Monday, April 14, 2014

Kufikia kikomo kwa Windows XP, nini athari zake kwa mtumiaji?


Mnamo tarehe 8/4/2014 kampuni ya utengenezaji wa mitambo endeshi ya kompyuta (Operating Systems) ya Microsoft ilisitisha utoaji wa huduma za muda mrefu kwa mitambo ya XP, ni moja ya mitambo endeshi inayotumika na watu wengi sana.Tangu kutoka kwa taarifa hizo, kumekuwa na maneno na mikanganyiko mingi mno kwa wateja hususan hapa Tanzania.

Kwakuwa ni mitambo inayotumika kwa weingi kwenye kompyuta nyingi zinazotumika kwenye mabenki na maofisini, hivyo watu walifika mbali hata kusema eti pesa zetu hazipo salama tena. Hivyo, ili kuondoa hofu hizi zinazoizunguka jamii, ungana nasi Dudumizi kwenye kujua nini maana ya kikomo hiki cha huduma na jinsi gani kinaweza kuathiri biashara yako?

 Kwanini XP imefikia kikomo?

XP iliingia sokoni miaka 12 iliyopita, tangu kuingia kwake, imekuwa ni mtambo endeshi unaotumika kwa wingi na makampuni mengi duniani kote. Na pia ni moja ya mtambo endeshi kutoka Microsoft uliokaa kwa muda mrefu sokoni. Ingawa katika uhai wa Windows XP, kumekuwa na matoleo mengine mengi kama Windows Vista, Windows 7 na ya sasa ambayo ni Windows 8, lakini kampuni ya Microfost imeendelea kutoka msaada wa kiufundi na kimatumizi kwa wateja wake wote, hivyo kwa maneno mengine tunaweza kusema,muda wake wa maisha umefika na ni mzigo kiutendaji na hata kibiashara kwa Microsoft kuendelea kuhudumia Windows XP ndiyo maana wameamua kusitisha huduma kwa Windows XP.

Je nini maana ya usisitshwaji wa Huduma?

Hapa ndipo palitokea mkanganyiko miongoni mwa watu wengi, kusitishwa kwa huduma hakumaanishi kuwa kompyuta zote zinazotumia XP hazitotumika tena kama wengine walivyoifananaisha na uhamaji wa mitambo ya analog kwenda Digital. 

Kusitisha kwa huduma kwa XP kunamaanisha, kampuni ya Microfot haitoendelea kutoa huduma (Support) kwa watumiaji wa windows XP tena, huduma hizi ni kama masasisho (updates) ya kiusalama, maboresho ya ufanyaji kazi (kama vile XP SP1, 2..) na huduma nyongine za utumiaji.

Hivyo, unaweza kuendelea kuitumia XP bila shida kama una uhakika kukosa huduma hizo hakutoathiri biashara.

Je kama ninatumia Windows XP, kompyuta yangu itaendelea kutumika?
Jibu ni ndiyo ila kuwa makini. Kusitishwa kwa huduma kwa Windows XP hakumaanishi kuondolewa kwa XP toka kwenye kompyuta yako, bali ni kutoweza pata huduma, hivyo Windows iliyopo kwenye komputa yako itaendelea kutumika kama kawaida, ila kuanzia sasa uhakika wa usalama wako utaendelea kupungua siku hadi siku.

Nini athari za kuendelea kubakia kwenye Windows XP?

Kama nilivyofafanua hapo juu, kusitishwa kwa utoaji wa huduma kwa XP, kunamaanisha Microsoft haitohusika na chochote kinachotokea kwenye matumizi ya XP, hivyo basi kuendelea kutumia XP inamaanisha ni kama mtoto aliyeamua kujitegemea yeye mwenyewe.

Kama wengi walivyowahi kusema, Windows XP ni moja ya mitambo endeshi ambayo haikuwahi kuwa tengevu (stable), imekuwa ikishambuliwa sana na virusi, minyoo nk, mara nyingi Microsoft wamekuwa wakitoa masasisho ya kuja kuzuia hizi vamizi, hivyo kama utaamua kuendelea kubaki kwenye XP, unatakiwa ujiandae na matumizi bora bila kusahau programu za usalama (Anti Virus) zilizo thabiti.

Virusi vinavyoishambulia Windows XP vilianza kupungua baada ya kuja kwa Windows Visa na Windows 7, ila kwa siku za hivi karibuni, tangu kutangazwa kwa kusitishwa kwa huduma, tumeshuhudia kurudi tena tena kwa kasi zaidi vamizi zinazolenga windows XP.

Je ni Windows ipi ninashauriwa kuhamia?

Kwa watu binafsi wanaweza kuhama kwenda Windows 8 kwa kununua leseni binafsi, na wale wa makampuni, wanaweza kuhama kwa kununua leseni ya kampuni na kuhama kwa ujumla. Timu yetu ya Dudumizi inaweza kukusaidia kwenye ushauri juu ya hili.

Ushauri:

Kwa wale wanaotumia Windows XP kwa watumiaji wakubwa (kama mabenki), ni dhahiri kuwa hawatoweza kuhama kwa mara moja, watahitaji muda mpaka waje kuhama, hivyo wanahitaji kuja na njia ya mpito itakayowawezesha kupambana na matatizo yoyote yatakayojitokeza kipindi wanajipanga kuhamia kwenye matoleo mengine ya Windows. 

Kwa mfano, Umoja wa nchi za Ulaya umeingia mkataba na Microsoft kuendelea kutoa huduma kwa Windows XP kwa miaka miwili hadi hapo watakapokuwa wamehama moja kwa moja.Na kwa watu binasi, unaweza kununua nakala ya Windows 8 na kuhamia huko bila kupotea chochote.

 Dudumizi Technologies inaweza kukusaidia kwenye hili, wasiliana nasi kwa kutuandikia info@dudumizi.com au tupigie0768816728.

Timu nzima ya Dudumizi inakushauri kuhakikisha unakuwa na mpango thabiti wa matumizi ya kompyuta katika kampuni yako, na kama ni kwa matumizi binafsi, basi hakikisha unafuata kanuni bora za matumizi ya kompyuta, na hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha unakuwa salama.

Na. Mkata Nyoni

No comments: