Mkurugenzi wa Kampuni ya Saseni Media, Bw. Issa Mbura akizungumza katika warsha hiyo kwa wasanii mbali mbali wa filamu hapa nchini.
Kampuni ya Saseni Media, kwa kupitia mpango wake wa kukuza vipaji vipya vya uigizaji na kuvisimamia, iliendesha kwa mafanikio makubwa zoezi la usaili kwa waigizaji wazoefu na wanaochipukia siku ya jumamosi, tar 25 Januari 2014.
Idadi kubwa ya watu ilijitokeza kujisajili na kufanyiwa usaili na kila mwigizaji alionekana kuwa ni mwenye shauku ya kutaka kupata fursa hiyo na hivyo kuonyesha umahiri wake katika uigizaji. Akizungumzia usaili huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Saseni Media, Bw. Issa Mbura amesema
“Zoezi lilienda vizuri na pamoja na kupata vipaji kama lilivyokuwa kusudio letu, pia tumeshuhudia mambo kadhaa yakijitokeza kama changamoto kwa tasnia ya filamu inayotegemea sana waigizaji ili kufanya vizuri,” “Moja, ni kwamba Tanzania kuna waigizaji wengi wanaochipukia na kutafuta fursa za kuigiza kuliko wale wachache tuliozoea kuwaona kwenye luninga zetu,”anasema Mwl. Issa.
Wanachohitaji ni jukwaa la kuwawezesha kuonyesha vipaji vyao lakini mfumo na biashara ya filamu haujatoa fursa hizo hasa pale unapotumia zaidi waigizaji wanaofahamika (Stars). Hii inapelekea wao kutafuta kila namna ya kufanikiwa na kujikuta wanagharamika bila mafanikio. Mfano mmoja ya vijana tuliowafanyia usaili amesema ametumia takribani zaidi ya elfu hamsini kama ada ya kujiunga na vikundi vya sanaa bila mafanikio ya kuigiza kwenye TV au filamu mpaka sasa.
Mbili, idadi ya watu waliojitokeza kwenye usaili wametoka kwenye vikundi vya sanaa wakiwa wamejiunga kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu. Nilichokigundua ni kwamba Dar es salaam inaweza kuwa na idadi kubwa zaidi ya vikundi vya sanaa ukilinganisha na mikoa mingine mikubwa kama Dodoma, Mwanza, Mbeya nk. Hii ina maana vipaji tunavyopata kuvishuhudia mpaka sasa ni vipaji vya wazawa au wahamiaji wa Dar es salaam. Hii inapunguza ladha na changamoto katika uigizaji anasistiza Bw. Mbura.
Tatu, na mwisho, waigizaji wamekosa fursa rasmi za mafunzo katika ngazi ya cheti ama diploma. Katika ngazi ya digrii idara ya sanaa ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam imekuwa ikitoa mafunzo lakini waigizaji wengi hawana vigezo vya kusoma digrii. Hii inamaanisha waigizaji wengi hawana mafunzo rasmi na wanategemea kutazama wanachokifanya wengine na kuiga au kujiunga na vikundi kupata nafasi za kufanya mazoezi kujifunza. Hii imepelekea pia wengi kudhani uigizaji ni ule wa filamu tu na kusahau uigizaji wa tamthilia za TV, Michezo ya Radio, Filamu fupi, Matangazo ya Biashara nk. ambayo humpa fursa muigizaji kuweza kukuza kipaji chake na kufikia ubora wa ndani na wa kimataifa kabla ya kuigiza kwenye filamu.
Ukiacha yote hayo, Tanzania ina vipaji vya kutosha kuipa tasnia ya filamu thamani inayostahili. Marehemu Steven Kanumba anaonekana kuwapa hamasa vijana wengi kujiingiza kwenye tasnia ya filamu na hasa uigizaji kwani idadi kubwa ya watu waliokuja kwenye usaili wamemtaja yeye kama ndio muigizaji wanaempenda. Wengine waliotajwa ni JB na Jackline Wolper.
Tunahitaji kuibua na kukuza vipaji vipya katika uigizaji na kujali ubora wa filamu zetu. Timu nzima ya Saseni media tunayo dhamira ya dhati kuona hilo linajitokeza. Pamoja na changamoto nyingi na uchanga wa kiwanda chetu kibiashara, kimfumo na kisera bado naamini kwamba tunayo nafasi ya kujenga msingi mzuri kwa vizazi vya watoto na wajukuu wa wajukuu zetu kama tukianza sasa.
Anaelezea Bw. Issa Mbura ambaye pia ni Mwandishi wa miswada, Mtayarishaji na Mwongozaji wa filamu hapa Tanzania.
No comments:
Post a Comment