Wednesday, May 7, 2014

VIONGOZI WA DINI MIKOA YA LINDI NA MTWARA ZIARANI THAILAND

Na Abdulaziz, Lindi 
Jumla ya Viongozi 19 wa Dini kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara wanaendelea na ziara ya mafunzo nchini Thailand kufuatia jitihada za serikali katika kuhakisha elimu kuhusu masuala ya gesi asilia na mafuta inatolewa kwa wananchi wa kada mbalimbali ili waweze kufahamu mchakato mzima wa upatikanaji wa gesi asilia na mafuta, faida zake katika nyanja za kiuchumi na kijamii, changamoto zake na namna nchi nyingine zinavyotumia rasilimali hiyo katika kukuza uchumi. 
Mafunzo hayo ya kujenga uelewa wa faida za kuwa na rasilimali hizo Viongozi hao wataitumia elimu hiyo katika kuwaelimisha wananchi kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini ili kujenga uelewa wa pamoja utakaowafanya wananchi kushiriki na kuwa na mtazamo chanya kuhusu miradi mbalimbali ya gesi asilia nchini. 
Akiongea kwa niaba ya viongozi hao wa dini waliokwenda nchini Thailand,Mkuu wa wilaya ya Kilwa,Abdallah Ulega aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kushirikisha viongozi wa dini katika masuala mbalimbali ya kitaifa. 
Amesema kuwa viongozi hao wa dini wamehudhuria mafunzo hayo kwa umakini mkubwa na baada ya kupata uelewa mpana kuhusu gesi asilia na mafuta kutoka nchi nyingine,sasa tutakuwa mabalozi katika kutoa elimu kwa waumini na wananchi kwa ujumla ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sekta hiyo nchini. 
Pamoja na kujifunza masuala ya gesi asilia na mafuta nchini Thailand,Tumetapata fursa ya kutembelea eneo maalum la viwanda ambalo ukuaji wake umetokana na kuwepo kwa gesi asilia, Shirika la Umma linalojishughulisha na masuala ya Gesi na Mafuta, Mamlaka ya Uzalishaji Umeme, Mamlaka ya Usambazaji Umeme, mtambo wa kuzalisha umeme unaotokana na Tungamotaka (Biomass), mtambo wa umeme wa jua, na mtambo wa umeme wa Bayogesi. 
Nae Katibu wa Baraza kuu la waislamu Mkoa wa Lindi,Alhaj Abdillah Salum akiongea kwa njia ya simu na mtandao huu alieleza kuwa Jamii ya Mikoa ya Kusini Lindi na Mtwara sasa wakati umefika wa kunufaika na rasilimali hizo hivyo aliwataka wanajamii kujikita katika Suala la Elimu ili Vijana wanufaike na ajira za Gesi na Mafuta.
Mafunzo hayo ya Viongozi wa dini ni mfululizo wa mafunzo yaliyotolewa kwa Wabunge,Madiwani na Viongozi wa serikali ambapo pia Wana habari 12 wa mikoa hiyo nao watapata Fursa ya Kwenda Nchini Humo kwa Mafunzo yanayogharamiwa na Wizara ya Nishati na Madini.










No comments: