UTANGULIZI
a) Masuala ya Jumla
Mheshimiwa
Spika,
1.
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu
mwenye wingi wa Rehema kwa kutupatia uzima na afya hadi kufikia siku ya leo.
Tumekuwepo hapa kwa takriban miezi miwili ambapo tumeweza kupokea na kujadili
Taarifa za Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na
Mwelekeo kwa mwaka 2014/2015 kwa Wizara mbalimbali na hatimaye kupitisha Bajeti
ya Serikali kwa mwaka 2014/2015.
2.
Napenda kutumia nafasi hii ya awali
kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi nzuri ya kutukuka ambayo
wameifanya kwa nidhamu na ufanisi mkubwa, hususan wakati wa Mjadala wa Bajeti
ya Serikali na Mafungu ya Wizara za Kisekta. Kipekee niwashukuru Wajumbe wa
Kamati ya Bajeti chini ya Uongozi mahiri wa Mheshimiwa Mtemi Andrew John Chenge, Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi kwa
kazi yao nzuri ya kuchambua Bajeti ya Serikali na Sheria zinazoambatana na
masuala ya Bajeti. Changamoto zilikuwa nyingi, lakini kwa pamoja tumekubaliana
na kuafikiana.
Kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kwenda kushirikiana na Wananchi katika utekelezaji
wa Bajeti hii ili kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa
Spika,
3.
Katika kipindi hiki tukiwa hapa Bungeni, yapo
matukio ya kusikitisha yaliyotokea ambapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge
walipoteza Wapendwa wao. Aidha, yapo matukio ya Kitaifa yaliyosababisha
kupoteza maisha ya Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda kutumia nafasi hii kuwapa
pole Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote waliofikwa na misiba na majanga
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wote waliopotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki.
Mheshimiwa
Spika,
4.
Kipekee niwape pole ndugu, jamaa na marafiki
waliopotelewa na ndugu zao na wote waliopata majeraha wakati kulipotokea
Mlipuko wa Bomu pale Darajani, Zanzibar. Tukio hili la kusikitisha halipendezi
kwa Nchi yetu. Niwaombe Wananchi wote kwa umoja wetu tushirikiane kuwa Walinzi
katika maeneo yetu na kuwezesha kuwatambua mapema wale wote wenye nia mbaya ya
kuharibu amani na utulivu katika Nchi yetu.
b) Shughuli za Bunge
Mheshimiwa
Spika,
5.
Katika Mkutano huu Waheshimiwa Wabunge
walipata fursa ya kufanya uchaguzi wa Wajumbe wa Wawakilishi kwenye Bodi za
Taasisi, Mabaraza na Tume za Bunge. Napenda nitumie nafasi hii kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. Terezya Luoga Huvisa,
Mbunge wa Viti Maalum kuwa Mjumbe
katika Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere; Mheshimiwa Goodluck Joseph Ole-Medeye, Mbunge wa Arumeru Magharibi kuwa Mwakilishi wetu
katika Bunge la Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC-PF); Mheshimiwa
Alphaxard Kangi Lugola, Mbunge wa Mwibara kuwa Mjumbe katika Tume ya
Utumishi wa Bunge; Mheshimiwa Henry
Daffa Shekifu, Mbunge wa Lushoto; Mheshimiwa Sylvester Massele, Mbunge wa Dole; na Mheshimiwa Zainab
Rashidi Kawawa, Mbunge wa Viti
Maalum wote kuwa Wajumbe katika Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Beatrice
Matumbo Shelukindo, Mbunge wa
Kilindi na Mheshimiwa Dkt. Maua
Abeid Daftari, Mbunge wa Viti Maalum
kuwa Wajumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi – Muhimbili; na
mwisho nimpongeze Mheshimiwa Rashid
Mfutakamba, Mbunge wa Igalula kuwa
Mjumbe wa Bodi ya Utawala ya Chuo cha Ufundi Arusha. Tunaamini wote
waliochaguliwa watatuwakilisha vyema katika Taasisi hizo.
Mheshimiwa
Spika,
6.
Pamoja na kupokea, kujadili na kupitisha
Bajeti ya Serikali, jumla ya Maswali 321
ya Msingi na 879 ya Nyongeza yaliulizwa
na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 37 ya Msingi na 30 ya Nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Papo kwa
Papo kwa Waziri Mkuu.
7.
Nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge
wote kwa kuuliza Maswali ambayo yalilenga katika kuwaletea Wananchi maendeleo
katika Majimbo yetu na kwa Taifa letu kwa ujumla. Vilevile, niwapongeza Mawaziri
na Naibu Mawaziri wote ambao wamefanya kazi kubwa ya kuandaa majibu na maelezo
ya ziada katika kila Swali lililoulizwa.
c) Miswada, Maazimio na Kauli za Serikali
Mheshimiwa
Spika,
8.
Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge
walipata fursa ya kujadili Miswada, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri.
Miswada iliyowasilishwa na Serikali na kukamilisha hatua zote ni Muswada wa
Sheria wa Fedha wa Mwaka 2014 [The Finance Bill 2014]; na Muswada
wa Sheria wa Kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2014 [The
Appropriation Bill, 2014].
Mheshimiwa
Spika,
9.
Miswada ifuatayo imesomwa kwa mara ya kwanza:
i)
Muswada wa Sheria wa Kufanya Marekebisho katika
Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa 2014 [The
Public Private Partnership (Amendment) Act, 2014] ulisomwa kwa mara ya
kwanza.
ii)
Muswada wa Sheria ya Utawala wa Kodi 2014 (The Tax Administration Act 2014);
iii)
Muswada wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali [Miscellaneous (Amendments) Bill 2014]; na
iv)
Muswada wa Sheria Mpya ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani [The Value Added Tax Act, 2014] unaopendekeza kufuta Sheria ya
Kodi ya Ongezeko la Thamani.
d) Maazimio
Mheshimiwa
Spika,
10.
Vilevile, katika Mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge pia walikubali Maazimio ya Bunge kama ifutavyo:
i)
Azimio la kuridhia kubadilisha Chuo cha
Maendeleo ya Jamii Tengeru kuwa Taasisi inayojitegemea kiutendaji [Tengeru
Institute of Community Development (Establishment Order, 2013)];
ii)
Azimio la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Fedha
na Uwekezaji (SADC Protocal on Finance and Investment);
iii)
Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kuanzisha Umoja
wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki [Protocol on the Stablishment of the East
African Community Monetary Union].
Kauli
za Mawaziri
Mheshimiwa
Spika,
11.
Katika Mkutano huu pia Mawaziri waliweza
kutoa Kauli za Serikali zifuatazo:
i)
Kauli ya Waziri wa Maji Kuhusu Matatizo ya
Uzalishaji Maji katika Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu;
ii)
Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii
Kuhusu Ugonjwa wa Homa ya Dengue;
iii)
Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii
Kuhusu Hali ya Mashine za Mionzi za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI).
SERIKALI
ILIVYOJIPANGA KUTEKELEZA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI MWAKA 2014/2015
Mheshimiwa
Spika,
12.
Wakati wa Mjadala wa Mpango na Bajeti ya
Serikali ya mwaka 2014/2015; Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili na
kutoa maoni na ushauri kuhusu Sera na Mikakati iliyopangwa na Serikali ya
kuimarisha maandalizi na usimamizi wa utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya
Serikali. Tunashukuru kwa michango hiyo mizuri ambayo Serikali inaahidi
kuifanyia kazi.
Mheshimiwa
Spika,
13.
Napenda kutumia fursa hii kuungana na
Waheshimiwa Wabunge wengine kuwapongeza Mheshimiwa Stephen Masato Wasira (Mb.)
- Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu; na Mheshimiwa Saada Mkuya
Salum (Mb.) - Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha vizuri Hotuba za Mpango na Bajeti
ya Serikali na pia kutoa maelezo mazuri ya ufafanuzi wakati wa kuhitimisha Hoja
hii tarehe 24 Juni 2014. Vilevile,
nawapongeza Mawaziri wa Kisekta na Naibu Mawaziri kwa kuwasilisha Bajeti za
Wizara zao kwa umahiri mkubwa. Pamoja na pongezi hizo, napenda kutoa msisitizo
katika maeneo machache yafuatayo:
a)
Kuimarisha
utengemavu wa Viashiria vya Uchumi Jumla
Mheshimiwa Spika,
14.
Ukuaji wa uchumi jumla
ulio endelevu unahitaji mazingira ya uchumi jumla yaliyotengamaa na
yanayotabirika. Mwenendo wa ukuaji wa uchumi katika miaka ya hivi karibuni
umekuwa ukiongezeka na kufikia wastani wa Asilimia
7 kwa mwaka licha ya changamoto za upandaji bei za chakula na mafuta ya
petroli katika soko la dunia. Ili kuweza kuendeleza ukuaji huu mzuri wa uchumi
hapana budi kuendelea kutengamaza vigezo muhimu vya uchumi jumla, ikiwa ni
pamoja na kuendeleza na kuimarisha Ukuaji halisi wa Pato la Taifa na kukua kwa
kiwango cha juu zaidi ya Asilimia 7.0;
kudhibiti kasi ya upandaji bei kwa kuhakikisha kwamba kiwango cha mfumuko wa
bei ni chini ya tarakimu moja, ikiwezekana kisichozidi Asilimia 5; na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili
kupunguza utegemezi. Kutengamaza viashiria hivi kutaihakikishia Nchi yetu
kuendelea kwa kasi katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini hasa ule wa
kipato kwa Wananchi wetu wengi wa Vijijini. Tayari dalili nzuri zinaanza
kujitokeza, kwani kiwango cha Watanzania walio katika umaskini kimepungua
kutoka Asilimia 33.6 mwaka 2007 hadi Asilimia 28.2 mwaka 2012. Aidha, wastani
wa Pato la Mwananchi kwa mwaka limeongezeka kutoka Shilingi 516,000 mwaka 2007
hadi Shilingi 1,003,000 mwaka 2012.
b) Kuimarisha utaratibu na usimamizi wa
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015
Mheshimiwa
Spika,
15.
Mwaka 2014/2015, ni wa
Nne wa utekelezaji wa Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 –
2015/2016). Ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango unafikia malengo
yaliyokusudiwa, Serikali imeiagiza Tume ya Mipango kuendelea na utaratibu wa
kukagua na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya Maendeleo ya
kipaumbele na ile ya kimkakati ili kuhakikisha kuwa inatekelezwa kwa kuzingatia
viwango vya ubora vilivyokubalika na inalingana na thamani ya fedha
zilizotolewa na Serikali (Value for money).
Vilevile, kuhakikisha kuwa Miradi hiyo inakamilika kwa wakati; na pale ambapo
kuna changamoto za kiutekelezaji kutoa ushauri stahiki Serikalini wa njia za
kufanikisha miradi husika. Kwa upande wa miradi inayotekelezwa katika ngazi za
Sekretariati za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo inasimamiwa na
Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Serikali itaimarisha mfumo wa ufuatiliaji kwa
kuzingatia uzoefu uliopatikana katika mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” (Big Results Now – BRN).
Mheshimiwa Spika,
16.
Sambamba na hatua hizo,
napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali imeanza kufanya mapitio
ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016).
Lengo la mapitio hayo ni kupima hatua ya utekelezaji wa mpango na kubaini
changamoto pamoja na kuweka mikakati ya maandalizi ya Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021). Taarifa
ya mapitio ya Nusu ya Kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2011/2012 – 2015/2016), itatolewa Desemba 2014. Madhumuni ya
Taarifa hii ni kuhakikisha kuwa maeneo ambayo hayakutekelezwa ipasavyo na
maeneo mapya yaliyoibuka (emerging issues)
hususan kuiandaa nchi kwa uchumi wa gesi
na umuhimu wa kuimarisha ushindani wa Tanzania katika uzalishaji na biashara ya
Kimataifa.
c) Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa
Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa
Spika,
17.
Kutokana na michango mizuri ya mawazo ambayo
Serikali imepokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wakati wa Mjadala wa Bajeti ya
Serikali na Mafungu ya Wizara za Kisekta, Serikali
imejipanga vizuri zaidi kuimarisha ukusanyaji wa Mapato katika Mwaka 2014/2015.
Hata hivyo, ni vyema Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa kwenye eneo la mapato
yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Serikali ya awamu ya nne
imefanikiwa kuongeza mapato hayo kutoka Wastani wa Shilingi Bilioni 117 kwa mwezi Mwaka 2005/2006
hadi Wastani wa Shilingi Bilioni 800
kwa Mwezi mwaka 2013/2014. Ongezeko hilo
ni sawa na Asilimia 351. Lengo la
Serikali ni kuongeza kasi zaidi katika eneo hili hata kuzidi kiwango hiki.
Mheshimiwa
Spika,
18.
Pamoja na kuipongeza TRA kwa jitihada hizo, Serikali itafanyia kazi maoni mbalimbali ya
Waheshimiwa Wabunge ya kupanua wigo wa vyanzo vya Kodi pamoja na taarifa
zilizopatikana zinazoonyesha kwamba bidhaa nyingi zinapita kwenye bandari bubu
au vituo vya forodha bila kulipakodi stahiki.
Hatua za kupunguza misamaha ya Kodi zitaendelea kuimarishwa. Aidha, napenda
kutumia fursa hii kuielekeza Mamlaka ya mapato Tanzania kuongeza ufanisi wa
kiutendaji na kuimarisha zaidi miundo ya ukusanyaji na ulipaji kodi. Ni muhimu,
Mamlaka ya Mapato kurahisisha zaidi taratibu za kukusanya Kodi kwa kuweka na
kutangaza kwa uwazi Kodi zinazostahili kulipwa kulingana na aina ya bidhaa na
kuondokana na utaratibu wa kufanya makadirio au kutumia mwanya wa majadiliano
na walipa kodi jambo ambalo linaweza kutoa mwanya kwa rushwa na hivyo
kuikosesha Serikali Mapato yake stahiki. Vilevile, naviagiza Vyombo vya Ulinzi
na Usalama kutoa ushirikiano wa kutosha katika kudhibiti na kuzuia ukwepaji wa kodi na ushuru katika bandari
zetu na maeneo ya mipakani.
Mheshimiwa
Spika,
19.
Ni imani yangu kuwa tukiweka wazi kodi
zinazopaswa kulipwa na tukirahisisha
taratibu za kukusanya Mapato ya Kodi hususan Bandarini na maeneo ya mipakani
tutaweza kuweka mazingira mazuri ya kusaidia kuongeza mapato ya Serikali na
kupunguza urasimu na vishawishi vya kudai Rushwa. Nashauri, Mamlaka ya Mapato
Tanzania ijipange upya vizuri ili kuhakikisha kwamba jukumu la kukusanya kodi
linatekelezwa vizuri na kwa weledi mkubwa. Tukiwa na uhakika wa makusanyo ya
mapato yetu ya ndani, naamini tutakwenda vizuri.
Mheshimiwa
Spika,
20.
Kuhusu mapato yasiyotokana na Kodi hususan
Maduhuli, uzoefu wa mwaka 2013/2014 umeonesha kwamba mwenendo wa ukusanyaji wa
mapato hayo hauridhishi. Kwa mfano, kuanzia Mwezi Julai, 2013 hadi Aprili,
2014; Makusanyo yasiyotokana na Kodi yalifikia Shilingi Bilioni 425.5 ikiwa ni Asilimia 57 ya lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 741.1 kwa mwaka. Aidha, kwa upande wa mapato ya
Halmashauri, makusanyo yalifikia Shilingi Bilioni
252.8, sawa na Asilimia 66 ya
makadirio ya mwaka. Mwenendo huo nao
hauridhishi hivyo, ni lazima sasa tujipange upya kuhakikisha malengo yanafikiwa.
Mheshimiwa
Spika,
21.
Ili
kuimarisha ukusanyaji wa Mapato yatokanayo na Kodi na yasiyo ya Kodi (Non-Tax Revenue) na ya Halmashauri
kuanzia Mwaka ujao wa Fedha, Wizara zenye jukumu la kukusanya Kodi na Maduhuli
pamoja na makusanyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala za Serikali, Idara
za Serikali zinazojitegemea kuanzia sasa zitatakiwa
kuandaa Mpango Mkakati na Mpango Kazi (Action Plan) wa mwaka wa kukusanya
Mapato na Maduhuli yao yote na kutoa
taarifa bila kukosa kwa Katibu Mkuu,
Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu
makusanyo ya kila robo mwaka; ifikapo tarehe 15 ya mwezi unaofuata kila baada ya robo mwaka ambaye atawasilisha
taarifa hiyo ya utekelezaji kwenye Kamati Ndogo za Baraza la Kazi la Baraza la
Mawaziri zinazohusika kwa ajili ya tafakuri na maelekezo.
Mheshimiwa
Spika,
22.
Tayari Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu
ameagizwa kuandaa utaratibu mzuri wa kupata Taarifa za Makusanyo ya Mapato
yatokanayo na Kodi na Maduhuli kutoka Wizara na Taasisi zote za Serikali
zinazojitegemea. Aidha, naagiza kila Katibu Mkuu wa Wizara, Wakurugenzi wa
Halmashauri na Watendaji Wakuu wote wa Taasisi, Wakala za Serikali na Idara za
Serikali zinazojitegemea kuhakikisha
zinakusanya Mapato kulingana na Mpango Mkakati wa Mpango Kazi na kuwasilisha
Taarifa hizo kwa wakati.
MISAMAHA
YA KODI
Mheshimiwa
Spika,
23.
Eneo la misamaha ya Kodi limekuwa
likilalamikiwa na Wananchi wengi na Waheshimiwa Wabunge kwa muda mrefu. Katika
eneo hili, ni vyema Wananchi na Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa kuna misamaha
ya Kodi ya aina mbalimbali. Kundi la Kwanza ni misamaha ya Kodi
inayotolewa kwa Washirika wetu wa maendeleo wanaotoa misaada katika miradi
mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi linajumuisha pia misamaha ya bidhaa za
Sukari, Mchele, Mafuta ya Diseli, n.k. Kundi la Pili ni misamaha ya Kodi kwa
Asasi zisizo za Kiserikali na Mashirika ya Dini yanayotoa huduma kwa Wananchi
pasipo kutegemea kupata faida. Kundi la Tatu ni misamaha ya Kodi
ambayo hutolewa ikiwa ni Mkataba wa kuvutia Uwekezaji Nchini. Kwa kawaida Misamaha ya aina hii hutolewa
kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) ili kuvutia Uwekezaji katika Miradi Mikubwa
ambayo tunategemea kuwa manufaa yatakayopatikana kutokana na uwekezaji huo
yatakuwa makubwa sana ikilinganishwa na msamaha wa kodi uliotolewa. Kwa mujibu
wa Takwimu za hivi karibuni za Mamlaka ya Mapato Tanzania za Mwaka 2012/2013
zinaonesha kuwa Misamaha ya Kodi ya bidhaa za mtaji kwa Wawekezaji waliopewa
Hati za Usajili na Cheti cha hadhi ya Uwekezaji mahiri kupitia Kituo cha
Uwekezaji (TIC) ni Asilimia 19.7 ya
Misamaha yote.
24.
Kwa mfano, utafiti uliofanywa na Kituo cha
Uwekezaji TIC mwaka 2012 kwa Makampuni Makubwa 50 ya Uwekezaji yaliyosajiliwa
na TIC, kiasi kilichowekezwa katika kipindi cha miaka mitano (2005 – 2010), ni
Shilingi Trilioni 1.7 ambapo katika
uwekezaji huo, Makampuni hayo yalilipa Kodi Shilingi Trilioni 1.1. Aidha, Makampuni hayo yalitoa ajira 981,000 za moja kwa moja na 112,070 zisizo za moja kwa moja.
Misamaha ya Kodi iliyotolewa kwa Makampuni hayo ni Asilimia Saba (7) tu ya Kodi
yote iliyolipwa na Makampuni hayo. Misamaha kwa makundi mengine ikiwemo Miradi ya Wahisani mbalimbali
na Asasi zisizo za Serikali (NGOs), n.k ni Asilimia 38.6; na Misamaha kwa Sekta Binafsi ni Asilimia 23.8 ya Misamaha yote iliyotolewa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mheshimiwa
Spika,
25.
Serikali inatambua kuwa bado tuna kazi ya
kubwa ya kuhakikisha kwamba misamaha ya kodi inayotolewa kwa Wawekezaji na
Walengwa wengine Nchini inatumika vizuri katika miradi iliyokusudiwa, na si
vinginevyo. Kwa mfano, msamaha wa kodi uliotolewa kwenye mafuta ya dieseli
hatutarajii mafuta hayo yaingie sokoni badala ya kutumika kwenye mradi wa
uwekezaji uliokusudiwa. Hivyo, kutokana na umuhimu wa kuvutia uwekezaji Nchini,
misamaha ya kodi iiliyoidhinishwa na Bunge Kisheria itaendelea kutolewa kwa Wahusika.
Nitoe wito kwa wote watakaopata misamaha
hii kuwa waadilifu na kuitumia kwa
malengo yaliyokusudiwa. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yoyote
atakayetumia vibaya misamaha hii. Serikali kwa upande wake itaimarisha zaidi
usimamizi wa matumizi ya misamaha hii na itahakikisha inatumika kwa lengo
lililokusudiwa.
KUONDOA
URASIMU KATIKA VITUO VYA FORODHA
Mheshimiwa
Spika,
26.
Mwezi Februari, 2014 nilipokutana na
Wafanyabiashara waliotaka kugoma kutumia Mashine za kisasa za kutoa Risiti (Electronic Fiscal Devise-EFD)
walinieleza kwamba moja ya eneo linalowasumbua ni urasimu mkubwa katika maeneo
mengi ya Vituo vya Forodha Mipakani na Bandarini hasa Dar es Salaam. Katika Vituo hivyo
vya Forodha walisema zipo Taasisi nyingi
za Serikali zinazofanya ukaguzi wa mizigo inayoingizwa Nchini na ile
inayotoka kwenda Nje ya Nchi. Miongoni mwa Taasisi hizo ni pamoja na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA); Idara ya Uhamiaji; Jeshi la Polisi; Wakala wa Viwango
(TBS); Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA); Mkemia Mkuu wa Serikali;
Tume ya Nguvu za Atomiki; Idara ya Misitu na Nyuki; Taasisi ya Utafiti wa Dawa
za Mimiea na Wadudu (TPRI); Kitengo cha Afya ya Mimea cha Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika; na Kitengo cha Afya ya Mifugo cha Wizara ya Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa
Spika,
27.
Serikali iliweka Taasisi nilizozitaja hapa kwa
nia njema ya kusimamia vizuri na kudhibiti uingizaji na utoaji wa mizigo
bandarini na bidhaa zinazopitishwa katika mipaka ya Nchi yetu. Hata hivyo,
baadhi ya Watendaji wasio waaminifu wanatumia mwanya huo kuwalazimisha
Wafanyabiashara kutoa fedha zao bila kupata risiti eti kwa ajili ya kusaidia
mizigo kupitishwa kwa urahisi. Aidha, nimeelezwa kuwa baadhi ya Watendaji
wanatumia nafasi zao kuongeza urasimu usio na lazima ili kudai rushwa, jambo
ambalo linaongeza gharama kwa Wafanyabiashara na kuleta athari za kuchelewesha
utoaji wa mizigo bandarini na kuathiri sifa za bandari zetu. Naagiza Wizara husika kufuatilia utendaji
kazi wa Vyombo hivyo kwa karibu na kushughulikia kwa haraka malalamiko
mbalimbali na kupata ufumbuzi wa tatizo la urasimu katika Vituo vya Forodha.
Yapo Makampuni ya Mawakala yapatayo 527
yanayofanya kazi za Mawakala wa kutoa bidhaa Bandarini. Tunayo taarifa kuwa, Utitiri wa Makapuni hayo nao umekuwa
chanzo kikubwa cha rushwa na ukwepaji Kodi. Serikali haikubaliani na aina hii
ya Utendaji wa Makampuni hayo. Utendaji huo uachwe sasa. Navitaka Vyombo husika
kufuatilia kwa karibu sana mienendo ya Makampuni yote ya Mawakala wa kutoa
bidhaa Bandarini na kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa
Spika,
28.
Pamoja na changamoto zilizopo katika bandari
zetu, napenda kutumia fursa hii kumpongeza Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt.
Harrison Mwakyembe (Mb.) kwa kazi kubwa anayofanya ya kusimamia kwa karibu
uboreshaji wa utendaji katika Mamlaka ya Bandari; hasa kupunguza muda wa kutoa
mizigo bandarini kutokana na kuweka utaratibu wa kufanya kazi kwa saa 24.
Ninamtaka aongeze juhudi zaidi ili kuimarisha utendaji kazi katika eneo hili
ili kuongeza sifa kwa Bandari zetu.
UTEKELEZAJI
WA MIRADI YA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG
RESULTS NOW-BRN)
Mheshimiwa
Spika,
29.
Utekelezaji wa mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa
umeendelea vizuri, na licha ya matatizo ya upatikanaji wa fedha matokeo yake
yameanza kuonekana kama ilivyoainishwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta husika
walipowasilisha Hotuba zao katika Mkutano huu. Uzoefu tulioupata katika kipindi
hiki, ni kwamba upatikanaji wa matokeo makubwa kwa muda mfupi unawezekana,
ilimradi tuwe tumechagua vipaumbele vyetu kwa usahihi, tunafuatilia utekelezaji
kwa karibu, na kutanzua changamoto mara zinapojitokeza. Napenda kutumia fursa hii
tena kuwashukuru Wadau wote wa Maendeleo waliowezesha kupata matokeo haya.
Natoa wito kwa Viongozi na Watendaji katika ngazi zote tuendeleze kasi na
umakini wa kufuatilia utekelezaji wa Miradi ya kipaumbele ya Mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” ili
tuweze kufanikiwa zaidi katika kipindi kijacho.
Mheshimiwa
Spika,
30.
Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu
kwamba katika Mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha mchakato wa Ajira za
nafasi wazi za Watumishi wa Taasisi ya Kuratibu na Kusimamia Mfumo wa Tekeleza sasa kwa Matokeo Makubwa
kilichopo Ofisi ya Rais, yaani President’s
Delivery Bureu (PDB). Vilevile, Serikali itaimarisha Vitengo na Taasisi
zote zinazosimamia mfumo huu, ikiwa ni pamoja na kukamilisha uundaji wa Vitengo
na Kamati za kuratibu utekelezaji katika Wizara na Taasisi zinazotekeleza
Programu ya Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara Nchini. Serikali pia itaandaa
na kutangaza matokeo ya utekelezaji wa mfumo huu katika mwaka wake wa kwanza wa
2013/2014, baada ya kuhakikiwa na jopo huru la Kimataifa. Hatua hii
inalenga kukamilisha mfumo wa uwajibikaji ambao ni chachu muhimu ya mafanikio
ya mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Vilevile, Wizara zingine, Mikoa na Halmashauri zote zinaendelea
kuhimizwa kutumia mfumo huu katika kuchambua, kupanga, na kutekeleza mipango na
miradi yake yote ya maendeleo kwa kuzingatia mfumo huu wa Matokeo Makubwa Sasa.
KILIMO
Hali ya
upatikanaji wa Chakula Nchini
Mheshimiwa
Spika,
31.
Hali ya upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuwa ya kuridhisha
katika maeneo mengi kufuatia albaki ya mavuno ya msimu uliopita na matarajio ya
mavuno mazuri katika msimu wa kilimo wa 2013/2014 ambayo uvunaji wake umeanza
katika baadhi ya maeneo. Aidha, kufuatia mwenendo mzuri wa hali ya unyeshaji wa
mvua katika msimu wa 2013/2014 katika maeneo mengi ya nchi, kuna matarajio ya
uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na hivyo upatikanaji mzuri zaidi wa
chakula kwa mwaka 2014/2015.
Mheshimiwa
Spika,
32.
Hali ya akiba ya chakula katika Maghala ya
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ni nzuri. Mwanzoni mwa mwaka 2013/2014
Akiba ya Chakula ilikuwa Tani 25,452.6
na baada ya kununua Tani 219,377.3,
akiba ilifikia Tani 244,829.9. Hadi
kufikia tarehe 4 Juni 2014 Serikali ilitoa Jumla ya Tani 54,845.0 kama chakula cha Msaada na Maafa ikiwemo njaa,
mafuriko na operesheni mbalimbali na kubaki na akiba ya Tani 189,984.9. Aidha, Serikali ina mpango
wa kuuza Tani 75,000 ili kuacha Maghala
wazi kwa ajili ya mazao mapya yatakayonunuliwa katika msimu mpya wa 2014/2015
na hivyo, kuyaacha Maghala ya Serikali yakiwa na Akiba ya Tani 114,984.9 za Mahindi ifikapo Julai, 2014. Katika mwaka
2014/2015 Serikali itanunua Tani 160,000
za Nafaka na kuzijumlisha zile za
akiba kutoka msimu wa 2013/2014, hivyo kuwa na hifadhi ya jumla ya Tani 274,984.9 za Nafaka.
Mheshimiwa
Spika,
33.
Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu na Wananchi
kuwa Serikali kwa mara ya kwanza imefikia uamuzi wa kununua Mpunga na kuhifadhi
katika Maghala ya Taifa kama Chakula cha Akiba. Uamuzi huu umefikiwa kwa
kuzingatia kuwa baada ya Serikali kuruhusu wafanyabiashara kuingiza mchele
kutoka nje ya Nchi kufidia pengo la upungufu wa mchele hapa Nchini, baadhi ya wafanyabiashara
hao waliendelea kuingiza mchele hata baada ya muda wa vibali vyao kuisha hivyo
kuwafanya Wakulima kukosa soko la mpunga baada mavuno kuongezeka. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa katika msimu huu wa mavuno, Serikali
imedhamiria kuanza na hifadhi ya Tani 10,000 za mpunga kwa lengo la
kujiridhisha kama hifadhi ya mpunga haitakuwa na matatizo. Baada ya
kujiridhisha, katika misimu inayofuata, Serikali itaongeza kiasi cha Mpunga
utakaohifadhiwa na Serikali kwa nia ya kuziba pengo la upungufu wa mchele iwapo
hali hiyo itatokea badala ya kutegemea Wafanyabiashara tu kuagiza Mchele kutoka
nje ya Nchi. Nitumie fursa hii kuwahimiza wakulima kuongeza uzalishaji wa zao
hili kwa vile sasa Serikali imeamua kuhifadhi Mpunga kama ilivyo kwa Mahindi na
Mtama. Aidha, niwaahidi Wananchi kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu
ya kuhifadhi mpunga katika Maghala ya Taifa ili kuwawezesha Wakulima wengi
kupata soko kama ilivyo kwa mazao ya Mahindi na Mtama. Ninaagiza kuanzia sasa Taasisi
zote zinazotoa vibali vya kuingiza sukari, mchele na ngano kutoka nje ya nchi
kuhakikisha kuwa Wafanyabiashara wenye vibali vinatumika tu kwa muda uliopangwa.
Mheshimiwa
Spika,
34.
Naagiza pia kwa Wakala wa Hifadhi Taifa ya
Chakula kuanza kununua nafaka kwa wakati ili wakulima waweze kunufaika na bei
nzuri zitakazotolewa. Ni matarajio yangu kuwa Wakala pamoja na kununua nafaka
kwa bei ya soko na kupitia vituo vya ununuzi, vikundi vya wakulima na mawakala,
watahakikisha kuwa wakulima hasa wa mahindi wanapata si chini ya Shilingi
500
kwa kilo ambayo ni bei ya msimu uliopita ili
kuwawezesha kurudisha gharama za uzalishaji. Aidha, nawasihi Wakulima
wasikubali kuuza mazao yao chini ya bei hiyo. Lengo ni kuwawezesha kurejesha
gharama za uzalishaji. Bei elekezi kwa nafaka nyingine pia zitangazwe kwa kuzingatia
gharama za uzalishaji mapema kabla ya msimu wa ununuzi kuanza. Nichukue fursa
hii kuwasihi Wananchi hasa katika Kanda zile wanazouza nafaka iliyo na ubora
hafifu hasa uchafu kujirekebisha na kuacha tabia hiyo mara moja, kwani kwa
kufanya hivyo wanavuruga jitihada za Serikali za kusaidia Wakulima Wadogo
kuinua maisha yao.
Mazao ya
Asili ya kuingiza Fedha za Kigeni
Mheshimiwa
Spika,
35.
Nchi yetu inayo mazao yanayotuingizia fedha
za kigeni ikiwa ni pamoja na Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Tumbaku n.k. Kwa
madhumuni ya Hotuba yangu ya leo nimeona nizungumzie uendelezaji wa mazao ya
Korosho na Pamba. Kutokana na bei ya mazao haya kuendeea kutegemea bei katika Soko
la Dunia, Wakulima wetu wameendelea kupata bei za chini na zisizokuwa na
uhakika kila msimu wa mauzo unapowadia. Hivyo, ni vyema sasa tukazingatia
umuhimu wa kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa soko la ndani linakuwa la
uhakika kwa mazao haya. Aidha, Serikali imekuwa ikiweka mikakati ya kusindika
mazao ya Pamba na Korosho hapa Nchini kwa lengo la kuyaongezea thamani na
kuongeza Tija katika uzalishaji kwa eneo. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali
sasa imejikita katika utafiti wa mbegu na miche bora pamoja na kufufua viwanda
ambavyo vitatumia malighafi zitokanazo na mazao haya hapa Nchini.
Mapango wa
kufufua Viwanda vya Korosho
Mheshimiwa
Spika,
36.
Uzalishaji wa korosho umeendelea kuwa tegemeo
kubwa la wakulima wa Mikoa ya Kusini ya
Lindi na Mtwara na pia Mkoa wa Pwani. Kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali
za kufufua zao hili, katika msimu wa 2013/2014, uzalishaji wa Korosho
umeongezeka hadi kufikia Tani 127,939.4
ikilinganishwa na Tani 121,703.8 kwa
msimu wa 2012/2013. Pamoja na ongezeko katika uzalishaji, mchango wa zao hili
kwa Pato la Mkulima na Taifa umekuwa mdogo kutokana na Taifa kuendelea kuuza
korosho ghafi nje ya Nchi kwa zaidi ya Asilimia 90 hivyo, kuikosesha Nchi mapato na faida nyingine nyingi kwa
wakulima. Hali hii imetokana na Wawekezaji wa Viwanda 12 vya kubangua korosho
vilivyojengwa na Serikali miaka ya 1980 na kubinafsishwa mwaka 2004 kushindwa
kuvifufua viwanda hivyo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa mitaji
na kuendelea kutumia Teknolojia iliyopitwa na wakati.
Mheshimiwa
Spika,
37.
Napenda
kulijulisha Bunge lako na wananchi kwamba kutokana na changamoto hizo, mwezi
Februari, 2014 niliitisha Kikao kilichohusisha baadhi ya Watendaji Wakuu wa
Serikali, baadhi ya Wamiliki wa Viwanda vya kubangua Korosho na baadhi ya
Taasisi ya Fedha kujadili mikakati ya kufufua viwanda vya kubangua korosho hapa
nchini. Hivyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau hao iliamua ifanyike tathmini
ya gharama na mikakati ya kufufua Viwanda vya kubangua korosho hatua kwa hatua
na kwa kuanzia Serikali kwa kushirikiana na Wamiliki itaanza kufufua Viwanda
vinne (4) vyenye uwezo wa uzalishaji (Installed
Capacity) wa kati ya Tani 5,000
hadi 10,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa
Spika,
38.
Kwa kuanzia Serikali iliamua tathmini
ifanyike kwa viwanda vya Newala-I; Masasi; Lindi
Farmers kilichopo Nachingwea; na Kiwanda cha Kampuni ya BUCCO kilichopo
Lindi kwa ushirikiano kati ya Serikali na Kampuni ya Oltremare ya Italy ambayo
ina uzoefu mkubwa duniani katika utengenezaji wa mashine za usindikaji wa
Korosho. Kampuni hii ndiyo iliyojenga baadhi ya viwanda vya kubangua korosho
hapa nchini kikiwepo Kiwanda cha TANITA. Tathmini hii itaangalia hali ilivyo
katika masuala ya kiufundi, usindikaji na miundombinu; uwezo na madeni ya
Kifedha; Masuala ya Kisheria kuhusu Mikataba mbalimbali iliyowekwa na
wawekezaji hawa, Mfumo wa upatikanaji wa malighafi; na uwezo wa Rasilimali watu
wa viwanda hivyo.
Mheshimiwa
Spika,
39.
Tathmini ya awali ya gharama za kufufua
viwanda hivyo vinne iliyofanywa na Kampuni ya Oltremare kwa kushirikiana na
Kampuni ya Agrofocus ya hapa Tanzania ilibaini kuwa kuna njia mbili zinazoweza
kutumika: Kwanza, iwapo Serikali
itaamua kuvifufua Viwanda vya Newala 1; Masasi na Lindi kwa kuvijengea uwezo wa
kila kimoja kubangua Tani 15,000 kwa
mwaka, pamoja na cha Nachingwea kubangua Tani 7,500 kwa mwaka; kwa pamoja
zitahitajika jumla ya Paundi 31,280,690.
Pili, iwapo Serikali itaamua kuvifufua
viwanda vya Newala 1, Masasi na Lindi kwa kuvijengea uwezo wa kila kimoja kubangua Tani
22,000 kwa mwaka, na Kiwanda cha Nachingwea kubangua Tani 7,500 kwa mwaka,
kwa pamoja zitahitajika jumla ya Paundi
44,185,022. Hata hivyo, kabla ya kuweka mikakati ya kupata fedha hizo,
Serikali imeamua kupeleka kikosi kazi chake kutathmini tena gharama hizo na
kuzilinganisha na hizo za awali kwa nia ya kushirikiana na vyombo vya fedha na
Kampuni ya Oltremare ya Italy kufufua viwanda hivi. Aidha, Kampuni ya Oltremare
ya Italy imekubali kutoa mafunzo kwa wazawa kuhusu utawala na uendeshaji wa
viwanda hivyo pindi vitakapofufuliwa; na kuisaidia Tanzania kupata Soko la
Korosho zitakazobanguliwa. Naamini kabisa ufufuaji wa viwanda hivi utasaidia
kuboresha teknolojia, kuongeza ufanisi, ajira na mapato ya Serikali na bei ya
korosho ghafi kwa mkulima badala ya kutegemea bei ya Soko la Dunia pekee.
Zao
la Pamba
Mheshimiwa
Spika,
40.
Zao la Pamba lina mchango mkubwa katika
kukuza Uchumi wa Nchi yetu na kuondoa umaskini kwa zaidi ya Wakulima 400,000 na wategemezi wao katika Mikoa
takriban 15 hapa Nchini. Hata hivyo,
bado Kilimo chake kinakabiliwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto hizo
ni pamoja na tija ndogo, matumizi kidogo ya teknolojia za kisasa na zana duni. Aidha,
kuna huduma duni za ugani na utafiti, kukosa mitaji na soko la uhakika;
migogoro baina ya wakulima na wafanyabiashara, na Uhaba wa Viwanda vya
kuongezea Pamba thamani.
Mheshimiwa
Spika,
41.
Katika msimu wa 2011/2012 Serikali kwa
kushirikiana na Shirika la Gatsby Charitable Foundation ya Uingereza chini ya
Ufadhili wa Lord David Sainsbury ilianza majaribio ya Mfumo wa Kilimo cha Pamba
cha Mkataba kupitia Program ya Kuendeleza zao la Pamba katika Mkoa wa Mara na
Wilaya za Bariadi na Kibondo kwa madhumuni ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto
nilizoeleza punde. Matokeo ya majaribio yalionesha kuwa, uzalishaji uliongezeka
kutoka Kilo 398 kwa ekari hadi Kilo 558 kwa ekari; na ubora wa pamba
uliongezeka hadi kufikia Asilimia 78
kutoka Asilimia 48 za awali.
Mheshimiwa
Spika,
42.
Baada ya Serikali kupitia Wakuu wa Mikoa na
Wilaya kuanza mikakati ya kusimamia kilimo cha Mkataba cha pamba, takwimu za mwezi Mei, 2014 zinaonesha kuwa Wilaya Saba (7) katika Kanda ya
Magharibi zilishiriki katika Kilimo cha Mkataba. Aidha, takriban wakulima 90,000 wamenufaika na mikopo ya
Pembejeo ya Kilimo cha Mkataba msimu huu
kupitia Wachambuzi takriban 15, ikilinganishwa na wakulima 30,000 katika msimu uliopita. Vilevile, takwimu hizo zinaonyesha
wakulima 140,000 ndani ya kilimo cha
mkataba wamelima zaidi ya ekari 400,000;
na kwamba katika msimu huu kati ya Makampuni 42 ya pamba, Makampuni 26,
yameshiriki kwenye kilimo cha mkataba ikilinganishwa na Makampuni 12 yaliyoshiriki msimu uliopita. Kwa
ujumla wakulima wengi wameelezea kunufaika kutokana na Kilimo cha Pamba cha
Mkataba hasa kutokana na kuongezeka kwa kipato.
Mheshimiwa
Spika,
43.
Pamoja na mafanikio hayo, yaliyojitokeza
changamoto kadhaa ikiwepo ya baadhi ya Wakulima kuuza na Makampuni kununua
pamba nje ya mkataba jambo lililokwamisha Mfumo wa kurudisha mikopo ya pembejeo
katika maeneo yaliyolimwa kwa mfumo wa Kilimo cha Mkataba. Hivyo, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia
utekelezaji wa Kilimo cha Mkataba kwenye zao la pamba katika maeneo yote
yanayolimwa pamba. Lengo ni kushirikisha Wadau wengine, kuainisha na kupata
ufumbuzi wa kasoro zilizojitokeza katika misimu iliyopita; kupanga mikakati ya
utekelezaji; kuweka utaratibu mzuri wa kulinda uwekezaji wa wachambuaji na pia
kulinda haki za wakulima kwa kuzingatia mikataba inayowekwa kati ya wakulima na
wachambuaji. Nitumie fursa hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutekeleza
agizo la Mheshimiwa Rais kwa Viongozi kusimamia kikamilifu kazi hiyo ili Wakulima
wanufaike na Mfumo huu wa Kilimo cha Mkataba. Njia nyepesi ya kutoa elimu juu
ya Kilimo cha Mkataba ni kutumia Mashamba Darasa na Mashamba ya Mfano.
Nawaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri
wasimamie vema na kwa karibu utaratibu huu.
Mheshimiwa Spika,
44.
Kutokana na tatizo lililojitokeza
la baadhi ya wakulima wa pamba kuuziwa Tani
1,088
za mbegu ya pamba kipara ambayo haikuota kutoka Kampuni ya Quton, kwa
niaba ya Serikali napenda kuwapa pole Wakulima hao. Kama Serikali ilivyoahidi
hapo awali, tumesitisha malipo ya Shilingi Bilioni
1.7 za ruzuku kwa Kampuni ya Quton. Aidha, Serikali inaitaka Kampuni ya
Quton kutorudia makosa haya katika siku zijazo. Maafisa Ugani wasimamie kwa
karibu upandaji wa mbegu hizi wakati wa msimu kwa kutoa elimu stahiki.
Mheshimiwa
Spika,
45.
Katika
kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili la mbegu hafifu, Serikali kupitia
Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
inaendelea na juhudi za kukaribisha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha
mbegu bora kipara kutoka ndani na nje ya Nchi ili kuweka mazingira ya ushindani
ambao utaleta ubora zaidi. Aidha, Taasisi zinazohudumia zao la pamba ziangalie
kama kuna uwezekano wa kupata mbegu za pamba hata kutoka nje ya Nchi kwa
kuzingatia masuala ya ubora na unafuu wa bei. Nichukue fursa hii kuwakumbusha
Bodi ya Pamba na wagani wa zao la pamba kuhakikisha kuwa ubora wa mbegu (germination
percentage) unafanyiwa tathmini kabla mbegu hazijagawiwa kwa wakulima.
Aidha, Wakulima waelimishwe manufaa ya kutumia Mbegu Kipara kwamba wakati wa kuziandaa
zinawekewa viuatilifu ambavyo vinaua vimelea na wadudu ambao wanatokana na
mavuno ya msimu uliopita, hivyo kupunguza uwezekano wa pamba inayotokana na
mbegu hizi kupata magonjwa na wadudu mapema ikilinganishwa na mbegu za manyoya.
46.
Mbegu Kipara zinaweza pia kutumika na mashine
za kupandia (planter) hivyo kuwezesha
mimea ya pamba kuota katika mstari na kwa nafasi stahili na kumwezesha mkulima
kupata mimea mingi kwa ekari (plant
population) kama inavyoshauriwa kitaalamu miche 22,222, hivyo kuongeza tija
kwa ekari tofauti na mbegu za manyoya. Naamini kupitia ushirika na Kilimo cha
Mkataba Wakulima wataweza kuungana kupata planter
ili kupunguza sulubu ya jembe la mkono wakati wa kupanda. Ninaiagiza Bodi ya Pamba
iendelee kusimamia zoezi la wakulima waliochaguliwa kuzalisha mbegu bora kwa
Kampuni ya Quton ili kuwezesha ongezeko la upatikanaji wa mbegu bora kwa
Wakulima.
Mheshimiwa
Spika,
47.
Pamoja na changamoto zinazoikumba tasnia ya pamba
na hasa Kilimo cha mkataba cha pamba, nichukue fursa hii kuwasihi wakulima wa
pamba ambao hawajajiunga na mfumo huu kufanya hivyo kutokana
na mafanikio yaliyopatikana kwa wale waliojiunga tayari. Napenda kuwakumbusha Wagani wa
Pamba kusimamia ipasavyo suala la usafi wa pamba inayouzwa na wakulima ili
wakulima wapate bei nzuri. Aidha, kutokana na kilimo cha mkataba katika zao la
tumbaku na mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani kwa zao la korosho kuwanufaisha
sana wakulima wa mazao hayo, niwatake viongozi wote wanaohusika na uimarishaji
wa zao la pamba kuimarisha kilimo cha pamba na suala la kilimo cha pamba cha
mkataba ili kuweka utaratibu utakaomfanya mkulima kuuza pamba kwa yule
aliyemwezesha kupata pembejeo na kwa kutumia mfumo wa Ushirika.
Mheshimiwa
Spika,
48.
Kupitia Mkutano Mkuu wa Wadau wa Sekta ya Pamba
wa tarehe 4 Julai 2013 Jijini Mwanza, wajumbe waliiomba Serikali kusimamia
uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya zao la pamba na utengenezaji wa
bidhaa za pamba hapa Nchini. Nakubaliana na azimio hilo kwa sababu hatuwezi
kama nilivyoeleza kwa zao la Korosho, kuendelea kusafirisha sehemu kubwa ya
pamba inayozalishwa hapa nchini kama malighafi kwa vile hakutainufaisha nchi na
hata wakulima. Hivyo, narudia tena wito wangu kuitaka Wizara ya Viwanda,
Biashara na Masoko kuhimiza uwekezaji katika viwanda vingi vya kusindika na
kutengeneza bidhaa za pamba hapa Nchini badala ya kuuza pamba ghafi. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu na Wananchi kuwa, katika kujiandaa na Raslimali
Watu kwa ajili ya Viwanda vya Nguo hapa Nchini, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam
kimewezeshwa kuanzisha Kozi za Shahada mbili za Uhandisi wa Viwanda vya Nguo na
Ubunifu, na Vyuo vya VETA vinatoa mafunzo hayo kwa Kada za Chini.
Mheshimiwa
Spika,
49.
Kwa kuwa msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka
2014/2015 umeshazinduliwa tangu tarehe 18 Juni, 2014, ninawasihi Wakuu wa Mikoa
yote inayolima pamba kusimamia kwa karibu mambo yafuatavyo:
Kwanza: Kuhakikisha kuwa bei ya chini ya kununua
Pamba inakuwa Shilingi 750 kwa kilo;
Pili: Kuhakikisha kuwa maeneo yote
ambayo Bodi ya Pamba itathibitisha kwamba hakuna mnunuzi aliyetoa huduma au
mkopo kwa Mkulima, yawe huru kwa mnunuzi yeyote kupewa Leseni ya kununua Pamba
ili kuwapa fursa Wakulima ambao hawapo katika mfumo wa kilimo cha mkataba kuuza
bila matatizo.
50.
Ni matumaini yangu kwamba, hatua hizi
zitasaidia kwa kiasi kikubwa uboreshaji wa zao la Pamba.
UMUHIMU WA
VIWANDA NA KULINDA VIWANDA NCHINI
Mheshimiwa
Spika,
51.
Maendelea ya Nchi yoyote ile yanategemea sana
ujenzi wa viwanda. Kwa maana hiyo, suala
la ujenzi wa viwanda haliepukiki kutokana na sababu kwamba, Viwanda husaidia
kuongeza thamani mazao ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na mazao ghafi yanayozalishwa
katika Sekta zingine. Aidha, Viwanda huongeza muda wa bidhaa hizo wa kutumika
kabla ya kuharibika. Vilevile, mazao yaliyoongezwa thamani humpatia mkulima bei
nzuri na kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa mazao. Uwepo wa viwanda pia unatusaidia
kupata fedha za kigeni, kutoa ajira na hivyo kupunguza tatizo la ajira kwa watu
wetu hasa Vijana. Kwa maana hiyo kuna
haja ya kuwepo Sera na Sheria mahsusi zitakazohimiza na kuchagiza uwekezaji katika Sekta ya Viwanda na pia
kuondoa vikwazo vya kibiashara.
Mheshimiwa
Spika,
52.
Kwa kutambua umuhimu wa viwanda Nchini, ndio
maana Serikali imeanzisha Mpango wa uanzishaji wa Maeneo Maalum ya Uzalishaji
kwa Mauzo Nje Export Processing Zones
- (EPZ) na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Special
Economic Zones - (SEZ) kama mkakati mahususi wa kuvutia Wawekezaji. Katika kipindi cha
mwaka 2012 na 2013 jumla ya miradi ya viwanda ipatayo 52 yenye thamani ya Dola
za Kimarekani Milioni 474.37 ilisajiliwa
na Mamlaka ya EPZ ambapo ajira 12,347 za moja kwa moja zinatarajiwa kupatikana.
Aidha, katika kipindi cha Januari hadi Mei 2014, pekee jumla ya miradi 21 yenye
thamani ya Dola la Kimarekani Milioni 121.4 inayotarajia kutoa ajira za moja
kwa moja zipatazo 4,814 imesajiliwa. Katika miradi hiyo, ipo Miradi inayosajiliwa
kwa utaratibu wa kushirikisha Sekta ya Umma na Binafsi (Private Public Partnership-PPP). Ujenzi wa miradi hiyo iko katika
hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa
Spika,
53.
Ni kweli kwamba, Serikali imeweka juhudi
kubwa katika ujenzi wa Viwanda katika sehemu mbalimbali Nchini na pia kupanua
wigo wa bidhaa zinazozalishwa. Kwa mfano, hivi sasa kuna Viwanda vya Chuma
takriban 17 vinavyojumuisha Viwanda
vya mabati, misumari, nyaya za uzio, nyaya za umeme, bidhaa za chuma, ikiwemo
nondo na mabomba ya chuma kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Lakini pia tunavyo Viwanda vya kuzalisha Saruji vipatavyo vitano
(5) vya Dar es Salaam, (TPCC), Tanga (TCC), Mbeya (MCC), Pwani (Rhino Cement Mkuranga), na Lindi (Lee
Building Material ya Kilwa Masoko). Vilevile,
Viwanda Vipya vya Saruji vinajengwa Arusha, Dar-es-Salaam (3), Tanga (2), Lindi,
Pwani na Mtwara. Upanuzi huu wa Viwanda vya Saruji vitaifanya Tanzania kuwa
miongoni mwa Nchi Wazalishaji Wakuu Barani Afrika na hivyo kujitosheleza
Kitaifa na kuuza nje.
54.
Tunavyo pia Viwanda vikubwa vya Kusindika Ngozi
Saba (7) katika Mikoa ya Arusha, Dar-es-Salaam, Kilimanjaro (2), Morogoro,
Pwani na Shinyanga. Tunavyo Viwanda vya Nguo Tisa (9) katika Mikoa ya Arusha,
Dar-es-Salaam (4), Mara, Morogoro, Mwanza na Tanga na tunavyo pia Viwanda vya
Sukari katika Mikoa ya Kilimanjaro, Kagera na Morogoro ambavyo vyote kwa ujumla
wao vina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa
Spika,
55.
Pamoja na jitihada kubwa iliyowekezwa katika
ujenzi wa Viwanda hivyo Nchini, tunayo Changamoto kubwa ya namna ya kuvilinda
Viwanda hivi dhidi ya ushindani usio halali (Unfair Competition) ili viweze kukua na kuimarika kiushindani,
Kikanda na Kimataifa. Mathalani, zipo bidhaa au vifaa vinavyoingizwa Nchini na
kuuzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na bei ya bidhaa aina hiyo hiyo zinazozalishwa
Nchini. Bidhaa hizo huuzwa kwa bei ya chini kutokana na wazalishaji wa Nchi
zinakotoka bidhaa husika kupewa ruzuku au bidhaa hizo zinakuwa na ubora duni
usiokidhi Viwango vya Ubora au kutozwa ushuru mdogo au kupewa msamaha wa ushuru.
Hali hii husababisha ushindani usio wa
haki katika Soko la Ndani na ni changamoto kubwa kwa Taifa letu na Afrika
Mashariki kwa ujumla. Naomba uniruhusu nitoe mifano michache ambayo
itatuwezesha kuona ni namna gani tunaweza kukabili changamoto hii kwa lengo la
kulinda Viwanda vyetu Nchini.
Mheshimiwa
Spika,
56.
Nikianza na Saruji. Kama nilivyosema tunavyo
Viwanda vitano vya Saruji vyenye
uwezo wa kuzalisha Saruji hadi Tani Milioni 3.8 kwa mwaka. Mahitaji ya Saruji
kwa sasa ni Tani Milioni 3.9 kwa mwaka na zipo juhudi za kuongeza uzalishaji
kupitia uwekezaji katika miradi tisa (9) mipya ya ujenzi wa Viwanda vya Saruji
ambavyo kwa ujumla wake inatarajiwa vitazalisha Tani Milioni 8.3 kwa mwaka.
Mheshimiwa
Spika,
57.
Pamoja
na uzalishaji huo mkubwa, changamoto kubwa ni namna ya kuhimili gharama kubwa
za uzalishaji wa Saruji ikiwemo umeme, gharama za usafirishaji, na ushindani
mkubwa dhidi ya saruji kutoka nje ya nchi ambayo ina ruzuku, hivyo kuvuruga
soko la ndani kwa Viwanda vya Saruji. Aidha, ziko taarifa za ukwepaji kodi na
udanganyifu ambao umeendelea kuwa tatizo kubwa sana katika Sekta ya Saruji. Kwa
kutambua changamoto hiyo, Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilikubaliana
kuweka Ushuru wa Forodha wa Asilimia 55
mwaka 2005 na kuushusha kufikia Asilimia 35 mwaka 2010. Matarajio yalikuwa
ni kuvilinda Viwanda hivi ili vijijenge kwa miaka mitano na baada ya hapo
kuendelea kuvilinda kwa kuviweka chini ya kundi la bidhaa nyeti, yaani kuwa na
wigo wa pamoja wa Ushuru wa Forodha wa zaidi ya Asilimia 25.
Mheshimiwa
Spika,
58.
Hali iliyojitokeza katika Viwanda vya Saruji
haitofautiani sana na Viwanda vya Chuma ambavyo navyo vina changamoto kubwa
hasa katika uzalishaji na ubora wa bidhaa za chuma. Mathalan, ziko taarifa
ambazo hazijathibitishwa kwamba karibu Viwanda vyote vya Nondo Nchini
vinazalisha chini ya viwango, jambo ambalo halikubaliki
kabisa. Nilibahatika kufanya Ziara Mkoa wa Mwanza ambapo nilikuta katika Mradi mmoja wa ujenzi wa Tanki la
Maji – Mkandarasi alikuwa ananunua Nondo kutoka Uganda kwa madai kuwa Nondo
zilizokuwa zinazalishwa na Viwanda vyetu kwa maelezo yake zilikuwa chini ya
viwango. Kiwango stahiki kinapaswa kuwa BS 406, BS 500, n.k. lakini Viwanda vyetu
vinazalisha chini ya kiwango hicho, yaani BS 400. Ni wakati muafaka sasa
Viwanda vyote kuzingatia viwango vya Kimataifa ili kuepusha majanga
yanayotokana na udhaifu huo na pia kuwezesha Nondo hizo kutumiwa na wahitaji
wote wa hapa ndani na nje ya Nchi. Ninahimiza Shirika la Viwango Nchini
liendelee kusimamia ubora wa bidhaa za Nondo kwa maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa
Spika,
59.
Kwa sasa kuna Viwanda vya Nondo takriban 15
ambavyo vina uwezo wa kuzalisha Nondo Tani 420,000 kwa mwaka. Mahitaji ya Nondo
ni Tani 200,000 kwa mwaka, ikiwa ni ziada ya Asilimia 40 zaidi ya mahitaji.
Aidha, Viwanda hivi vya Nondo peke yake vinatoa ajira ya moja kwa moja ya watu
4,000 na wengine takriban 40,000 ambao siyo wa moja kwa moja.
60.
Lakini pia tuna Viwanda vikubwa vya Chuma viwili
(2) vyenye uwezo wa kuzalisha Mabati Tani 150,000 kwa mwaka, wakati mahitaji ni
Tani 100,000 kwa mwaka ikiwa ni ziada ya Tani 50,000, sawa na Asilimia 50 ya mahitaji. Viwanda hivi navyo
vimezalisha ajira ya takriban Watu 16,000.
Mheshimiwa
Spika,
61.
Mifano hiyo miwili ya Uzalishaji wa Nondo na
Mabati inadhihirisha kwamba tatizo la uzalishaji kukidhi mahitaji halipo, bali
tatizo ni uagizaji wa Nondo zinazoingizwa Nchini kwa kulipiwa Ushuru mdogo,
naambiwa wa Asilimia 10 tu kama Kodi kwa visingizio mbalimbali na hivyo kutoa
ushindani usio halali kwa Nondo zinazozalishwa Nchini. Aidha, mabati
yanayoingizwa Nchini yamewekwa katika orodha ya “Deemed Capital Goods”
ambayo haiwabani watekelezaji wa Miradi mbalimbali nchini kutumia mabati
yanayotengenezwa na Viwanda vya Ndani.
Mheshimiwa
Spika,
62.
Tunavyo Viwanda vya kusindika Ngozi takriban
tisa (9). Viwanda hivi vina uwezo wa kusindika vipande vya Ngozi Milioni 13.2
kwa mwaka katika hatua ya mwanzo yaani (Wet
Blue). Kati ya hivyo vipande vya ngozi za ng’ombe ni milioni 2.5 na vya
mbuzi na kondoo ni Milioni 10.7. Aidha, usindikaji wa ngozi ghafi umefikia
Vipande 945,596 vya Ng’ombe na Vipande 2,713,636 vya Mbuzi na Kondoo kwa mwaka
2013. Kama ilivyo kwa Viwanda vya Chuma na Saruji, changamoto kubwa ya usindikaji wa ngozi ni pamoja na ushindani usio wa haki unaosababishwa na
uingizaji wa viatu vya plastiki na mitumba ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa
uzalishaji wa viatu vya Ngozi na bidhaa nyingine za Ngozi Nchini.
Mheshimiwa Spika,
63.
Vilevile, tunalo tatizo kubwa katika Viwanda
vya uzalishaji wa Sukari Nchini. Tunavyo Viwanda
takriban Vinne vya Sukari. Uwezo wa uzalishaji Sukari Nchini ni Tani 300,000 kwa mwaka. Mahitaji ya Sukari
ni Tani 590,000 kwa mwaka (Tani 420,000 ni Sukari ya Matumizi ya
Kawaida na Tani 170,000 Sukari ya
Matumizi ya Viwandani). Kwa maana hiyo, kuna upungufu wa Tani 290,000 sawa na Asilimia
49. Kati ya hizo Tani 170,000 (29%)
ya Sukari ya matumizi ya Viwandani na Tani 120,0000 (20%) Sukari ya Matumizi ya
Kawaida. Kutokana na upungufu huo, Serikali iliweka utaratibu wa kuagiza na
kusambaza Sukari kutoka Nje ya Nchi ili kufidia pengo hilo kwa kuruhusu
Waagizaji kulipa Ushuru wa Asilimia 25 na pia Ushuru wa Forodha Asilimia 10 kwa
Viwanda vinavyotumia Sukari kwa ajili ya matumizi ya Viwandani. Vipo pia vibali
vya bila ushuru kabisa vinavyotolewa wakati wa upungufu wa sukari.
Mheshimiwa
Spika,
64.
Utaratibu
huu pamoja na kusimamiwa na Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), umesababisha
malalamiko mengi kuwa hatua hizi za kushusha Viwango vya Ushuru wa Forodha
zimesababisha waingizaji Sukari kukwepa kabisa Kodi, ikiwemo Ushuru wa Forodha
na VAT. Aidha, zipo hisia kuwa sukari hiyo ambayo ni nyingi zaidi ya kiasi
kilichoruhusiwa kuingizwa Nchini inatokana na Wafanyabiashara wasiokuwa
waaminifu kutumia kinyume cha Sheria vibali vya Mamlaka ya Mapato Tanzania
vinavyowaruhusu kupitishia Nchini Sukari inayosafirishwa kwenda nje ya Nchi (Transit Sugar) kwa kuibakiza bidhaa hiyo
hapa Nchini na sukari ya viwandani kuuzwa kama sukari ya mezani.
Mheshimiwa
Spika,
65.
Sukari hii inayoingizwa nchini huathiri
uzalishaji na mtiririko wa usambazaji sukari ya ndani hivyo kutishia ukuaji wa
viwanda vya ndani vya Sukari na uzalishaji wa sukari kwa ujumla. Vilevile, itakumbukwa
kuwa Serikali kwa nia njema, tulianzisha utaratibu wa “Outgrowers” ili Wakulima wanaoishi kandokando ya Viwanda vya
Sukari kulima Miwa na kuuzia wenye Viwanda kule Kilombero, Mtibwa na Kagera ili
kuboresha maisha yao kiuchumi. Hivyo, kutokana na hali ilivyo kwa sasa,
Wakulima hawa wakiwemo Wakulima wa Kilombero wameshindwa kulipwa kwa wakati
baada ya kuuza Miwa yao Kiwandani kwa vile Wazalishaji wamekuwa wakiuza Sukari
chini ya Wastani wa mauzo ya kawaida.
Mheshimiwa Spika,
66.
Nimeamua kuongea haya
yote kuhusu hali halisi ya Viwanda vyetu na bidhaa zinazozalishwa humu Nchini
ili kuona umuhimu wa kujenga Viwanda na changamoto tulizonazo katika kulinda
Viwanda vyetu vya ndani kwa kutumia mifano ya bidhaa za Chuma ikiwemo Mabati,
Nondo, Saruji na Sukari. Yapo mambo mengi ambayo yanajitokeza katika kila moja.
Lakini jambo la msingi ni
namna ya kuangalia
kama tunapokuwa na mahitaji yanayozidi uwezo wa uzalishaji Viwandani
tuchukue hatua gani. Ni lazima kama Nchi pamoja na upungufu
wa bidhaa uliopo, sasa tuamue kulinda
Viwanda vyetu vya ndani dhidi ya Ushindani usio halali kwa nguvu zetu zote.
Lazima sasa tukae tuone namna ya kudhibiti uingizaji wa bidhaa ambazo
zinakwamisha maendeleo ya Viwanda vyetu. Aidha, tuangalie njia bora ya
kupunguza gharama za uzalishaji, ikiwemo bei kubwa za umeme. Matarajio ni kwamba,
baada ya kupatikana kwa Gesi tunaamini gharama za Umeme zitapungua na kupunguza
gharama za uzalishaji Viwandani.
Mheshimiwa Spika,
67.
Tumeona changamoto
zinazokabili bidhaa za Mabati, Nondo, Sukari, Ngozi na Saruji kama mfano. Ninaagiza
Taasisi zetu zikiwemo Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Maendeleo
ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA), Bodi ya Sukari, Jeshi la Polisi na Uhamiaji kukaa kwa
pamoja kuangalia njia bora ya kudhibiti
uingizaji kiholela wa bidhaa zinazokwamisha maendeleo ya Viwanda vyetu. Kwa
maana hiyo ni vizuri sasa kuchukua hatua stahiki kulinda Viwanda vyetu kuhimiza
mambo muhimu yafuatayo:
i)
Wizara ya Viwanda na
Biashara ni lazima sasa kuhakikisha kwamba Viwanda vyetu vinazalisha bidhaa
zenye ubora kwa Viwango vya Kimataifa. Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
lisaidie, lakini lazima ubora uwe unalingana na Viwango vya Kimataifa;
ii)
Wizara ya Fedha
ihakikishe kuwa bidhaa zilizomo katika kundi la bidhaa nyeti katika Afrika
Mashariki haziondolewi katika kundi hilo katika kipindi kirefu kijacho hadi
hapo suala la Ruzuku likipatiwa ufumbuzi wenye manufaa kwa Nchi changa katika Shirika
la Biashara Duniani (WTO);
iii)
Wizara ya Fedha iangalie
uwezekano wa watumiaji wa Industrial
Sugar wanalipia Ushuru kamili na kisha baadaye wapewe Duty Drawback baada ya kuthibitishwa kuwa Sukari husika kweli
ilitumika katika uzalishaji. Wizara ya Fedha pia iweke utaratibu ulio bora wa uagizaji
wa Sukari kufidia upungufu huu kutumia Bulk
Importation, na kisha kusambazwa kwa usimamizi madhubuti na kwa bei maalum,
n.k.;
iv)
Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika na Bodi ya Sukari wakae na kutathmini mahitaji halisi ya
Sukari, ikilinganishwa na uwezo wa Viwanda vya Sukari vilivyopo Nchini, pamoja
na kukamilisha taratibu za kisheria na kimfumo za uagizaji wa Sukari kuziba
upungufu pale inapobidi. Aidha, ni muhimu kuhimiza upanuzi katika uzalishaji wa
Sukari kwa kuhamasisha Uwekezaji mpya katika Sekta hii;
v)
Utaratibu wa kuagiza bidhaa
zitakazoingizwa Nchini kuziba pengo lililopo lazima uangaliwe upya ili uagizaji
huo usiathiri Viwanda vya ndani;
vi)
Tathmini ya upungufu wa
bidhaa unaojitokeza uangaliwe kwa umakini na kupanga njia bora ya kufidia
upungufu huo, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa vibali vya kuruhusu
kuingiza bidhaa Nchini. Vibali vihusishe muda ule wenye upungufu pekee. Aidha, utaratibu
wa sasa wa kutumia Wafanyabiashara kuleta bidhaa kwa lengo la kufidia upungufu wa
bidhaa husika uangaliwe upya ili kuepuka uingizaji bidhaa kwa wingi kuliko
upungufu ambako kunasababisha kudumaza Viwanda vya ndani; na
vii)
Bei za bidhaa zizingatie
maeneo yanayozunguka eneo la Uzalishaji. Kwa mfano, haitarajiwi bei ya Sukari
kilo moja inayozalishwa na Kiwanda cha Sukari cha Kagera iwe kubwa sawa na
Sukari hiyo ya Kagera inavyouzwa Mtwara au Ruvuma.
Mheshimiwa Spika,
68.
Ipo mifano kwa baadhi ya
Nchi Duniani ikiwemo India ambazo zimejaribu kuweka Nembo inayoonesha kwamba
bidhaa hizi zinazalishwa Nchini na bei yake ni kiasi fulani. Lengo likiwa ni
kuhakikisha kulinda watumiaji wa bidhaa hizo na kulinda pia Viwanda. Majirani
zetu Kenya wameanza kuchukua hatua katika Bajeti ya 2014 kulinda Viwanda vyao.
Kwa mfano, Serikali ya Kenya imeongeza Ushuru wa bidhaa za Chuma kutoka
Asilimia 0-10 na kufikia Asilimia 25 na kuahidi kuweka mezani Muswada mpya wa
Sheria ya Ushuru wa Forodha ili kulinda Viwanda vyake. Nasi tukidhamiria hata
kama hatukufanikiwa kwa kiasi kikubwa mwaka huu, tunaweza kufikia lengo hilo
kwa mwaka ujao wa Bajeti. Nina hakika Tukidhamiria
tutaweza kufika!
UTOAJI WA
ELIMU KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU NCHINI
Mheshimiwa
Spika,
69.
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995
inasisitiza kuhusu haki ya kila raia wa Tanzania kupata Elimu wakiwemo watu Wenye
Mahitaji Maalumu; Sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 1996 inayozungumzia
umuhimu wa kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule kwenda na kupata elimu bora;
na Sera ya Taifa ya Watu wenye Ulemavu ya 2004 – inasisitiza umuhimu wa Elimu
ya watoto wenye Ulemavu kutolewa katika mazingira Jumuishi na rafiki. Katika
kutekeleza Sera hizo, Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa elimu bora kwa watoto
wote wenye umri wa kwenda shule, wakiwemo wenye Mahitaji Maalumu.
Mheshimiwa
Spika,
70.
Kwa
sasa zipo Shule za Msingi 22 ambazo
ni maalum kwa ajili ya Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum na Shule za Msingi 354 zenye Vitengo Maalum kwa ajili ya Wanafunzi hao. Jumla ya Wanafunzi wenye
Mahitaji Maalum katika Shule za Msingi na Vitengo hivyo ni 11,689. Aidha, ipo Shule moja ya Sekondari ambayo ni maalum kwa
Wanafunzi wa Sekondari wenye Mahitaji Maalum pamoja na Shule za Sekondari 61 ambazo zina Vitengo Maalum kwa ajili ya Wanafunzi wa aina hiyo. Kwa sasa, wapo
Wanafunzi 1,406 wenye Mahitaji
Maalum waliopo katika Shule za Sekondari Nchini.
Mheshimiwa
Spika,
71.
Tarehe 3 Mei 2014 nilifungua maonesho ya
Elimu yaliyokuwa yameandaliwa na Wadau mbalimbali wa Elimu kwenye Uwanja wa
Jamhuri hapa Dodoma. Nilipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali yaliyokuwa
yakionesha shughuli mbalimbali za elimu. Moja ya Banda nililotembelea ni lile
lililokuwa likionesha hatua mbalimbali za utoaji wa elimu maalum. Katika Banda
hilo nilielezwa njia zinazotumiwa kuwafundisha Wanafunzi wenye Mahitaji maalum
hususan Wasioona na nilioneshwa vifaa vinavyotumika na kuelezwa changamoto
zilizopo.
Mheshimiwa
Spika,
72.
Tarehe 4 Juni 2014 nilitembelea na kukagua
Shule ya Msingi Bwigiri – Wasioona, Wilayani Chamwino. Katika ziara hiyo
nilikagua maktaba, chumba cha kompyuta, chumba cha kutayarishia mitihani na vyoo.
Niliongea pia na Wanafunzi waliokuwa wamebaki hapo shuleni baada ya wanafunzi
walio wengi kuwepo kwenye likizo. Shule hiyo ni miongoni kwa Shule 120 za
Msingi zilizoko kwenye Wilaya ya Chamwino ikiwa na jumla ya Watumishi 39 kati
yao 25 wakiwa ni Walimu. Shule ina Wanafunzi 87, kati yao 61 ni Wasioona na 26
Wanaona. Jambo lililonifurahisha katika Shule hiyo ni kuwa Wanafunzi
wanaohitimu Darasa la Saba wamekuwa wakifaulu wote (Asilimia 100) kwa muda wa
miaka 13 mfululizo. Wanafunzi hao wanaofaulu wamekuwa wakijiunga na Shule
Maalum za Sekondari kama vile Shule ya Sekondari Diocese of Central Tanganyika (DCT)
Mvumi n.k.
Mheshimiwa
Spika,
73.
Tarehe 7 Juni 2014 nilitembelea pia Shule ya
Sekondari ya Mvumi DCT ambako baadhi ya Wanafunzi Wasioona wanasoma. Nilikutana
na Walimu pamoja na Wanafunzi wa Kidato cha Pili na Nne ambao walikuwa
wanajiandaa na mitihani ya Kitaifa ya mwaka 2014. Nilifurahishwa na kazi kubwa
inayofanywa na Serikali, Kanisa la Anglikana Nchini na Walimu wa Shule hiyo kwa
kuwawezesha Wanafunzi Wasiiona kupata haki yao ya elimu.
74.
Ziara zangu hizo zilinithibitishia kuwa
Walimu Nchini wakiwemo Walimu wa Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum wanafanya kazi
kubwa na ya Kizalendo ambayo inahitaji kuungwa mkono wakati wote. Nawapongeza
Walimu wote Nchini kwa kazi yao muhimu ya kutoa elimu kwa Taifa letu. Nitumie
fursa hii ya kipekee kabisa kuwapongeza Walimu na Wanafunzi wote wa Shule ya
Msingi Bwigiri – Wasioona kwa kuwezesha mafanikio makubwa na ya kuigwa
yaliyopatikana Shuleni hapo. Aidha, nawapongeza Wasimamizi wa Elimu wa Mkoa wa
Dodoma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa
usimamizi wao mzuri uliowezesha ufaulu na mafanikio hayo kwa ujumla.
Mheshimiwa
Spika,
75.
Pamoja na pongezi hizo, Ziara zangu hizo
ziliniwezesha kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo Wanafunzi Wasioona
wakiwa shuleni. Ni kweli changamoto ni nyingi, lakini kubwa nililoliona na
ambalo limewagusa Wanafunzi hao pekee ni lile la Wanafunzi Wasioona
kutofundishwa somo la Hisabati katika ngazi ya Sekondari na hivyo, kutofanya
mtihani wa somo hilo wa kumaliza Kidato cha Nne na kusababisha kushushwa
madaraja yao ya ufaulu sawa na Wanafunzi wa kawaida katika Shule zingine Nchini
wasiofaulu somo hilo. Lakini Shule hizi zinakosa vitendea kazi muhimu kama vile
Braille Printer, Embossing Photocopy Machine, Kompyuta, n.k.
Mheshimiwa
Spika,
76.
Ninafahamu kuwa changamoto nyingine si za
Wanafunzi wasioona tu bali zinawahusu pia Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum
pamoja na Walimu wao kwa ujumla. Napenda kutoa wito kwa Watendaji wanaohusika
na elimu maalum Nchini kushughulikia changamoto zonazowakabili Walimu na
Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum pamoja na Majengo ya Shule zao. Ni imani yangu
kuwa kila mmoja anayehusika atachukua hatua mapema ili kuwawezesha Wanafunzi
Wasioona na wote Wenye Mahitaji Maalum kupata elimu stahiki katika mazingira
stahiki.
AFYA
Uwiano wa Idadi ya Watu wa Vijijini na Mijini wanaohudumiwa na Daktari
Mheshimiwa Spika,
77.
Idadi ya Watanzania
inakadiriwa kuwa Milioni 48.2 kati
yao wanaoishi Vijijini ni Milioni 36.6
na wanaoishi Mijini ni Milioni 11.6. Watanzania hao wanahudumiwa na Madaktari ni 2,311 waliopo Nchini kwa sasa. Madaktari wanaoishi maeneo ya
Vijijini ni 523 na wanaoishi maeneo ya Mijini ni 1,788. Mgawanyo huu wa Madaktari unafanya kuwa Daktari mmoja
kitaifa anahudumia Wastani wa Watanzania
19,982. Kwa upande wa Vijijini,
Daktari mmoja anahudumia Wananchi 66,211
wanaoishi Vijijini na kwa maeneo ya Mijini, Daktari mmoja anahudumia Wananchi 6,460. Hali hii inaonesha kuwa Daktari
mmoja anayehudumia maeneo ya Vijijini anahudumia zaidi ya mara kumi ya idadi ya
watu wanaohudumiwa na Daktari anayefanya kazi Mjini.
78.
Kiwango hiki cha Daktari
mmoja kwa Watanzania 19,982 ni kikubwa sana ikilinganishwa na wastani wa
kawaida wa Daktari mmoja kwa Watu 10,000.
Kinahitaji kupunguzwa kwa kuongeza idadi ya Madaktari Nchini. Serikali
itaendelea kugharamia elimu ya Madaktari Nchini na kuwawezesha kuwa na
mazingira bora ya kazi kwa kuzingatia hali ya uchumi wa Nchi. Nia ni kuongeza
idadi ya Madaktari wa ngazi na vitengo mbalimbali vya Afya na kuwasambaza
Nchini hususan maeneo ya Vijijini ili Daktari mmoja ahudumie Watanzania
wachache zaidi.
Saratani
ya Shingo ya Kizazi
Mheshimiwa
Spika,
79.
Serikali imeanzisha mpango wa kitaifa wa
kukinga na kuzuia saratani ya shingo ya kizazi. Aidha, Serikali itaendelea
kutoa elimu kuhusu kujikinga na saratani ya awali, kupanua vituo vya kupima
dalili za awali za saratani na kupatiwa tiba ya ugandishaji baridi kwenye Mikoa
mitatu iliyobakia ya Mtwara, Rukwa na Simiyu. Huduma ya rufaa itaboreshwa kwa
wagonjwa wanaofikiriwa kuwa na saratani kwa ajili ya tiba katika Taasisi ya
Saratani ya Dar-es-Salaam. Aidha, chanjo ya kuwakinga Wasichana wenye umri wa
miaka 9-13 dhidi ya saratani imeanza kutolewa katika Mkoa wa Kilimanjaro ili
kujifunza mfumo wa kutumia Shule kwa ajili ya kutoa chanjo hii nchi nzima.
HALI
YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa
Spika,
80.
Kwa ujumla hali ya usalama katika Mipaka yote
ya Nchi yetu inaendelea kuwa shwari licha ya kuwepo changamoto kadhaa. Mathalani katika Mpaka wa Kaskazini ambapo
Tanzania inapakana na Kenya na Uganda kumekuwepo na changamoto ya Wahamiaji
haramu hususan katika Wilaya za Misenyi na Karagwe na changamoto ya uharibifu
wa alama za Mipaka. Aidha, katika Mpaka wa Kusini pamekuwepo na changamoto ya
utata wa Mpaka kati ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa na changamoto ya
ujenzi holela unaofanywa na Wananchi waishio Mpakani eneo la Tunduma.
Mheshimiwa
Spika,
81.
Serikali kupitia Vyombo vyake vya Ulinzi na
Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inaendelea
kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti hali hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya
mazungumzo ya pamoja baina ya Wataalamu wetu na Wataalamu wa Nchi hizo jirani
kwa mfano:
i)
Tarehe 05 hadi 12 Octoba, 2013 Mjini Arusha
vilifanyika Vikao vya pamoja kukagua, na kuhakiki Mpaka kati ya Tanzania na
Kenya;
ii)
Mwezi
Februari 2014 Jijini Dar es Salaam kilifanyika kikao cha kuboresha Mipaka ya
Tanzania, Burundi, Zambia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika ziwa
Tanganyika;
iii)
Mwezi Mei, 2014 kilifanyika Kikao cha TUME ya
Uimarishaji na Uhakiki wa Mpaka baina ya Tanzania na Burundi Mjini Ngara.
Mheshimiwa
Spika,
82.
Pamoja na kwamba kwa ujumla hali ya usalama
wa Mipaka yetu ni shwari, bado Nchi yetu kama sehemu ya Afrika Mashariki
inakabiliwa na tishio la mashambulizi ya Kigaidi ambalo linawakumba Majirani
zetu. Serikali kupitia Jeshi la Wananchi
Tanzania inaendelea kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Nchi
jirani, Nchi Marafiki pamoja na Jumuia ya Kimataifa ili kukabili tishio hilo.
Nitoe wito tena kwa Wananchi wetu kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Vyombo vya
Usalama katika kuhakikisha Nchi yetu inakuwa salama wakati wote.
AJALI ZA BARABARANI
Mheshimiwa
Spika,
83.
Suala la ajali za barabarani bado ni
changamoto kubwa hapa Nchini likichangia vifo na majeruhi wengi na uharibifu wa
mali. Pamoja na hatua mbalimbali za kisheria, bado kumekuwa na ongezeko la
ajali za barabarani mwaka hadi mwaka. Katika kipindi cha Januari 2011 hadi Mei
2014, jumla ya Ajali 78,654 ambazo
zilisababisha Vifo 13,375 na Majeruhi
67,936 zilitokea. Hii ni idadi kubwa
ya ajali, vifo na majeruhi.
Mheshimiwa
Spika,
84.
Ziko sababu mbalimbali zinazochangia
kuongezeka kwa ajali za barabarani zikiwemo makosa ya kibinadamu (Uzembe wa
Madereva, Ulevi, Mwendokasi na Uegeshaji mbaya wa magari barabarani n.k.)
ambayo kwa ujumla yanachangia Asilimia 77 ya ajali zote zinazotokea, ubovu wa
vyombo vya moto unaochangia Asilimia 16, na mazingira ya barabara yaani ubovu wa miundombinu na hali ya hewa vinavyochangia Asilimia
7.
Mheshimiwa
Spika,
85.
Katika kukabiliana na
ajali za barabarani, Serikali kupitia Vyombo mbalimbali imechukua hatua za
kuimarisha mafunzo kwa Madereva kwa kutunga Kanuni zinazowalazimisha kusoma
masomo ya umahiri wa kuendesha magari ya abiria na magari makubwa ya mizigo
(HDV); kudhibiti mwendokasi na kuanzisha Mfumo wa kufuatilia mwendo wa Mabasi
na Malori utakaodhibiti makosa mbalimbali ya usalama barabarani. Hatua nyingine
ni kuanzisha mfumo wa uwekaji nukta (Point
system) katika Leseni za Madereva ili kuwaondoa barabarani madereva
wanaokithiri kwa makosa, kupima kiasi cha ulevi kwa Madereva; na kupanua wigo
wa elimu ya usalama barabarani kwa njia ya televisheni, redio, simu na
magazeti. Kwa upande wa Usimamizi wa Sheria zilizopo, hatua stahiki
zinachukuliwa kwa kuongeza usimamizi na mafunzo kwa watendaji wote wanaosimamia
Sheria ili kuwaongezea ufanisi na kudhibiti nidhamu yao. Watendaji wanaokiuka
maadili ya kazi wanachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mheshimiwa
Spika,
86.
Kwa upande wa ubovu wa vyombo vya moto,
Serikali inaandaa Kanuni za Ukaguzi wa Lazima. Chuo cha Taifa
cha Usafirishaji (NIT) kimekamilisha ujenzi wa mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa
magari ikiwa ni pamoja na mitambo ya kukabiliana na uchafuzi wa hewa. Ninatoa
wito pia kwa Sekta Binafsi kujitokeza kuwekeza katika eneo hili ili mitambo hii
iwepo ya kutosha. Aidha ni muhimu sasa kuanzisha Gereji maalum kwa ajili ya
matengenezo yatakayokuwa yanapimwa kwa mfumo huu. Sambamba na hatua hizo, Jeshi
la Polisi pia linaandaa Kanuni zitakazowalazimu Madereva kubandika mkanda ang’avu
kuzunguka magari makubwa ya mizigo na mabasi ili kusaidia kuongeza muonekano wa
magari hayo wakati wa giza.
Mheshimiwa
Spika,
87.
Pamoja na jitihada hizo za Serikali za
kuandaa Kanuni mbalimbali, Sheria mpya ya Usalama Barabarani inaweka muundo
bora wa usimamizi wa shughuli za Usalama barabarani kwa kuweka hitaji la
kuundwa kwa Taasisi Kiongozi ya Usalama Barabarani (Road Safety Lead Agency). Sheria hiyo itaanisha majukumu ya Taasisi
Wadau wa Usalama Barabarani na kuratibu utekelezwaji wa majukumu ya Taasisi
hizo. Uwepo wa Chombo hiki utaongeza uwajibikaji wa kila Taasisi katika eneo
lake tofauti na sasa ambapo suala la usalama barabarani linachukuliwa kama
jukumu la Polisi pekee. Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Taasisi na Wadau mbalimbali wanafanya mapitio ya rasimu ya Muswada huu
ambao mara utakapokamilika utawasilishwa Bungeni.
MAUAJI YA WALEMAVU WA NGOZI NA VIKONGWE
Mheshimiwa
Spika,
88.
Nchi yetu bado inaendelea kukumbwa na tatizo
la Mauaji ya Watu wenye Ulemevu wa
Ngozi na Vikongwe kwa imani za ushirikina. Katika kipindi cha mwaka 2012 hadi
2014, takwimu zinaonesha kwamba jumla ya Watu 3 wenye Ulemavu wa Ngozi waliuawa katika Mikoa ya Arusha, Tabora na
Simiyu na wengine 2 walijeruhiwa
katika Mkoa wa Rukwa. Kufuatia matukio hayo, watuhumiwa 8 wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa mauaji na wengine 4
wanashtakiwa kwa kujeruhi. Aidha, katika kipindi hicho jumla ya Vikongwe 1,393 waliuawa kikatili katika Mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu,
Mwanza, Tabora, Singida, Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa.
Mheshimiwa
Spika,
89.
Kwa kutambua ukubwa wa tatizo hili, Serikali
inachukua hatua ya kuzihusisha Kamati za Ulinzi na Usalama za ngazi mbalimbali
kuanzia Vitongoji na Mitaa katika mapambano dhidi ya mauaji ya Vikongwe kwa kufanya Mauaji ya Watu wenye Ulemavu na Vikongwe
kuwa Agenda ya kudumu katika Mikutano yao. Aidha, tutaendelea kutoa elimu
kwa Wananchi kupitia Vyombo vya Habari, Viongozi wa Dini na Watu mashuhuri
katika maeneo husika ya kuepukana na imani potofu za ushirikina. Jeshi la
Polisi linaendesha Program mbalimbali kuelimisha Jamii kukabiliana na uhalifu
kufanya ufuatiliaji wa matukio ya mauaji ya Vikongwe ikiwa ni pamoja na kuweka
mkakati wa kuharakisha upelelezi wa kesi za matukio ya Mauaji.
MAUAJI YA
WANAWAKE MKOANI MARA
Mheshimiwa
Spika,
90.
Pamoja na Mauaji ya Vikongwe na Watu wenye
Ulemavu wa Ngozi katika Mkoa wa Mara kumetokea mauaji ya kinyama ya Wanawake
kutokana na sababu za kishirikina katika kipindi cha Januari hadi Mei 2014 hususan
katika Wilaya za Butiama na Musoma. Waathirika wa matukio
haya walikuwa wakiuawa kwa kunyongwa kwa kutumia khanga nyakati za mchana
wakiwa katika shughuli zao na hivyo kusababisha hofu kubwa katika Jamii. Jumla ya
matukio tisa (9) ya kuuawa Wanawake yaliripotiwa katika Kata
nne za Mugangwa, Etaro, Nyegina na Nyakatende.
Mheshimiwa
Spika,
91.
Kufuatia matukio hayo
Serikali kupitia Jeshi la Polisi na kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa imechukua hatua za haraka na jumla ya watuhumiwa 15 wamekamatwa
na kufikishwa Mahakamani kwa kesi za mauaji. Aidha, Kikosi Kazi cha Makosa
dhidi ya Binadamu na vitendea kazi kutoka Makao Makuu ya Upelelezi kikiongozwa
na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania Kamishna ISAYA MNGULU
walifika Mkoani Mara kwa ajili ya ufuatilia wa karibu wa kitaalamu wa matukio haya.
Timu hiyo wenye Wataalam mahiri katika eneo la Upelelezi wanaendelea kufuatilia
matukio haya sambamba na kutoa elimu juu
ya Ulinzi Shirikishi wa namna ya
kukabiliana na matukio
kama haya,ikiwa ni pamoja na kutoa elimu zaidi kuhusu uhalifu huu na kufanaya
Operesheni ijulikanayo kama “Zuia Mauaji ya akina Mama Wilaya ya Butiama.”
Mheshimiwa
Spika,
92.
Kutokana na juhudi hizo,
hali ya Usalama katika maeneo hayo imeimarika na matukio hayo hayajajitokeza
tena. Napenda kutoa wito kwa Wananchi wote kutambua kuwa jukumu la ulinzi ni
la kila Mwananchi, hivyo hatuna budi kuwafichua wale wote wanaofanya uhalifu
katika Jamii. Lengo ni kuwalinda Wananchi na kuhakikisha kuwa maeneo
tunayoishi yanakuwa na ulinzi na usalama wa kutosha ili Wananchi waendelee na
shughuli zao za uzalishaji badala ya kuhofia maisha yao.
MCHAKATO
WA KATIBA MPYA NA MUSTAKABALI WA TAIFA
Mheshimiwa
Spika,
93.
Kama wote tunavyofahamu, Bunge Maalum la
Katiba liliaanza majukumu yake mapema mwezi Februari 2014 ambapo katika kipindi
hicho Wajumbe walikamilisha kuandika na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum la
Katiba, kufanya uchaguzi wa Viongozi wa Bunge Maalum, Wajumbe kujadili Sura ya
Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba hiyo na Kamati za Bunge Maalum
kuwasilisha maoni yao Bungeni. Hata hivyo, na kwa masikitiko makubwa wakati tukiwa
katika hatua za uwasilishaji, baadhi ya Wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba na
Wananchi (UKAWA) waliamua kutoka nje ya Bunge kwa sababu ambazo wanazijua wao.
Mheshimiwa
Spika,
94.
Wote tunafahamu kuwa, Bunge Maalum la Katiba lina Wajumbe wa
aina tatu wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Waheshimiwa Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi na Wajumbe 201
wanaotoka katika Makundi mbalimbali. Kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge
hili ni sehemu ya Wajumbe wa Bunge Maalum, naomba nitumie fursa hii kupitia
Bunge lako Tukufu kutoa ujumbe mfupi kwa Wajumbe wa Bunge Maalum ambao naamini
utaweza kuwafikia popote walipo.
Mheshimiwa
Spika,
95.
Kifungu cha 26 (1) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba kinatoa masharti na mamlaka ya Bunge Maalum kutunga
Kanuni kwa ajili ya kuendesha
shughuli za Bunge Maalum. Ni kwa kupitia mamlaka kama
ilivyofafanuliwa katika Kifungu hiki, Wabunge wa Bunge Maalum waliweza kutunga
Kanuni za Bunge Maalum kwa maridhiano kwa muda wa takriban mwezi mmoja. Vilevile,
ni kupitia Kanuni hizo, Viongozi wa Bunge Maalum waliweza kuchaguliwa na
kufanya Bunge hilo kuwa Chombo Maalum chenye Uongozi na kuwa na Mamlaka yake ya
Kisheria.
Mheshimiwa
Spika,
96.
Kanuni ya 46 ya Bunge Maalum la Katiba inaeleza mambo yasiyoruhusiwa kwenye
Bunge Maalum yakiwemo kutumia lugha ya kuudhi, kubagua, kunyanyapaa au
inayodhalilisha watu wengine. Aidha, Kanuni hii ya 46 inatoa utaratibu mzima wa jinsi ya kushughulikia masuala haya
ndani ya Bunge Maalum. Kanuni ya 16 (3)
inatoa nafasi kwa Mjumbe au Wajumbe wa Bunge hilo ambaye hakuridhika na uamuzi
wa Mwenyekiti uliotolewa, kuwa atakuwa na haki ya kuwasilisha kwa maandishi
malalamiko yake kwa Katibu ndani ya siku moja kuanzia tarehe ya uamuzi.
97.
Kwa muendelezo huo huo, Kanuni ya 59 (1) (d) inaelekeza kuwa, moja ya
majukumu ya Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum ni kuchunguza kuhusu
masuala yote ya haki, kinga na madaraka ya Bunge Maalum yatakayopelekwa kwenye
Kamati hiyo na Katibu kutoa taarifa kwa Mwenyekiti baada ya taarifa hiyo
kuwasilishwa kwenye Bunge Maalum. Kutokana na utaratibu huo wa Kikanuni kama
ilivyoainishwa katika Kanuni hizo za Bunge Maalum, ninapenda kutumia fursa hii
kuwashauri “Wana UKAWA” ambao wengi
wao wamo ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wenzangu wote wa Bunge
Maalum ambao wamo ndani na nje ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa ujumla wetu kutumia mifumo iliyowekwa na Bunge Maalum kupeleka malalamiko yote
katika Kamati ya Kanuni ya Bunge Maalum ili yapatiwe ufumbuzi ndani ya Bunge
Maalum na siyo nje ya Bunge. Hilo ndilo
jambo la busara!!
Mheshimiwa
Spika,
98.
Mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya, ambao
kimsingi ni wa Kisheria umeanza siku nyingi na kwa hatua mbalimbali shirikishi
kwa makundi ya watu na Vyombo mbalimbali, kupokezana majukumu kwa lengo la
kufanikisha azma ya kupata Katiba Mpya. Ninapenda kuwakumbusha Wajumbe wenzangu
wa Bunge Maalum la Katiba popote walipo ndani na nje ya Bunge hili kuwa, kuwepo
kwetu katika Bunge Maalum la Katiba ni jambo la Kisheria na si jambo la kawaida
wala la hiari. Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, sote kwa ujumla wetu tuna
wajibu wa kukamilisha sehemu yetu kama Wajumbe wa Bunge Maalum kwenye mchakato
mzima wa kuandaa Katiba Mpya.
Mheshimiwa
Spika,
99.
Vilevile, napenda kukumbusha kuwa Bunge Maalum
la Katiba si hatua ya mwisho ya mchakato huu. Baada ya Bunge Maalum la Katiba
kumaliza wajibu wake, Rasimu itakayokuwa imependekezwa na Bunge Maalum
itatakiwa kuwasilishwa kwa Wananchi wote wa Tanzania waisome, waielewe na kisha
waweze kuipigia kura ya maoni kuikubali au kuikataa kwa mujibu wa Sheria iliyopo
ya Kura ya Maoni mwaka 2013. Hivyo, ni vyema tukaelewa vizuri suala hili na kwamba,
bado kuna Wananchi wenzetu wengi kwa idadi ambao nao wanasubiri haki yao ya
Kisheria katika kukamilisha mchakato huu kabla ya kupata Katiba Mpya. Hivyo tusiwanyime haki hiyo!
100.
Ninapenda kuwashauri Wajumbe wenzangu ambao wameamua kususia Vikao vya Bunge Maalum la
Katiba kutafakari uamuzi na matendo yao kwa kutambua masharti ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalum la Katiba na wajibu wao kwa
Wananchi. Sisi wote tuliopo hapa tuna wajibu huo wa kukamilisha kazi hii muhimu
tuliyopewa kisheria ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata Katiba Mpya.
101.
Hivyo, natoa wito kwa Wajumbe wote wa Bunge
Maalum la Katiba ambao wamesusia Vikao vya Bunge Maalum la Katiba, warejee kwenye Bunge hilo ili tuweze
kuendelea na Mjadala wa Rasimu ya Katiba huku tukitumia utaratibu mzuri wa maridhiano
uliowekwa Kikanuni kutatua tofauti zilizopo.
HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika,
102.
Changamoto kubwa iliyoko mbele yetu baada ya
kuwepo hapa Bungeni kwa takriban miezi miwili ni kusimamia utekelezaji wa
Bajeti ya Serikali tuliyoipitisha. Sisi kama Wabunge tuondoke hapa kwa lengo
moja la kushirikiana na Wananchi kusukuma maendeleo na Bajeti tuliyoipitisha
ikiwa ndiyo kichocheo kikuu. Twendeni tukasisitize umuhimu wa kuishi kwa amani,
upendo na mshikamano. Tukiwasimamia vizuri na kuwaongoza Wananchi katika
matumizi ya rasilimali hata kama ni kidogo kiasi gani, Nchi yetu itasonga mbele
kimaendeleo na maisha bora kwa Wananchi wetu yatapatikana.
SHUKRANI
Mheshimiwa
Spika,
103.
Baada ya kusema hayo, napenda hasa nimalizie
kwa kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Nikushukuru kwa namna
ya pekee wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri
kulingana na Kanuni za Bunge. Aidha, nimshukuru Mwenyekiti, Mheshimiwa Mussa
Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala kwa kuongoza vizuri baadhi ya Vikao vya Bunge
wakati wa Mkutano huu. Ninawashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango
yenu ya dhati na yenye Mantiki kwa ajili ya Maendeleo ya Nchi yetu. Niwashukuru
Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Watumishi na Wataalam wote wa Serikali
waliosaidia kujibu Maswali na hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge
zilizojitokeza hapa wakati wa Mkutano huu. Vilevile, nawashukuru Waandishi wa
Vyombo vya Habari kwa kuwapatia Wananchi habari kuhusu Majadiliano yaliyokuwa
yanaendelea hapa Bungeni. Wote kwa ujumla wenu nawashukuru sana.
Mheshimiwa
Spika,
104.
Kipekee napenda kuwashukuru Madereva wote
ambao wamekuwa makini katika kazi ya kuwaendesha Viongozi wote, wakiwemo
Waheshimiwa Wabunge na Wataalam kutoka shemu mbalimbali Nchini na kuwawezesha
kufika hapa Dodoma kuhudhuria Mkutano huu wa Kumi na Tano. Vilevile,
nawashukuru Wananchi wa Mkoa wa Dodoma, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa
Dkt. Rehema Nchimbi kwa ukarimu wao kwa muda wote tuliokaa hapa Dodoma.
Nivishukuru pia Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambavyo vimehakikisha muda wote
tumekaa kwa Amani na Utulivu mkubwa. Mwisho namshukuru Katibu wa Bunge, Dkt.
Thomas Kashilillah na Watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa huduma nzuri
zilizowezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa katika Mkutano huu bila
matatizo.
Mheshimiwa
Spika,
105.
Nitumie fursa hii kuwaombea safari njema
mnaporudi katika maeneo yenu ya
kazi. Lakini pia niwaombee
kheri na Baraka tele Waislamu wote ambao wameanza na wanaendelea
na Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kila atakayeamua kufanya Ibada hiyo
aifanye kikamilifu na kama Kitabu cha Quran Tukufu kinavyoelekeza.
Mheshimiwa
Spika,
106.
Baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja
kwamba, Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 04 Novemba, 2014 siku ya Jumanne, Saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 16 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
No comments:
Post a Comment