Wadau mbalimbali wa madini ya vito waliopata bahati kutembelea Banda la Tanzania katika siku ya kwanza ya Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok, wakishangazwa na mng’ao wa Kito cha Tanzanite katika Pete iliyovalishwa kidoleni mwa Mwanafunzi, Raia wa Thailand aliyeomba kujaribisha Pete hiyo. Anayetoa maelezo ni Mfanyabiashara wa Madini ya Vito kutoka Tanzania, Bw. Gregory Kibusi (Mwenye mavazi ya Bhatiki).
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo akizungumza na mdau wa madini ya vito aliyetembelea Banda la Tanzania. Kalugendo alitumia fursa hiyo kumkaribisha mdau huyo katika Maonesho ya Vito ya Arusha yanayotarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu nchini Tanzania. Katikati ni Afisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Asimwe Kafrika.
Sehemu ya shehena ya madini mbalimbali ya vito katika Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok.
Wafanyabiashara wa Madini ya Vito kutoka Tanzania, Gregory Kibusi (Mwenye nguo za Bhatiki) na Kassim Iddi Pazi (Mwenye Shati la rangi ya Bluu), wakimwonyesha Mteja aina mbalimbali za madini ya vito yanayopatikana Tanzania.
Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Thailand, Bi. Chutima Bunyapraphasara, akikata utepe kuzindua rasmi Maonesho hayo. Kushoto kwake ni Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito wa Thailand, Bw. Somchai Phornchindarak na Kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Uhamasishaji Biashara Kimataifa, Bibi Nuntawan Sakuntanaga.
Baadhi ya Viongozi kutoka Taasisi na Mashirika mbalimbali ya kiserikali na binafsi yanayoshiriki katika Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok, wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Thailand, Bi. Chutima Bunyapraphasara (katikati – mwenye sketi ndefu).
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini - Tanzania (TANSORT), Archard Kalugendo (wa kwanza kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati iliyoandaa maonesho husika.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini - Tanzania (TANSORT), Archard Kalugendo akisalimiana na Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito wa Thailand, Bw. Somchai Phornchindarak baada ya uzinduzi rasmi wa maonesho hayo.
Na Veronica Simba - Bangkok
Banda la Tanzania katika siku ya kwanza ya Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok, yaliyozinduliwa Septemba 9, 2014 nchini Thailand, limekuwa na mvuto wa kipekee kwa wadau wa madini husika kutoka mataifa mbalimbali duniani waliofika katika maonesho hayo.
Mkuu wa Banda la Tanzania, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo alisema, wadau wengi waliofika katika maonesho hayo, walivutwa na aina mbalimbali za madini ya vito yanayopatikana Tanzania hususan Tanzanite.
“Unajua, Tanzanite ni madini yanayopatikana Tanzania pekee ambapo sifa hii inayafanya kuwa madini yenye mvuto wa pekee,” alisema Kalugendo.
Aliongeza kuwa, mbali na kuwa Tanzanite inapatikana Tanzania pekee, lakini pia ina mvuto wa pekee machoni mwa watazamaji ambayo ni sababu nyingine inayowavutia watu wengi kupenda kufahamu zaidi kuhusu madini hayo, hali ambayo imesababisha watu wengi kutembelea Banda la Tanzania.
Alifafanua kuwa, pamoja na kuwepo mabanda kutoka nchi nyingine yaliyo na madini ya Tanzanite katika maonesho hayo, wengi wa wadau walitembelea Banda la Tanzania wakitaka kuelimishwa zaidi kuhusu madini hayo, hali inayodhihirisha kuwa ufahamu kwamba Tanzanite inatoka Tanzania pekee umeongezeka kwa watu kutoka mataifa mbalimbali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wafanyabiashara wa Madini ya Vito kutoka Tanzania wanaoshiriki katika maonesho hayo, Gregory Kibusi na Kassim Pazi walisema ushiriki wa Tanzania katika maonesho husika kwa msimu huu umeboreka zaidi kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanyika.
“Tulitumia uzoefu tulioupata katika maonesho ya msimu uliopita na hivyo tukajipanga vizuri zaidi kuhakikisha tunakuwa na ushiriki wenye tija msimu huu na ndiyo maana katika siku ya kwanza tu ya maonesho, tumeshuhudia banda letu likitembelewa na watu wengi sana,” alisema Kibusi.
Naye Gregory alifafanua kuwa maandalizi waliyofanya ni pamoja na kuandaa madini ya kutosha hasa yale yaliyokatwa tayari, ambayo ndiyo yanayopendwa zaidi na wadau wengi wanaofika katika maonesho.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Madini ya Vito kutoka TANSORT, ambao ndiyo waratibu na wasimamizi wa ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo, Teddy Goliama alisema maandalizi mengine yaliyofanyika ni pamoja na kuwepo na washiriki wengi zaidi wakijumuisha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini husika pamoja na maafisa kutoka Wizarani.
Vilevile alisema kuwa, mbali na kutangaza madini mbalimbali yaliyopo Tanzania, Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki katika maonesho hayo unafanya kazi ya kuitangaza nchi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji pamoja na vivutio vya utalii.
“Tumeamua kutumia fursa hii ya maonesho kuitangaza nchi kwa ujumla. Tunawashukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii ambao walitupatia vipeperushi, picha za video na makabrasha mbalimbali yenye kutangaza vivutio vya utalii wa nchi yetu. Tumegawa vipeperushi vingi ambavyo tunaamini vitasaidia sana kuitangaza nchi yetu katika anga za kimataifa na hivyo kuvutia watalii na wawekezaji wengi zaidi,” alisema Teddy.
Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok, yaliyofunguliwa Septemba 9 mwaka huu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Thailand, Bi. Chutima Bunyapraphasara, yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba 13, 2014. Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kushiriki maonesho hayo.
No comments:
Post a Comment