Thursday, January 2, 2014

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI JOHN CASMIR MINJA AHUTUBIA BARAZA LA KUFUNGA MWAKA 2013 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2014

Na; Inspekta Lucas Mboje, Jeshi la Magereza

Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja amekemea vikali tabia ya baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza wenye tabia ya kutofuata Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika utendaji wao wa kazi za kila siku hivyo ameonya kuwa yeyote atakayekwenda kinyume hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake bila kujali cheo au wadhifa alionao.

Kamishna Jenerali John Minja ameyasema hayo juzi wakati wa Baraza la Kufunga Mwaka 2013 na kuukaribisha Mwaka 2014 lililowahusisha baadhi ya Maafisa na Askari kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga, D'Salaam, Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani(KMKGM) pamoja na Magereza Mkoa wa D'Salaam.

Aidha, amewataka Maofisa, Askari na Watumishi wote kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea bali wawe wabunifu kwa kutumia raslimali zilizopo kwenye maeneo yao ya kazi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo.

"Kila mmoja wenu anapaswa kujipima kwa kufanya vitu ambavyo atakumbukwa baada ya yeye kuondoka hapo alipo". Alisisitiza Jenerali Minja.

Wakati huo huo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja pia ametumia fursa hiyo kuelezea baadhi ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa Mwaka uliopita 2013 ambayo ni kufunguliwa kwa Maduka yenye kuuza bidhaa zisizo na tozo la Kodi( Duty Free Shops) katika Mikoa ya D'Salaam - Ukonga, Dodoma - Gereza Isanga, Kilimanjaro - Gereza Karanga, Morogoro - Chuo cha Udereva na Ufundi Kingolwira, Mwanza - Gereza Kuu Butimba ambapo pia tayari maandalizi yamekamilika ya kufunguliwa kwa huduma hiyo katika Mkoa wa Mbeya - Chuo cha Ufundi Ruanda, Arusha na Mtwara.

Pili, Jeshi limeendelea na utekelezaji wa zoezi la kuwasafirisha mahabusu Mahakamani na kurudi Magerezani na tayari zoezi hili linafanyika kwa mafanikio makubwa Mkoani Pwani, D'Salaam, Arusha na Dodoma. Zoezi hilo linaendelea hatua kwa hatua ili kuhakikisha kuwa huduma hii inasambaa nchi nzima.

Tatu, kwa Mwaka uliopita wa  2013 jumla ya Maafisa, Askari na Watumishi raia 3,300 wa Jeshi la Magereza wamepandishwa vyeo mbalimbali. Pia idadi ya Wakuu wa Magereza wa Mikoa Wanawake imeongezeka na kufikia Sita (6) baada ya Maafisa wawili (2) kuteuliwa hivi karibuni. Hatua hii inalenga kuwapa nafasi zaidi za Uongozi Wanawake wanaodhihirisha kuwa na uwezo katika Uongozi.

Vilevile, Jeshi la Magereza limefanikiwa kuadhimisha Siku ya Magereza( Magereza Day), Sherehe ambazo zilifanyika Chuo cha Maafisa Magereza, Ukonga mwezi Juni 22, 2013 ambapo yalifanyika maonesho mbalimbali ya shughuli zinazofanywa na Jeshi hilo. Pia Jeshi la Magereza limeendelea na Mchakato wa kuandaa Sera ya Magereza ambapo tayari hatua mbalimbali muhimu za maandalizi zimekamilika ikiwemo kukamilika kwa rasimu ya kwanza na kazi hiyo inafanyika kwa kushirikiana na Mshauri Mwelekezi toka Chuo Kikuu cha D'Salaam.

Kwa upande wa Michezo, Jeshi limeshiriki kikamilifu kwenye mashindano kadhaa na kushika nafasi mbalimbali za ushindi katika Michezo ikiwemo Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu, Handball, Volleyball. Aidha, timu ya Mpira wa Miguu ya Jeshi (Tanzania Prisons Sports Club) inashiriki kwenye Ligi Kuu inayoendelea.

Pamoja na Mafanikio hayo, Kamishna Jenerali Minja ameelezea maeneo yatakayopewa kipaumbele kwa Mwaka huu wa 2014 ikiwemo kuimarisha na kuongeza uzalishaji kwenye miradi mbalimbali ya Jeshi la Magereza, kuendelea kuimarisha huduma za ustawi wa Watumishi kwa kufungua maduka ya bidhaa zisizotozwa Kodi(Duty Free Shops), kuendelea na mchakato wa uandaaji wa Sera ya Magereza pamoja na kutatua tatizo la makazi kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza.

Aidha, Jeshi la Magereza litaendelea na mikakati ya kupunguza msongamano Magerezani kwa kuimarisha ushirikiano na Vyombo vya Haki Jinai, kuhamasisha matumizi ya adhabu mbadala, Pia, Jeshi litaendelea na jitihada za kutatua tatizo la Madeni ya Watumishi na wazabuni ikiwa ni pamoja na kufanya mawasiliano ya karibu na Mamlaka zinazohusika ili madeni hayo yaweze kulipwa kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu. Vilevile, Jeshi la Magereza litaendelea na mchakato wa kuunda Bodi ya Shirika la Magereza na kuhakikisha kuwa linachangamkia fursa za kibiashara zilizopo kama Shirika.

Baraza la kufunga Mwaka na kuukaribisha Mwaka unaofuata ni utamaduni wa siku nyingi ambao unaenziwa na Viongozi Wakuu wa Jeshi la Magereza. Baraza la aina hii hufanyika kila Mwaka ambapo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini hupata fursa ya kuongea na Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini kupitia Baraza hilo lengo ikiwa ni kufanya tathmini ya yale yaliyojiri katika Jeshi kwa kipindi cha Mwaka unaisha kwa kuzungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza na  kutazama matarajio ya Mwaka mpya.

No comments: