*Wajawazito hufukuzwa na kutelekezwa na waume zao.
*Waomba sheria kali zitumike kuwalinda.
*Hali ya kijiografia ni tatizo kuhudhuria tiba kliniki.
"WAJAWAZITO tunapenda kupima afya zetu ili kujua hali tulizonazo,
lakini hali ya unyanyapaa kwa wagonjwa wanaoishi na virusi vya ukimwi
hususani kinamama tunaonyonyesha tunalazimika kujificha kwa kuogopa
kutengwa na familia na jamii kwa ujumla".......
Hiyo ni kauli ya kina mama wajawazito na walioambukizwa virusi vya
(VVU) katika wilaya za Kaliua na Uyui mkoani Tabora wakati walipokuwa
wakiongea na mwandishi wa makala hii.
Hayo yamebainika baada ya ujumbe wa Shirika la EGPAF linalofadhiliwa
na watu wa Marekani kupitia mashirika yake ya USAID na CDC ukiongozwa
na Afisa Mawasiliano Anna Sawaki kutembelea wilaya hizo ili kujua
ukubwa wa tatizo la unyanyapaa, huduma na changamoto zilizopo.
Aidha hatua hiyo pia katika kuendeleza harakati za kuhamasisha elimu
ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi toka kwa mama kwenda kwa
mtoto.
Ujumbe huo ulishuhudia akinamama wanaopata huduma ya afya katika vituo
mbalimbali wakielezea adha wanazopata hasa baada ya kugundulika
wameambukiza virusi vya ukimwi.
Akina mama tuliowakuta katika Zahanati ya kata ya Usinge wilaya ya
Kaliua, kituo cha afya
Misheni Kaliua na kituo cha afya Ilolangulu katika kata ya Ilolangulu
wilayani Uyui walibainisha ukweli huo kuwa baadhi yao wamekuwa
wakipata shida kwa ndugu na jamaa zao na mara kadhaa wametengwa na
familia zao kwa kigezo cha kuambukizwa virusi vya
ukimwi.
Walisema baadhi yao hadi sasa wamefukuzwa na waume zao huku wengine
wakidai waume wamewatelekeza na watoto.
Hata hivyo walieleza kuwa wanapenda kuendelea kutumia dawa za kumkinga
mtoto na virusi vya ukimwi akiwa tumboni kwa wenye ujauzito lakini vitendo vya
kunyooshewa vidole na ndugu zao au jamii, ikiwemo kufukuzwa na wenza imekuwa
ikiwatia hofu kubwa kuhudhuria Zahanati na Vituo vya afya kupata huduma.
Wakielezea zaidi adha wanazokutana nazo walisema wanapenda huduma
zinazotolewa lakini wanashindwa kujiweka wazi kutokana na hali ya
unyanyapaa wa jamii na ndugu ambao wamekuwa wakiwatenga kama
hawastahili kuishi.
Aidha waliongeza kuwa wanakuwa katika wakati mgumu hasa wanapotaka
kwenda kupata dawa ya kupunguza makali ya VVU katika vituo vya afya
kwani mara kadhaa wanalazimika kufanya siri na wenza wao ili ndugu na
jamii wasijue.
Ndugu wanapojua hali zao wanawatenga na kuwanyanyapaa kwa
kiasi kikubwa huku jamii iliyoko mitaani ikiwanyooshea vidole pindi
wanapokuwa katika shughuli za kijamii ama za kuwaingizia kipato na
wanapenda kuwa mabalozi kuhusiana na afya zao lakini wanaamua
kujificha kukwepa adha hiyo, waliongeza.
Hata hivyo wameiomba serikali itupie macho suala hilo japokuwa ipo
sheria inayowalinda waathirika lakini sheria hiyo haijaonyesha makali
yake.
Hali ya kijiografia yawa kikwazo.
Kwa upande mwingine walisema kukosekana kwao kuhudhuria kliniki
wanalazimika kukatisha huduma hiyo kutokana na hali ya kijiografia
kwa mkoa wa Tabora kwani yapo maeneo ambayo usafiri ni wa shida hasa
kutokana na vituo vya kutolea huduma kuwa mbali.
Walisema yapo maeneo ambayo kipindi cha kiangazi usafiri hupatikana
lakini kipindi cha masika hali huwa mbaya kwani usafiri haufiki maeneo
wanayoishi kutokana na hali ya barabara kadhaa kutopitika.
Waliishauri serikali kuangalia namna ya kuboresha miundombinu ya
barabara ili huduma kama hiyo na nyinginezo ziwafikie wote na wazipate
kwa wakati.
Watoa huduma wanazungumziaje.
Mganga wa zahanati ya kata ya Usinge wilaya ya Kaliua Abdulaziz Adinan
Kishangagha alikiri kuwepo tatizo la unyanyapaa japokuwa wamekuwa
wakiendelea kutoa elimu kwa jamii.
Alisema licha ya hali hiyo kuwepo bado kuna wagonjwa ambao wamebainika
kuambukizwa wamekuwa wakikatisha tiba na wengine wakijificha kwa hofu
ya kunyanyapaliwa.
“Kero ya unyanyapaa kwa wagonjwa imekuwa ni kubwa sana kiasi cha
wagonjwa kuamua kujificha…..ikiwemo ukosefu wa vifaa tiba vya wagonjwa
ni vitu ambavyo vinaathiri utendaji wetu.”alisema.
Upimaji wa VVU kwa wajawazito waongezeka.
Meneja wa program ya (EMTCT) katika shirika la EGPAF mkoa wa Tabora
Alphaxard Lwitakubi anasema mwitikio wa upimaji wa virusi wa ukimwi
kwa wajawazito kutoka mwezi februari 2006 hadi machi 2014 hali ya
maambukizi imepungua toka asilimia 3 hadi asilimia 2.3.
Lwitakubi alifafanua wajawazito walioweka wazi kipindi cha 2006 hadi
2014 hali zao ni asilimia 63 wakati waliopata dawa za kuzuia
maambukizi ya (VVU) toka kwa mama kwenda kwa mtoto imepanda toka
asilimia 26 hadi 97 kwa mwaka 2014.
Aidha alisema watoto waliozaliwa na kinamama wenye VVU na kusajiliwa
katika huduma za RCH ni 143 ambao wote waliochukuwa damu ni asilimia
100 na waliogudulika na VVU ni 5 sawa na asilimia 3.4 na wote
wameanzishiwa dawa na vituo vya (PMTCT) meneja alisema vimeongezeka
kutoka vituo 5 katika mwaka 2006 hadi 44 mwaka 2014.
Changamoto zilizopo.
Akizungumzia changamoto alisema ushirikiano mdogo kwa upande wa
wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na upimaji (VVU).
Alitaja changamoto nyingine ni kinamama wajawazito kujifungulia
nyumbani kwa wakunga wa jadi, waliogundulika na (VVU) kupotea na
kutorudi vituoni kutokana na unyanyapaa unaoendelea.
Aidha aliongeza changamoto ya walezi na wazazi kutopeleka katika vituo
watoto waliogundulika wana maambukizi ya (VVU) wapate dawa za ARV,
hali ya jiografia ya mkoa wa Tabora yapo maeneo ambayo vituo viko
mbali, upungufu wa dawa na vifaa tiba.
Namna watakavyokabiliana na changamoto hizo.
Hata hivyo Lwitakubi alibainisha wamejipanga kukabiliana na changamoto
hizo kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu huduma zote za (MHCH),
uagizaji wa dawa,vigaa tiba na vitendanishi.
Aliongeza mipango mingine ni kuendelea kuomba watumishi toka wizara ya
afya na ustawi wa jamii,kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW)
na kutenga bajeti ya kununua mashine za kupima kinga ya mwili CD4.
Mratibu msaidizi wa afya ya uzazi na mtoto anasemaje.
Mratibu msaidizi huduma za Afya ya uzazi na mtoto Audrey Bakuza wa
hospitali ya rufaa Kitete mkoani Tabora anazungumzia huduma ya
Elimination of Mother To Child Transmission of HIV (EMTCT).
Bakuza alisema kabla ya hapo huduma hiyo ilijulikana kama Prevention
of Mother To Child Transmission of HIV (PMTCT) iliyolenga kupunguza
maambukizi ya VVU toka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto lakini sasa
mkakati uliopo ni
kutokomeza kabisa au kuzuia maambukizi.
Bakuza anasema kwa huduma hiyo inajulikana kama huduma mpya ya
Elimination of Mother To Child Transmission of HIV (EMTCT) mjamzito
kabla na baada ya kujifungua.
Alisema katika jitihada za kufanikisha mkakati huo wamekuwa
wakishirikiana na EGPAF, ambapo Wizara ya Afya na ustawi wa jamii
ilitoa maelekezo vituo vya afya kutoa elimu kwa mama mjamzito namna
anavyoweza kujikinga mwenyewe
na namna anavyoweza kumkinga mtoto.
Changamoto wanazokutana nazo.
Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo Bakuza alisema wazazi wengi
hasa akina mama na wenza wao wanaogopa kujitokeza kupima afya na elimu
duni ya wenza wao kugoma kuongozana kuja kupima afya imekuwa tatizo
kwa watoa huduma.
Alitaja changamoto zingine ni upungufu wa watoa huduma za mama na
mtoto , uhaba wa dawa kwa baadhi ya maeneo, ubadilishaji namba za kadi
kwa waliogundulika kuambukizwa.
Mafunzo kwa watoa huduma.
Bakuza anasema kuhusu mafunzo kwa watoa huduma zaidi ya robo tatu
wamepatiwa mafunzo hayo na robo iliyobaki watapatiwa mafunzo kabla ya
mwezi Julai mwaka 2014.
Afisa wa mawasiliano ya shirika la EGPAF Anna Sawaki alisema bado lipo
tatizo katika mwitikio wa huduma za Elimination of Mother To Child
Transmission of HIV (EMTCT) hasa kwa upande wa wanaume na jamii, ipo
haja kuongeza nguvu ya kutafuta ufumbuzi wa kuduma kufikia malengo.
No comments:
Post a Comment