Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Juma Assad na ambaye kwa wadhifa wake ni Mkaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa akiwa na baadhi wa wasaidizi wake katika Kikao cha Bodi ya Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kilichofanyika jana ( Jumanne) Hapa Umoja wa Mataifa.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwenye tai nyekundu akimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Bodi ambaye pia ni Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu kutoka Uingereza aliyekuwa akimkaribisha kwenye Bodi hiyo, upande wa kulia ni Ujumbe wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka India. Uingereza, India na Tanzania ndiyo inayounda Bodi ya Wakaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa na Mashirika yake. Katika mkutano huo ilielezwa kuwa Tanzania kwa maana ya CAG itachukua uenyekiti wa Bodi ifikapo Januari Mosi mwakani, uenyekiti huo ni wa miaka miwili.
Pamoja na Kushiriki Vikao vya Bodi, CAG alipata nafasi ya kufika katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ambako alipokelewa na Mwenyeji wake, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhani Mwinyi. Akiwa katika Uwakilishi wa Kudumu CAG alijionea maendeleo ya ukarabati wa Jengo la Uwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa
Na Mwandishi Maalum, New York
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Juma Assad ameelezea kuridhishwa kwake na mwenendo wa vikao vya Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa ( UNBoA) na kuahidi kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na wajumbe wenzie wanaounda bodi hiyo.
Ameyasema hayo siku ya jumanne wakati wa wajumbe wa Bodi hiyo walipokutana hapa Umoja wa Mataifa. Hii ni mara ya kwanza kwa CAG kuhudhuria vikao vya Bodi hiyo ambayo wajumbe wake ni wadhibiti na wakaguzi wakuu wa hesabu za serikali kutoka Uingereza, Tanzania na India
Profesa Mussa Juma Assad ambaye ameteuliwa hivi Karibu na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akichukua nafasi ya Bw. Ludovick Utouh ambaye amestaafu kwa mujibu wa sharia, amewaeleza wajumbe wenzie kuwa amejifunza mengi.
Katika kikao chao cha siku moja kilichotanguliwa na kikao cha jopo la wakaguzi wa nje kilichojadilia taarifa mbalimbali za mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwamo taarifa ya Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic, wajumbe wa Bodi walijadiliana pamoja na mambo mengine changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao kama wakaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa.
Awali wakizugumza kwa nyakati tofauti, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Uingereza Bw.Amyas Morse na Bw. Shashi Sharma Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka India pamoja na kumkaribisha Profesa Assadi katika Bodi hiyo pia walimuahidi ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu waliyokabidhiwa.
Aidha katika kikao hicho cha Bodi ilitolewa taarifa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Tanzania ( CAG) atashika uenyekiti wa Bodi kuanzia Januari Mosi mwakani. Nafasi hiyo ya uenyekiti huwa ni ya mzunguko wa kipindi cha miaka miwili ambapo hivi sasa inashikiliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Uingereza.
Aidha Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Nje, Bw. Fransis Kitauli ambaye ndiye anayemwakilisha CAG katika utekelezaji wa mukumu ya kila siku ndani ya Bodi hiyo naye atakuwa mwenyekiti wa Kamati ya Operesheni za Ukaguzi ( AOC)
Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa, ni chombo huru na kinachojitegemea chenye jukumu la kukagua vitabu vya hesabu za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Mashirika na Taasisi zote zilizochini ya Umoja wa Mataifa, Misheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa na Miradi mbalimbali inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Tanzania kupitia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilichaguliwa kuwa Mkaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa mwaka 2012 ikichukua nafasi ya Afrika ya Kusini. Aidha Tanzania ambayo itadumu katika Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa kwa Miaka sita inakuwa nchi ya Tatu ya Afrika kushika wadhifa huo nyeti ikitanguliwa na Ghana na Afrika ya Kusini.
No comments:
Post a Comment