Tuesday, January 28, 2014

MKUTANO WA BARAZA LA MAWAZIRI WA AU WAFUNGULIWA ADDIS ABABA

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma akitoa hotuba ya ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unaofanyika Mjini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 27 na 28 Januari, 2014. Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi  na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika mjini hapa tarehe 30 na 31 Januari, 2014.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa AU, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa inatolewa na Dkt. Dlamini-Zuma (hayupo pichani). Wengine katika picha ni Mhe. Naimi Aziz (kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mhe. Balozi Tuvako Manongi (kulia), Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani akiwa na Wajumbe wengine wakifuatilia kwa makini hotuba ya Dkt. Dlamini-Zuma (hayupo pichani)
Makamishna wa AU na Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Dkt. Dlaini-Zuma  (hayupo pichani).
Mawaziri kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa baraza la mawaziri.
Kabla ya ufunguzi Dkt. Dlamini-Zuma aliwaongoza Wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri kusimama kwa heshima na kumkumbuka aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Hayati Mzee Nelson Mandela aliyefariki dunia mwezi Desemba, 2013.
Picha ya Pamoja mara baada ya ufunguzi.
Mhe. Membe akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, Mhe. Simbarashe Mumbengegwi (katikati) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Maite Nkoana-Mashabane
Maafisa Waandamizi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia wakibadilishana mawazo nje ya Ukumbi mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri.
Bw. Bujiku Sakila, Afisa Mambo ya Nje akimweleza jambo Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mambo ya Nje mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri.

Na Rosemary Malale, Addis Ababa

Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) imetoa rai kwa nchi za Afrika kuongeza uzalishaji na uwekezaji katika kilimo kwa vile kinachangia kwa kiasi kikubwa Pato la Taifa kwa nchi Barani Afrika.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma wakati akifungua Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ulioanza leo tarehe 27 Januari, 2014 Mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Dkt. Dlamini-Zuma alisema kuwa,  kwa Afrika kuhakikisha ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 7 na zaidi ni vema kilimo kiwe kipaumbele kwa nchi wanachama, kwa vile kinachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kwa nchi zao. Alisema kuwa kwa mwaka huu wa 2014 ni muhimu kuongeza uwekezaji katika kilimo, uzalishaji, kuboresha miundombinu na ujuzi ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika tafiti za kilimo.

Alisisitiza kuwa Kamisheni yake kwa mwaka huu imejipanga kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha kilimo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake ambao ndio kundi kubwa linaloshughulika na kilimo na chakula kwa kuwapatia  mafunzo, mitaji na kuwasaidia kuanzisha vikundi vya ushirika na masoko kwa bidhaa za kilimo. Pia, alieleza kuwa imefika wakati sasa kwa Afrika kuwa na kauli katika kupanga bei ya mazao na bidhaa zitokanazo na kilimo.

Aidha aliongeza kuwa, ili kufikia malengo hayo, Kamisheni ya Umoja wa Afrika itashirikiana na Taasisi nyingine za Kimataifa kama UNECA, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Nchi Wanachama, Vyama vya Kiraia na Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi.

Dkt. Dlamini-Zuma alieleza kuwa Mkutano wa mwaka huu wenye kaulimbiu isemayo “Mwaka 2014 ni mwaka wa Kilimo na Usalama wa Chakula; Kuadhimisha miaka 10 ya Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP)” unalenga kuweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha kilimo kinakuwa ni mkombozi wa Watu Barani Afrika kiuchumi na kwa usalama wa chakula.

Katika hatua nyingine, Dkt. Dlamini-Zuma ametoa wito kwa Waafrika wote kutoa michango na mawazo yao kuhusu Muundo wa Agenda 2063 ambayo inalenga katika kujenga Afrika Tunayoitaka katika kipindi cha miaka 50 ijayo kuanzia mwaka 2014.

Aidha, aligusia migogoro inayoendelea kusumbua baadhi ya nchi za Afrika kama vile Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo alisema kuwa Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi na Jumuiya ya Kimataifa zitaendelea kushirikiana ili kuzisaidia nchi hizi kupata suluhisho la kudumu katika migogoro yao.

“Mwezi Mei mwaka uliopita wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Afrika tuliahidi  kwa watu wetu kuwa hatutavirithisha vizazi vijavyo vita na migogoro bali tuliapa kufanya kazi bila kuchoka kuhakikisha migogogro Barani humu inamalizwa kabisa hadi kufikia mwaka 2020” alisema Dkt. Dlamini Zuma. Vile vile, Dkt. Dlamini-Zuma alizipongeza nchi za Mali, Madagascar na Somalia kwa hatua waliyofikia katika kushughulikia migogoro yao.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri  ambao utamalizika tarehe 28 Januari, 2014 ni matayarisho ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ambao utafanyika mjini hapa tarehe 30 na 31 Januari, 2014. Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri unaongozwa na Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

No comments: