Monday, December 22, 2014

MILIKI KAMPUNI, JIFUNZE NAMNA YA KUUNDA KAMPUNI

Na Bashir Yakub
Ni ukweli usiofichika kuwa  biashara  na ujasirimali  kwa pamoja vimekua  kwa kiwango kikubwa. Hili linatokana na sababu nyingi ikiwemo ya kukua kwa biashara za kimataifa, maendeleo ya mawasiliano, marekebisho ya baadhi ya sera za nchi na sababu nyinginezo. Hali  hii imeleta ugumun kwa wanaofanya biashara nje ya kampuni. Si rahisi kufanikiwa katika biashara bila kuifanya biashara yako katika mtindo wa kampuni. Hata iwe ndogo ya kuuza mayai au kufuga kuku mafanikio zaidi ni pale biashara hiyo utakapoifanya kampuni. Ni kutokana na umuhimu wake ikanilazimu niwajuze, hasa vijana wenzangu, kuhusu kampuni tukijielekeza zaidi katika aina na uundwaji wake kutokana na Sheria ya Makampuni  ya mwaka 2002.

 KAMPUNI NI NINI
Awali ya yote tujue nini maana ya kampuni. Kwa ufupi sana twaweza kusema kuwa, Kampuni ni muunganiko  wa kibiashara wa mtu zaidi ya mmoja ulioundwa na kusajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni  2002.
Katika maana hii tunaona kuwa lazima uwe muunganiko wa watu. Waweza kuwa wawili, watatu na kuendelea. Hii ina maana kuwa hakuna kampuni ya mtu mmoja. Lazima awe zaidi ya mmoja,  uwe na mke wako au mume wako au na rafiki, au na mtoto wako itategemea lakini huwezi kuwa mmoja.
Pili, lazima  iwe imesajiliwa chini ya sheria ya makampuni kama nilivyoonesha. Hiyo  ndio itaitwa kampuni. Zaidi ya hapo hicho ni kitu kingine na sio kampuni.

AINA ZA KAMPUNI
Kabla hatujaingia katika mchakato wa kuunda kampuni ni vema kabisa tukajua kuna aina ngapi za kampuni. Hii itakusaidia kujua  sifa za kila kampuni  na aina ya kampuni unayotaka. Makampuni yamegawanyika katika mgawanyo ufuatao.

( a ) Kampuni ya umma (public company).            Kampuni hii ni ya umma kama jina lake lilivyo. Imeitwa  kampuni ya umma kwasababu kuu kuwa  unapounda kampuni hii kila mtu au kila mwanaumma,mwanajamii  anaruhusiwa kuomba  uanachama  ikiwa tu atatimiza masharti  kadhaa. Uanachama katika kampuni ndio umiliki. Ukisikia mtu mwanachama ( member) ni mmiliki. Na  umiliki au uanachama unatofautiana kutokana na kiasi  cha hisa anazomiliki mtu. Hivyo katika kampumi hii huwezi kumzuia mtu kuwa mmoja wa wamiliki, yeyote mwenye uwezo awe adui yako au rafiki ilimradi umesajili kampuni kama ya Umma  atakuwa pamoja nawe katika umiliki wa kampuni.

Pili, ili kampuni ya umma  ianzishwe ni lazima iwe na wanachama wasiopungua saba. Wanachama wakiwa sita , watano na kushuka hawawezi kuanzisha kampuni hii.

Tatu,Wakurugenzi wake wanaanzia wawili, hii ni kusema mtu mmoja hawezi kuwa mkurugenzi katika kampuni hii.
Nne, ni kuwa hisa zake ni huru. Hii ina maana kuwa  hisa zinaweza kuhama kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Mwanachama mmoja anaweza kumuuzia  mwanachama mwingine hisa zake zote au kiasi. Kila mtu yuko huru na hisa zake  anaweza kumuuzia mwingine au akampa zawadi, haizuiwi.

( b ) Kampuni binafsi(private company). Hii  ni aina ya kampuni ambayo watu wengi huunda.Karibia asilimia kubwa ya makampuni tunayoyaona  ni ya binafsi. Kampuni binafsi zina sifa zifuatazo.   
Kwanza, wanachana wake hawapaswi kuzidi hamsini . Katika idadi hiyo wafanyakazi waajiriwa hawahesabiwi.

Pili,hisa zake hazihamishiki kirahisi. Ina maana kuwa huwezi kuuza au kugawa hisa zako kwa mtu mwingine bila ridhaa ya wanachama wengine. Kwa kuwa ni kampuni binafsi  mtu yeyote anayeingia lazima awe  amekubalika kwa wanachama wengine pengine asiwe adui au yeyote asiyehitajika.

Tatu, inakatazwa kwa kampuni binafsi kuwaalika au kuwaita watu kuja kununua hisa.

Nne, inawezekana kuwa hata na mkurugenzi mmoja. Si lazima wawe wawili au zaidi hata mmoja anatosha.

(c ) Kampuni za kisheria(statutory company). Hizi ni kampuni zinazoanzishwa na sheria maalum za bunge. Mara nyingi kampuni hizi huundwa ili kutimiza majukumu maalum katika jamii hasa huduma za kijamii. Taasisi nyingi za serikali pamoja na mashirika ya umma huwa ni kampuni za aina hii.
Kwa uchache ni hizo.

JINSI YA KUUNDA KAMPUNI
Huu ndo mzizi wa mada kwakuwa wengi wangependa kujua ni kwa taratibu zipi  kampuni inaweza kuundwa .Kwetu hapa Tanzania kampuni inaundwa kwa kufuata utaratibu huu.

( a )  Kwanza kabisa ni kuchagua jina la kampuni. Kampuni lazima iwe na jina linalotambulika. Hatua hii huwa inaitwa Name Search ambapo unatakikwa kuandika barua kwa msajili wa makampuni kwa Dar es salaam ni pale mnazi mmoja jengo la ushirika. Utaeleza jina la kampuni yako. Hii husaidia kutokuwa na majina yanayofanana baina ya makampuni. Majina ya makampuni yote yapo kwa msajili wa makampuni hivyo si rahisi kampuni zaidi ya moja kuwa na majina yanayofanana.
Msajili wa makampuni baada ya utafiti atajibu kama jina hilo halipo uendelee nalo au lipo uachane nalo.

( b ) Baada ya jina kuwa limethibitishwa  hatua inayofuata ni kuwasilisha kwa msajili wa makampuni waraka wa kampuni na katiba ya kampuni. Waraka wa kampuni (memorandum of association)   ni waraka maalum uliosainiwa na wanachama wote ambao hueleza na kuchambua kile ambacho kampuni itakifanya. Shughuli za kampuni zinatakiwa kuelezwa vyema ndani ya waraka huu. Waraka huu lazima uwe na mhuri wa mwanasheria.

Katiba ya kampuni kwa upande mwingine(article of association) nayo lazima iwe imesainiwa na wanachama wa kampuni . Katiba ndiyo inayoeleza uendesahaji  mzima wa kampuni . Inaeleza haki na wajibu wa  wanahisa, uongozi wa kampuni, mgao wa mapato, nguvu na mamlaka ya wakurugenzi, mikutano  na utaratibu wake, umiliki na ugawaji wa hisa, uhamisho wa hisa n.k. Hii nayo lazima iwe imesainiwa na mwanasheria.

( c ) Lazima kupeleka kwa msajili wa makampuni maelezo(statement) yanayowahusu wakurugenzi wa kampuni. Katika maelezo hayo wasifu wa wakurugenzi unatakiwa kuwa umeelezwa vyema.

( d  ) Lazima pia ijazwe fomu maaalum yenye maelezo yanayohusu anuani kamili ya ofisi za kampuni.Anuani hapa sio tu S.L.P bali wapi ofisi za kampuni zilipo inakoendeshea shughuli zake.

( c ) Pia  lazima ijazwe fomu maalum ambayo ipo kama kiapo kuonesha kuwa matakwa yote ya kisheria yametimizwa  hivyo kampuni inatakiwa kupatiwa usajili. Fomu hiyo inajazwa na wakili au mtu yeyote ambaye jina lake limetajwa katika katiba kama mkurugenzi wa kampuni au katibu wa kampuni. Fomu hii inakuwa ni ushahidi kuwa matakwa yote yametimizwa kwa ukamilifu.

Baada ya hapo kampuni inaweza kusajiliwa kwa kupewa cheti cha kuzaliwa.
Taratibu zote hizi ikiwa ni pamoja na kuandaa katiba, fomu na waraka kwa wepesi zaidi hufanywa kwa wanasheria.

Kwa kumalizia nishauri kuwa kufanya biashara kwa mtindo wa kampuni ni muhimu sana  kuliko ambavyo baadhi ya watu wanaweza kufikiria.Na karibia biashara zote za kisasa hufanyika kwa mtindo huu. Asikudanganye mtu kuwa atatoka mfanyabiashara ulaya , Amerika au hata hapa nchini mfanyabiashara mkubwa ambaye atakubali kufanya biashara na mtu binafsi . Labda iwe biashara  ya kukufanya kibarua. Makampuni yote ya nje au ndani  huwa hayafanyi biashara na watu binafsi isipokuwa tu mmejiunga na kuwa kampuni. Na hapa nieleweke vyema kuwa ninaposema biashara simaanishi biashara kubwa saana. Hapana ninamaanisha biashara hiyohiyo ndogo unayoifanya. Biashara yako ya ufugaji kuku kama nilivyosema usikubali kuifanya kama mtu binafsi, biashara ya kuuza maziwa usikubali kuifanya kama mtu binafsi vivyohivyo biashara yako ya duka, biashara yako ya  huduma ya pesa kwa njia ya simu, kuuza mazao, kijiwe chako cha ufundi magari au seremala  na biashara nyingine ndogo zote usizifanye wewe kama wewe.
Ukweli ni kuwa hakuna atayekupa kazi ya maana kama wewe ni mtu binafsi.Biashara ya sasa haifanywi hivyo. Usikwamishe kukua kwa biashara zako... Unda kampuni sasa!

Mwandishi wa makala ni Mwanasheria na mshauri wa masuala ya sheria kupitia gazeti la serikali Habari leo la kila jumanne, gazeti  Jamhuri kila jumanne, na Nipashe kila jumatano.
0784482959
0714047241
bashiryakub@ymail.com


5 comments:

Anonymous said...

Nimefurahishwa sana na makala yako nzuri na ya kuelimisha. Nina swali moja, ikiwa niliwahi kusajili kampuni zaidi ya miaka kumi iliyopita na sikuwahi kufanya biashara yoyote toka muda huo, na sasa nina wazo la kuanza upya na kuboresha jina la biashara. Kipi kitakuwa rahisi kwangu kusajili kampuni upya au kubadili jina la usajili wa awali? Tafadhali naomba ufafanuzi!

Unknown said...

Naam! Nimefarijika na makala hii, asante msomi.

Unknown said...

Asante kwa ufafanuzi

Tungaraza Benedicto said...

Nilikuwa natafuta namna ya kusoma kuhusu kampuni uanzishaji na uendeshaji wake asante sana

Brunohealth and fitness said...

Asante umenisaidia kwa kiwango flani