Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu (wa pili kulia) akisisitiza jambo wakati wa ziara yake katika shamba la Mkulazi lililopo katika kata ya Mkulazi mkoani Morogoro Alhamis wiki hii. Wengine ni Meneja Kitengo cha Ardhi kutoka Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), Bw. Desiderius Narwango (kushoto) Mkurugenzi wa Huduma wa TIC, Bi. Nakuala Senzia (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro vijijini, Bw. Said Amanzi (wa pili kushoto).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu (wa pili kulia) akimsikiliza Meneja Kitengo cha Ardhi kutoka Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), Bw. Desiderius Narwango (kushoto) wakati wa ziara katika shamba la Mkulazi lililopo katika kata ya Mkulazi mkoani Morogoro Alhamis wiki hii. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma wa TIC, Bi. Nakuala Senzia na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro vijijini, Bw. Said Amanzi (wa pili kushoto).
Na Mwandishi wetu, Morogoro.
Serikali imewakikishia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwa itaendelea kuhakikisha kuwa inajenga miundombinu imara na muhimu kama barabara ili kufanya kazi zao kuwa nyepesi na hivyo kufikia maendeleo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu alitoa kauli hiyo katika eneo la kata ya Mkulazi, Wilaya ya Morogoro vijijini Mkoani humo Alhamis wiki hii, wakati alipofanya ziara katika shamba la Mkulazi linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 63 elfu.
Alisema siku zote wawekezaji wanapenda maeneo ambayo yanafikika kwa wepesi ili waweze kufanya biashara kwa uhuru, hivyo ni wajibu wa serikali kuiimarisha na kujenga mipya zaidi ili kuweka mazingira bora ya biashara nchini.
Alisema shamba la Mkulazi ni kubwa na wawekezaji wapo tayari kuwekeza hasa katika kilimo cha miwa hivyo ni jukumu la kituo cha uwekezaji nchini kuiona changamoto hiyo ili waweze kuwasiliana na mamlaka husika katika kuboresha miundombinu ya barabara.
“Hii ni changamoto kubwa, naomba tushirikiane wote kwa pamoja ili tuweze kulifanyia kazi jambo hili kwa haraka na mafanikio,” alisema waziri huyo.
Alisisitiza kuwa nchi itaondokana na umasikini kwa kiasi kikubwa iwapo dhamira itaelekezwa kwenye uwekezaji wa kilimo hasa katika mashamba makubwa ya mazao mbalimbali kama sukari na mpunga.
“Hivi sasa nchi yetu inaupungufu wa sukari hivyo uwepo wa wawekezaji katika sekta hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hili,” alisisitiza Dk. Nagu.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kutenga maeneo mengi kwa ajili ya uwekezaji na kuisisitiza kuendelea kutangaza vivutio vilivyopo katika nchi ili wawekezaji wengi waweze kuja na kuwekeza na hivyo kuinua uchumi wa nchi.
“Kwa kufanya hivyo tutapiga hatua kubwa katika uwekezaji,” aliongeza.
Awali akitoa maelezo kuhusu shamba hilo la Mkulazi, Mkurugenzi wa Huduma kutoka Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), Bi Nakuala Senzia, alisema tayari wataalamu wameshafika na kupima shamba hilo na tayari limegawanywa kulingana na matumizi.
“Shamba hili tayari limekwishagawanywa kulingana na matumizi ya wale watakaohitaji kuwekeza, vibali vimekwishatolewa tunachosubiri ni mkataba kutoka wizara ya ardhi,” alisema Mkurugenzi huyo.
Aliongeza kuwa kwa sasa wameshafanya mawasiliano na kambi ya jeshi ya Ngerengere ili waweze kusaidia kusafisha eneo la shamba hilo liwe katika muonekano mzuri tofauti na ule wa sasa.
“Tayari tumekwishaomba msaada wa jeshi la wananchi Ngerengere ili waweze kutusaidia na wako tayari kwa msaada huo, hivyo baada ya siku kadhaa muonekano washamba hili utakuwa katika hali nzuri,” alisisitiza.
Eneo la Mkulazi lililopo katika wilaya ya Morogoro vijijini ni eneo linalopitiwa na mito ya Ngerengere na Ruvu, na tayari baadhi ya wawekezaji walishafika na kujionea eneo hilo ambalo mazao kama miwa na mpunga yanatajwa kuwa yanaweza kustawi kwa wingi.
No comments:
Post a Comment