Thursday, January 30, 2014

Wachimbaji wadogo watakiwa kuzingatia kanuni za usalama migodini

Mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mhandisi Dkt. Crispin Kinabo akiwasilisha mada juu ya utunzaji wa mazingira kwenye migodi wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika mapema leo katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. Mafunzo hayo yalishirikisha viongozi na watendaji wa wilaya, madiwani, wakuu wa vitongoji na wachimbaji wadogo lengo lake likiwa ni kuwapa uelewa wa kanuni za uchimbaji bora wa madini.
Mmoja wa wakilishi wa wachimbaji wadogo ambaye ni mmiliki wa mgodi katika eneo la Mhesi Mapinduzi lililopo wilayani Tunduru Bi Sofia Hamdan akichangia mada wakati wa mafunzo hayo.
Mpepo Ismail ambaye ni mmoja wa wachimbaji wadogo na mmiliki wa machimbo ya shaba Mbesa akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho. Ameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwakopesha vifaa vya kuchimba madini.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zinawasilishwa na watoa mada kwa nyakati tofauti (hawapo pichani).


Na Greyson Mwase, Tunduru

Wachimbaji wadogo wametakiwa kuzingatia kanuni za usalama migodini ili kuepuka majanga yanayoweza kujitokeza na kuleta athari kwa jamii kwa ujumla.

Hayo yalisemwa na Afisa Madini Mkazi Tunduru Mhandisi Frederick L. Mwanjisi alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mafunzo yaliyoshirikisha wachimbaji wadogo, viongozi na watendaji wa wilaya, madiwani na wenyeviti wa vitongoji yanayoendelea wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Mhandisi Mwanjisi alisema kuwa wachimbaji wengi wamekuwa wakithamini madini kwanza badala ya mazingira kwa jamii inayowazunguka jambo linalosababisha kujitokeza kwa majanga ya mara kwa mara kama vile kuanguka kwa vifusi na kemikali kuathiri binadamu ikiwa ni pamoja na wanyama.

“ Wachimbaji wamekuwa wakitanguliza msemo usemao “madini kwanza” kwa kufikiria maslahi yao binafsi badala ya kufikiria jamii inayowazunguka kwa kuweka mazingira katika hali ya usalama yaani msemo uwe “Usalama kwanza” Alisisitiza Mhandisi Mwanjisi.

Mhandisi Mwanjisi alibainisha athari zinazosababishwa na majanga yanayotokana na kutokuzingatia usalama migodini ni pamoja na mmiliki kupoteza fedha nyingi kwa ajili ya fidia, miundombinu kuharibika, kupoteza imani kwa wafanyakazi na umma kwa ujumla hali inayoweza kupelekea hata mgodi kufungiwa.

Aliendelea kutaja athari nyingine kwa upande wa wafanyakazi kuwa ni pamoja na kupoteza nguvu kazi, ulemavu wa maisha, kuathirika kisaikolojia ikiwa ni pamoja na kukosa furaha ya maisha.

Mhandisi Mwanjisi aliongeza kuwa jukumu la usalama kwenye migodi ni la wote kuanzia wamiliki wa migodi, wafanyakazi, serikali ikiwa ni pamoja na jamii inayozunguka migodi.

Mhandisi Mwanjisi aliainisha kanuni za usalama migodini ikiwa ni pamoja na uvaaji wa vifaa vya kujikinga na mazingira hatarishi, kuweka mgawanyo wa kazi kulingana na taaluma na uzoefu wa wafanyakazi migodini, kufukia mashimo ikiwa ni pamoja na kuwekea wigo maeneo hatarishi ndani ya migodi.

Aliongeza kanuni nyingine za usalama ni pamoja na kufanya ukaguzi wa maeneo ya machimbo kabla ya kuanza kazi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa mkaguzi wa migodi juu ya matukio ya hatari au ajali zinazotokea migodini.

Kanuni nyingine ni pamoja na kuwa na orodha ya wafanyakazi wote wa mgodi katika daftari maalumu, vifaa vya huduma ya kwanza na kutoshirikisha watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 katika kazi za machimbo.

Aidha Mhandisi Mwanjisi aliwataka wachimbaji wadogo kuwa na mpango wa usalama kwenye migodi wenye kuainisha tahadhari zinazoweza kuchukuliwa pindi majanga yanapotokea katika migodi badala ya kutokuwa na mpango wowote hali inayopelekea ugumu katika kushughulikia kwa haraka majanga yanapojitokeza.

Wakati huo huo mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Jiolojia Mhandisi Dkt. Crispin Kinabo aliongeza kuwa wachimbaji wadogo mbali na kuzingatia kanuni za usalama migodini wanatakiwa kufanya tafiti za kijiolojia kabla ya kuanza uchimbaji wa madini ikiwa ni pamoja na kusoma ramani za kijiolojia.

Dkt. Kinabo aliwataka wachimbaji wadogo kuachana na uchimbaji wa mashimo kiholela bila kusoma ramani za kijiolojia za maeneo husika hivyo kupelekea kuwa na mashimo kila mahali na hivyo kupelekea majanga ya kujitakia.

Aidha Dkt. Kinabo aliwataka wachimbaji kuzingatia kanuni za mazingira kwa kutunza vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na mpango wa kuotesha miti.

Mafunzo haya yaliandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini lengo lake likiwa ni kuwapa uelewa wa kanuni za uchimbaji bora wa madini wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na viongozi na watendaji wa wilaya, madiwani, wakuu wa vitongoji na wachimbaji wadogo.

No comments: