Monday, September 29, 2014

Benki ya Azania, TAFSUS yakabidhi shilingi milioni 100 kuboresha makazi Manzese

 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka (kulia) na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro (kushoto) kwa pamoja wakionyesha hundi ya shilingi milioni mia moja iliyotolewa kwa wakazi wa kata Mvuleni, Manzese mkoani Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kupitia asasi ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS) ili kuboresha makazi yao
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni mia moja kwa wakazi wa kata Mvuleni, Manzese ikiwa ni mkopo uliyotolewa kwa wakazi hao ili kuboresha makazi yao. Mkopo huo ulitolewa na Benki ya Azania kupitia asasi ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS). Kutoka kulia ni Mwakilishi toka UN HABITAT Bw,   Phillemon Mutashubirwa, Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro, na Mkurugenzi wa Bodi ya wakurugenzi ya TAFSUS Bw. John Ulanga.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni mia moja kwa wakazi wa kata Mvuleni, Manzese ikiwa ni mkopo uliyotolewa kwa wakazi hao ili kuboresha makazi yao. Mkopo huo ulitolewa na Benki ya Azania kupitia asasi ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS). Wa kwa kulia ni Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro, na Mkurugenzi wa Bodi ya wakurugenzi ya  TAFSUS Bw. John Ulanga (wa pili kulia) na wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mvuleni, Manzese Bw. Muhidini Lyomeko.
Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni mia moja kwa wakazi wa kata Mvuleni, Manzese ikiwa ni mkopo uliyotolewa kwa wakazi hao ili kuboresha makazi yao. Mkopo huo ulitolewa na Benki ya Azania kupitia asasi ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS) ili kuboresha makazi ya wakazi hao. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa Bodi ya wakurugenzi ya  TAFSUS Bw. John Ulanga, mgeni rasmi wa hafla hiyo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka (wapili kushoto) na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mvuleni, Manzese Bw. Muhidini Lyomeko (wa kwanza kushoto)


Wakazi wa kata ya Manzese na mtaa wa Mvuleni iliyopo Jijini Dar es Salaam wamepokea zaidi ya shilingi milioni 100 kutoka benki ya Azania kwa ajili ya kuboresha makazi yao duni.

Fedha hizo zinazotolewa kwa udhamini wa asasi inayoshughulikia na uboreshwaji wa makazi duni nchini Tanzaia ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS) itatolewa kama mikopo ya kati ya shilingi milioni 1.5 mpaka milioni 9 kwa kila kaya.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika kata ya Mvuleni mwishoni mwa wiki, Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi, Mh. Prof. Anna Tibaijuka alisema mradi wa kuboresha nyumba Manzese Mvuleni umeonyesha mafanikio makubwa na kuboresha maisha ya wakazi hao.

“Ninafurahi kuwepo katika uzinduzi huu wa awamu ya pili na tatu  ya mradi huu, kwani hii ni moja ya juhudi ambazo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ingependa kuziona kote nchini katika  kuboresha makazi ya  Watanzania.

“Kama unavyofahamu, namna bora ya kuboresha maisha ya mwanadamu ni kwanza kuboresha makazi yake.  Ukishakuwa na makazi bora, basi hata afya yako itakuwa bora zaidi, watoto wako wataishi na kukua katika mazingira bora zaidi, watajisomea katika mazingira bora zaidi, na mambo mengine mengi yatakuwa bora zaidi,” alisema Prof. Tibaijuka.

Naye mkurugenzi wa bodi ya wakurugenzi ya TAFSUS Bw. John Ulanga alisema TAFSUS ni chombo cha Kitaifa kinachotoa huduma za udhamini wa kifedha ili kusaidia kuboresha makazi hapa Tanzania hasa katika maeneo ambayo yana changamoto ya ubora wa makazi na ufinyu wa huduma mbalimbali.

“Lengo la msingi la TAFSUS ni kuhamasisha na kuwezesha taasisi za fedha kutoa mikopo ya kuboresha makazi pale ambapo kwa taratibu za kawaida, mikopo hiyo isingetolewa. Mikopo hiyo hutolewa kuboresha makazi yakiwemo yale yasiyo rasmi na kuziwezesha jamii zenye kipato cha chini kuwa na maisha bora,” alisema Bw. Ulanga.

Aliongeza kuwa lengo ni kufikia kaya 2000 na kutekeleza  miradi yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 3.58  kufikia mwishoni mwa  mwaka 2015.

“Ili kutimiza malengo haya, TAFSUS ilipokea dola za kimarekani zipatazo million moja na laki mbili kutoka UN-Habitat, kwa ajili ya kuwezesha miradi ya Jamii kupata mikopo ya uboreshaji makazi,” Bw. Ulanga alisema.

Bw. Ulanga aliongeza kuwa TAFSUS imetenga fungu la fedha la mikopo yenye thamani ya shilingi  250,000,000 kwa ajili ya kuboresha nyumba za Mvuleni, takwimu zikionyesha kwamba mtaa huo wa Manzese Mvuleni una jumla ya kaya 2180 na makadirio ya jumla ya wakazi ni 10,645. 

Ningependa kusema kuwa sisi kama TAFSUS tunajipanga vizuri zaidi kuhakikisha huduma zetu zinakuwa bora zaidi na tunawakifikia watu wengi zaidi, ikiwemo kubuni miradi itayosaidia kuboresha makazi ya Jiji letu na majiji mengine hapa Tanzania, na kuchangia katika kuboresha maisha ya Watanzania hasa wenye kipato cha chini,” Bw. Ulanga aliongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro alisema benki hiyo iliitikia wito wa kutoa mikopo ya riba na masharti nafuu kwa ajili ya kuunga mkoni mradi huo wa kuboresha makazi ya watu, wakitambua kwamba wateja wao wanatokana na jamii, na hivyo kuwasaidia kuboresha maisha yao ni fahari ya benki hiyo.

Wakazi wa Manzese Mvuleni walishauriwa na Waziri Tibaijuka kutumia Ushiriki wa Nyumba (Housing Cooperative) waliyoianzisha kukusanya hela za kutosha na kuchukua mikopo kutoka kwenye mabenki au kushirikiana na wawekezaji wengine kujenga majengo ya vitega uchumi kwenye eneo hilo.

No comments: