Monday, October 27, 2014

CHANZO CHA MAJI IKORONGO MKOMBOZI WA MJI WA MPANDA

 Wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakiangalia chanzo cha chemichemi ya maji cha Ikorongo kilichoko kilometa 13.2 kutoka Mpanda mjini. Chanzo hicho kina uwezo wa kutoa maji ya kutosha mji wote wa Mpanda.
 Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda Magdalena Mkeremi (aliyejifunika mtandio) akifafanua jambo kwa timu ya wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi Rais, Tume ya Mipango walipotembelea chanzo hicho hivi karibuni
 Mhandisi Happiness Magalula, Naibu Katibu Mtendaji anayesimamia Klasta ya Miundombinu na Huduma (mwenye sweta la blue) akitaka ufafanuzi wa miundombinu ya kuwezesha maji kuwafikia wananchi kutoka katika chanzo hicho. Bomba la inchi kumi limetandazwa kutoka kwenye chanzo hicho mpaka mjini ambako kuna tanki kubwa la maji yanayosambazwa katika mji wa Mpanda na vitongoji vyake
 Tanki la maji lenye uwezo kujaza lita 1,000,000 linalosambaza maji katika mji wa Mpanda, mkoani Katavi
Moja ya bomba la maji katiak shule ya Sekondari ya Shanwa katika mji wa Mpanda ambao wanapata maji kutoka katika chanzo cha maji cha Ikorongo. Anayefungua bomba ni Festo Katanti, Mtalaam wa maji wa Halmashauri (Techenician) nyuma yake ni mwalim Mkuu wa Shule hiyo Emmanuel Nkumbo na kushoto kwa Katanti ni Mhandisi Happiness Mgalula, Naibu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango.

Na Mwandishi wetu, Katavi
Chanzo cha maji cha chemichemi ya Ikorongo ambacho ni cha asili kipo kilometa 13.2 kutoka Mpanda mjini, mkoani Katavi. Chanzo hiki cha maji kinazungukwa na miti na uoto wa asili unaolinda maji hayo yawe safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Katavi Magdalena Mkeremi anasema chanzo hiki cha maji ni chemichemi yenye maji masafi yasiyokauka hata wakati wa kiangazi. Chanzo hiki kina uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita milioni sita kwa siku.Mradi wa maji wa Mji wa Mpanda ni wa gharama nafuu kwa sababu hautumii pampu ya aina yoyote bali maji husambazwa kwa njia ya mserereko (gravity).

Bomba kubwa la maji la inchi kumi limelazwa kutoka kwenye chanzo na kupelekwa Kazima kwenye tanki kubwa la ujazo wa lita milioni moja ambalo limejengwa eneo la kilometa 13 kutoka kwenye chanzo cha maji.  Vile vile  maji kutoka kwenye tanki hilo na kwenda mjini na katika mitaa au vijiji pia hutumia mserereko hivyo, kurahisisha gharama zake.

Mradi huo wa maji wa vijiji kumi au mitaa kumi ya mji wa Mpanda unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia chini ya mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa. “Maji yalikuwa tatizo kubwa hapa kwetu lakini ujio wa mradi huu umerahisisha upatikanaji wa maji mjini na kwenye mitaa ya mji wa Mpanda,” anasema Mhandisi.

Tayari vimejengwa vituo vya kuchotea maji 41 katika mitaa kumi na watu binafsi wapatao 300 wameunganishiwa maji kupitia chanzo hicho cha maji. Amesema mradi huo umetekelezwa kwa muda wa miaka mitatu tangu 2012/13 -2014/15 ambapo umekamilika mwezi Septemba 2014.Amesema ili kuufanya mradi huo kuwa endelevu wamejenga nyumba ya mlinzi ili kulinda chanzo hicho cha maji kisiharibiwe kwa namna yoyote ile ikiwa ni pamoja na kulinda mazingira yanayozunguka eneo hilo.

No comments: