Thursday, November 13, 2014

WANANCHI WAOMBWA KUCHANGIA DAMU

MPANGO Taifa wa Damu Salama Tanzania (NBTS) unatoa rai kwa wananchi wote wenye sifa za kuchangia damu wajitokeze kuchangia damu katika vituo vya Damu salama hasa kipindi cha mwezi Novemba mpaka Januari mwakani , kipindi ambacho wanafunzi wa sekondari wanakuwa likizo hivyo kusababisha kuongezeka kwa uhaba wa damu nchini.

Hayo yalisemwa leo na Afisa Habari wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Tanzania Bw. Rajab Mwenda (pichani) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ilala mchikichini, Dar es salaam, alisema damu salama kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Chama cha Msalaba Mwekundu umekusanya chupa za damu asilimia 97% na kuvuka lengokatika kipindi cha miezi mitatu julai hadi septemba 2014.

Jumla ya chupa 40,974 zilikusanywa , lengo lilikuwa kukusanya chupa 42,500. \“Katika kipindi hicho chupa za damu zilizokusanywa toka vituo vidogo( Blood collection satellite sites) ni 2,886 (8%) ambapo kituo cha Morogoro chupa 1,158, Dodoma-818, M/moja-490, kigoma- 93 na Lindi-327)” alisema.

Alisema katika robo mwaka ya Julai- Septemba 2014 asilimia 32 ya jumla ya chupa zilizokusanywa zilitengenezwa mazao ya damu; Packed Red blood cell,   chembe sahani (platelets) na plasma. Lengo lilikuwa ni kutengeneza 40% ya damu iliyokusanywa.

Damu iliyokusanywa pamoja na mazao ya damu zilisambazwa katika hospitali 271 ( hapa nchini zenye uwezo wa kutoa huduma ya damu na asilimia 50 (135) ya hizo hospitali zilipata zaidi ya 80% ya mahitaji Kipindi cha Julai-Septemba 2014 asilimia 53 ya wachangia damu walijulishwa majibu yao lengo lilikuwa ni kufikia asilimia 70 ya wachangia damu.

Kanda iliyoongoza kwa makusanyo ya damu ni kanda ya Mashariki ambayo ilikusanya chupa 10,525 ikifuatiwa na kanda ya ziwa chupa 5,561.

Mpango wa Taifa wa Damu salama kwa kushirikiana na Bloomberg, Engender health , Chama cha msalaba mwekundu na Mganga mkuu wa mkoa wa kigoma ulifanikiwa kufungua kituo kidogo cha kukusanya na kusambaza damu (satellite blood center) tarehe 08/9/2014 Mkoani Kigoma, kituo ambacho kitakuwa na uwezo wa kukusanya wastani wa chupa 5000 kwa mwaka.

Pamoja na mafanikio ya kuongezeka kwa wachangia damu wa hiari mwaka hadi mwaka kumekuwepo na changamoto mbalimbali . Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na: Mahitaji makubwa ya damu kuliko upatikanaji, Mahitaji ni wastani wa chupa 400,000-450,000 kwa mwaka, mpango unakusanya 140,000- 160,000 kwa mwaka Uuzwaji wa damu mahospitalini, tabia inayofanywa na watumishi wasio waaminifu.

Ufinyu wa bajeti ya uendeshaji ambao unasababisha Mpango kuto tekeleza baadhi ya mikakati iliyojiwekea Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeweka mikakati ili kufikia malengo kwa kipindi cha Octoba- Disemba 2014  Kuendelea kushirikiana na Taasisi za dini katika kutoa elimu na kuhamasisha waumini wachangie damu kwa hiari, tarehe 02/11/2014 Jumuiya ya madhehebu ya Shia kwa kushirikiana na Damu salama waliendesha zoezi la kuchangia damu nchini ambapo jumla ya chupa 900 zilikusanywa. Jitihada zinafanyika kuhamasisha madhehebu mengine kuchangia damu. Rai kwa taasisi zote za kidini kuchangia damu katika kipindi tunachokaribia ambapo wanafunzi wa sekondari wata kuwa likizo. Kipindi hiki ni katikati ya Novemba mpaka Januari 2015.

Kuendesha zoezi maalumu la kuchangia damu kutoka kwa wanachama wa klabu ya wachangia damu. Zoezi hili litafanyika nchi nzima tarehe 06/ 12/2014 kwenye vituo vikubwa vya kanda vya damu salama. , Lengo ni kukusanya chupa 1,800

Kufanya kampeni ya kuhamasisha wanachi kuchangia damu wakati wa madhimisho ya siku ya ukimwi duniani (01/12/2014) na siku nyingine zitakazo fuata

Kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali Puplic private partnership (PPP) katika shughuli za kuchangia damu Kushirikiana na uongozi wa mkoa kupitia mganga mkuu wa mkoa ili wilaya zitenge bajeti ya kukusanya damu kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa damu salama

Kuendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii (nje ya shule na vyuo) umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari ili kuongeza kiwango cha damu kinachokusanywa na kupunguza changamoto ya upungufu wa damu katika mahospitali hali inayopelekea watu kutoa rushwa ili wapatiwe huduma ya damu

Kuendeleza utaratibu wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya simu kwa wachangia damu. Ujumbe huo utakuwa wa kuhamasisha, kumkumbusha mchangiaji siku ya kuchangia tena damu n.k Kushirikiana na Wizara ya afya na Bohari kuu ya madawa (MSD) kuhakikisha vitendanishi vya kutosha vinapatikana kwa wakati Kuendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya damu kwa watumishi wa hospitali, kuhamasisha jamii kutoa ushirikiano wa kubaini, kuzuia na kukemea vitendo vya uuzaji wa damu

Kutoa majibu ya wachangia damu kwa wakati ili kuwapa hamasa ya kuchangia damu wakati mwingine unapofika

No comments: