehe nyinginezo tena kwa kiwango kikubwa lakini linapokuja suala la kuchangia mifuko ya afya kwa ajili ya kupata matibabu bora jambo hilo linakuwa zito.

Alisema kiwango cha uchangiaji kwa wilaya ya Sikonge ni sh 5,000 na matibabu yatapatikana kwa muda wa miezi 12 kwa mume,mke na watoto nane.

Adina alisema afya ni jambo muhimu duniani na kama taifa lolote halina jamii yenye afya bora basi taifa hilo katika kuzalisha mali na kukuza uchumi ni ndoto.

Alibainisha mfuko wa afya ya jamii CHF ni mkombozi wa wananchi ambao wako kwenye sekta binafsi hivyo ni vyema jamii ikahamasika kujiunga nao.

Meneja huyo katika hatua nyingine alichangia kaya tano ambazo hawana uwezo na wako kwenye mazingira magumu ya kimaisha.

Aidha meneja huyo alifanikisha kupata wanachama wapya katika kata hiyo ikiwa ni jumla ya kaya 614 huku kaya wengine wakihamasika kujiunga na mfuko.

Adina aliwashawishi wananchi hao kutumia fursa walizonazo ikiwemo tumbaku kilo mbili tu zinatosha kujiunga na mfuko baada ya mauzo,jogoo na biashara ndogo walizonazo kwani matibabu ni jambo zuri kwa afya zao na kwamba ugonjwa unapokuja hautoi taarifa.

Aidha alibainisha kuwa mwananchi yoyote ambaye atashawishi mwanachama kujiunga na mfuko wa CHF atapewa kiasi cha sh 500 kama motisha ya kusababisha mfuko kupata mwanachama mpya.

No comments: