Tuesday, February 25, 2014

WADAU WA MADINI WATAKIWA KUJENGA MITANDAO YA BIASHARA YA MADINI

Kamishna Msaidizi wa Madini ,Wizara ya Nishati na Madini , Mhandisi Hamis Komba akiongea jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Thailand Mhe. Srirat Rastapana mara baada ya kufungua maonesho ya 53 ya “Bangkok Gems & Jewelry Fair” mapema leo. Nyuma ya Kamishna ni Bw. Edward Rweymamu ni Mthamini wa Madini ya Almas Wizara ya Nishati na Madini. Kushoto Mhe. Dora Mushi mfanyabiashara wa madini kutoka Arusha.
Rais wa Shirikisho la madini ya vito na usonara la Thailand Bw. Somchai Phornchindarak akiangalia madini ya Almas katika banda la Tanzania. Anamwelekeza jambo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Vito ya Shirikisho la Wachimbaji Tanzania (FEMATA), Bw. Gregory Kibusi. Wengine wanaoshuhudia ni baadhi ya ujumbe wa Tanzania unaoshiriki maonesho hayo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) Sam Mollel wa pili kulia akionesha Hati ya Maridhiano ya kuendeleza ushirikiano wa tasnia ya madini ya vito na usonara baada ya kusaini kati yake na Rais wa Rais wa Shirikisho la madini ya vito na usonara la Thailand Bw. Somchai Phornchindarak. Wanaoshuhudia ni Kamishna msaidizi wa Madini, Mhandisi Hamis Komba (Wa kwanza kulia) na Makamu wa Rais wa Shirikisho la madini na usonara la Thailand Bw. Peter Brooke.
Ujumbe wa Tanzania katika maonesho ya 53 ya Kimataifa ya Bangkok katika picha ya pamoja na Rais Rais wa Rais wa Shirikisho la madini ya vito na usonara la Thailand Bw. Somchai Phornchindarak (aliyeshika kinyago cha mamba kilichochongwa kutokana na mawe ya madini yanayopatikana nchini Tanzania. Kinyago hicho kimechongwa na Kituo cha 'Tanzania Geomological Center' kilichopo Arusha.) Wa tatu kutoka kushoto ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la madini na usonara la Thailand Bw. Peter Brooke.
Balozi wa Afrika ya Kusini nchini Thailand Mhe. Ruby Marks (katikati) katika picha ya pamoja na wafanyabiashara ya madini( wa kwanza kushoto, Bw. Sam Mollel mwakilishi kutoka Tanzania Geomological Center (wa tatu kulia) Bw. Musa Shanyangi Mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Kamati ya Vito ya Shirikisho la Wachimbaji Tanzania (FEMATA), Bw. Gregory Kibusi.(nne kulia).

Na Asteria Muhozya, Bangkok,

Nchi washiriki wa Maonesho ya 53 ya Kimataifa ya “Bangkok Gems & Jewelry Fair” wametakiwa kuyatumia maonesho hayo kujenga mitandao ya biashara ya madini ya vito na  usonara ili kusaidia kuinua uchumi na mapato ya nchi zao.

Akizungumza katika ufunguzi wa maonesho hayo, yaliyoanza leo jijini Bangkok, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Thailand, Mhe. Srirat Rastapana, ameeleza kuwa, maonesho hayo ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa biashara, ukuaji wa uchumi na uwekezaji kupitia sekta ya madini.

Vilevile alieleza kuwa, mbali ya kujenga mtandao wa kibiashara, amewataka washiriki kuyatumia maonesho hayo, kubadilishana uzoefu na teknolojia zinazotumika katika sekta hiyo.

Akielezea uzoefu wa nchi hiyo katika sekta ya madini ameongeza kuwa, madini ya vito na usonara  yamechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa  nchi hiyo na kuongeza pato la taifa hivyo, serikali ya Thailand inayapa kipaumbele kikubwa  maonesho hayo  kutokana na mchango wake katika maendeleo ya taifa.

Akielezea mafanikio katika sekta hiyo, ameongeza kuwa, madini na vito nchini Thailand yamesaidia kuzalisha watalaamu  zaidi ya milioni moja katika sekta ikiwa  ni pamoja na kuongeza pato la taifa ambapo kwa mwaka 2013 Serikali iliingiza kiasi cha zaidi ya dola za Marekani bilioni moja.

 “ Tunataka  kuona Bangkok inakuwa kituo kikubwa cha biashara ya madini, na tunakuwa bora katika  kutengeneza bidhaa zinazotokana na madini duniani. Alisema”.

Kwa upande wake Kamishna msaidizi wa Madini, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Hamis Komba ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika maonesho hayo ya 53 amesema kuwa, Serikali imeimarisha ushirikiano na wafanyabiashara wa madini na wachimbaji ili kuiwezesha seka ya madini kuleta tija kwa taifa ikiwemo kuvutia uwekezaji  na kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara ya madini ya vito na usonara.

Aidha ameongeza kuwa, tayari Serikali imeondoa kwa muda zuio la kusafirisha madini ghafi aina ya Tanzanite ili kuwezesha uwepo wa Tanzanite katika maonesho ya 53 na katika banda la Tanzania, jambo ambalo linarahisisha na litawasaidia wafanyabiashara wa Tanzanite kufanya biashara kimataifa.

Vilevile ameongeza kuwa, tayari Serikali iko katika hatua za kukusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu  Sheria ya Uongezaji thamani madini  jambo ambalo litasaidia kuboresha sekta hiyo, hivyo, kukamilika kwa sheria hiyo kutawanufaisha  wadau wote  wa sekta ya madini wakiwemo wafanyabiashara, masonara wachimbaji na  Serikali jambo ambalo litachangia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya madini kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo  zimefanikiwa katika sekta hiyo.

Kuhusu suala la utoroshaji wa madini, Kamishna komba amesema kuwa, sheria pekee haiwezi kuzuia tatizo hilo, hivyo amewataka wafanyabiashara kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali ili sekta ya madini iweze kunufaisha pande zote na kuwanufaisha watanzania wote.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) Sam Mollel amewataka wafanyabiashara kuyatumia maonesho ya kimataifa kuonesha bidhaa zao kwa kuwa  kuna  mafanikio makubwa, mbali ya kufanya biashara kwani watajifunza  mengi kuhusiana na madini, kwa kuwa yapo mengi ya kujifunza ikiwemo kujifunza kutoka kwa waoneshaji wengine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati  ya  Vito  ya Shirikisho  la Wachimbaji Tanzania (FEMATA) Bw. Gregory Kibusi ameishukuru Serikali kuwawezesha kushiriki maonesho hayo, kwani kufika kwao  kumewafunza mengi ikiwemo kupata uzoefu
kuhusu sekta hiyo ikiwemo kujua tecknolojia zinazotumika kukata madini, kujua umuhimu wa kukata madini,  kujua bei, fursa ya kukutana na wafanyabiashara wa kimataifa  jambo ambalo limechangia kuwapa elimu zaidi kuhusu madini na vito kutoka nchi zilizofanikiwa katika biashara ya madini ikiwemo  wenyeji Thailand, Marekani, India na Sirilanka lakini pia uzoefu kutoka nchi za kiafrica kutoka Senegal, Ghana, Madagasca, Nigeria, Cameroon na nchi nyingine za nje ya Africa.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini (TAMIDA) Bw. Sam Mollel, amesaini hati ya maridhiano ya kuendeleza ushirikiano katika tasnia ya madini ya vito na usonara na Rais wa Shirikisho la madini ya vito na usonara la Thailand Bw. Somchai Phornchindarak.

No comments: