Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wa tatu kutoka (kushoto) Makamu wa Rais wa
Kenya, William Ruto, (kushoto kwake) Makamu wa Rais kwanza wa Burundi,
(kulia kwake) wakijumuika kwa pamoja na viongozi wengine wakionyesha
Taarifa ya pamoja waliyoisaini kuhusu majadiliano ya kuimarisha
Miundombinu kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
katika mkutano wa 3 wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC) kuhusu
Miundombinu, uliofanyika kwenye Ukumbi wa KICC, jijini Nairobi jana
Novemba 29, 2014. Picha na OMR.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na baadhi ya viongozi wakati wakitoka
kwenye Ukumbi wa mikutano wa KICC, baada ya kushiriki katika mkutano wa
3 wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC) kuhusu Miundombinu
uliofanyika jijini Nairobu, Kenya jana Novemba 29, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi
wengine walioshiriki katika mkutano huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, kifurahia jambo na Makamu wa Rais wa Kenya
William Ruto na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, wakati
wakiondoka katika viwanja vya Ukumbi wa mikutano wa KICC, baada ya
kushiriki kwenye mkutano wa 3 wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC)
kuhusu Miundombinu, uliofanyika jijini Nairobi, Kenya jana Novemba 29,
2014. Picha na OMR
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI (EAC) KUHUSU MIUNDOMBINU JIJINI NAIROBI, KENYA
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI (EAC) KUHUSU MIUNDOMBINU JIJINI NAIROBI, KENYA
Mheshimiwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib
Bilal jana Novemba 29, 2014 aliiwakilisha Tanzania katika mkutano wa
siku moja wa Wakuu wa Nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini
Nairobi, Kenya. Mkutano huo, kwa mujibu wa utaratibu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, unafanyika kila baada ya miaka miwili na lengo lake
kuu ni kufanya tathmini juu ya miradi ya miundombinu inayoshirikisha
nchi washirika, sambamba na kutazama fursa ya kutanua miundombinu mipya
katika nchi hizi kwa lengo la kukuza uchumi wa pamoja kwa nchi za Afrika
Mashariki.
Tathmini
hii ya Miundombinu inafanyika kwa kuwa mataifa ya Afrika Mashariki
yanatambua umuhimu wa kuwa na miundombinu bora katika nchi hizi ili
kuharakisha ukuaji wa uchumi, sambamba na kutanua mtengamano wa nchi
hizi na hivyo kuwafanya wananchi wanaoishi ndani ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki kuzidi kuwa wamoja.
Mkutano
wa jana uliongozwa na Kaimu Rais wa Kenya Mheshimiwa William Ruto na
kuhudhuriwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal, Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Burundi, Waziri Mkuu wa Rwanda pamoja na Waziri wa Afrika
Mashariki wa Uganda. Viongozi wengine waliopata nafasi ya kuhudhuria
mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa Balozi Richard Sezibera, Katibu Mkuu
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Waziri wa Wizara hiyo kutoka Tanzania,
Mheshimkiwa Samwel Sitta, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt.
Donald Kaberuka, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Ukanda wa Afrika,
Bwana Makhtar Diop, Katibu Mtendaji wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi na
Baalozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Balozi Filiberto Sebregondi.
Pia mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi za China, Marekani,
Japan na nyinginezo ambazo ni wadau wakubwa wa ujenzi wa miundombinu
katika nchi za Afrika Mashariki.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Kaimu Rais wa Kenya, William Ruto
alifafanua juu ya umuhimu wa kuhakikisha Afrika Mashariki inaunganishwa
kwa miundombinu imara ili kukuza uchumi na akapongeza jitihada
mbalimbali zinazofanyika katika kufanikisha azma hiyo huku pia akiomba
nchi wanachama wa Afrika Mashariki kuendelea kuungana katika kutekeleza
miradi ya miundombinu na kujitahidi kutafuta fedha kwa ajili ya
kukamilisha miradi hiyo.
Mkutano
huu pia uliambatana na kupokea ripoti ya utekelezaji wa maagizo ya
Wakuu wa Nchi za EAC kuhusu Miundombinu kutoka kwa Mawaziri wa Nchi za
Jumuiya. Wakuu wa Nchi katika Mkutano huu walipokea taarifa ya
utekelezaji wa maagizo waliyoyatoa katika mkutano wa pili uliofanyika
mwezi Novemba, 2012 na kuidhinisha miradi 72 ya miundombinu ya
kipaumbele ya Barabara, Reli, Nishati na Bandari.
Kwa
upande wa utekelezaji; miradi 16 imekamilika, 39 inaendelea kutekelezwa
na 17 ipo katika hatua za awali za kutafutiwa fedha kwa ajili ya
utekelezaji wake.
Kwa
upande wa Tanzania miradi minne imekamilika ambayo ni Umeme katika mji
wa Kibondo, mradi wa barabara ya Mbezi-Shule-Tangibovu-Makutano ya
Nelson Mandela na barabara ya Tabata. Barabara nyingine iliyokamilika ni
Nyangunge – Musoma – Sirari na sehemu ya Simiyu - Musoma inayounganisha
Kenya na Tanzania huko ujenzi unaendelea.
Akizungumza
katika Mkutano huo Makamu wa Rais amezitaka nchi wanachama kuharakisha
utekelezaji wa miradi ya Miundombinu ili kusaidia utekelezaji wa Itifaki
ya Soko la Pamoja, ambayo inalenga kurahisisha usafirishaji wa bidhaa
na abiria. “Tusiishie kubakiza mipango hii katika karatasi, tusiishie
kuzungumza tu bali huu ni wakati wa kuhakikisha tunarahisisha ufanyaji
biashara katika nchi zetu na kupunguza vikwazo visivyo vya lazima,”
alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
Katika
mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais pia aliambatana na Mheshimiwa
Dkt. Mahadhi J. Maalim, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zanzibar,
Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui. Mheshimiwa Makamu wa Rais na msafara
wake tayari wamerejea nyumbani Tanzania ambapo kesho anatarajiwa kuwa
Mgeni Rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani,
maadhimisho yanayofanyika Kitaifa Mkoani Njombe.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Novemba 30, 2014
No comments:
Post a Comment