HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI
OFISI YA WAZIRI MKUU TAMISEMI MHE. HAWA ABDULRAHAMAN GHASIA WAKATI WA KUFUNGUA
MKUTANO MKUU WA SITA WA WADAU WA LAPF TAREHE 11/10/2013 KATIKA UKUMBI WA
KIMATAIFA WA MIKUTANO (AICC) – JIJINI ARUSHA
Mheshimiwa Gaudencia
Kabaka, Waziri wa Kazi na Ajira
Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Manaibu Mawaziri mlioko
hapa;
Waheshimiwa Wabunge;
Makatibu Tawala wa Mikoa
na Makatibu Wakuu mlioko hapa;
Mwenyekiti na Wajumbe wa
Bodi ya Wadhamini ya LAPF;
Mkurugenzi Mkuu wa LAPF;
Viongozi wa Wizara, Wakurugenzi
wa Halmashauri, Makampuni, Mashirika na Taasisi mbalimbali mnaochangia LAPF;
Wageni toka Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii ndani na nje ya nchi,
Wanahabari, Wageni
Waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Nianze kwa kukushukuru Mwenyekiti wa Bodi, Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini
pamoja na Menejimenti ya LAPF kwa kunikaribisha kwenye mkutano wenu huu lakini
pia niwapongeze sana kwa maandalizi mazuri ambayo sote tumeyaona.
Ndugu Washiriki, tumesikia maelezo toka kwa Mwenyekiti wa Bodi kuhusu masuala ya kisera
na mwelekeo wa Mfuko lakini pia tumesikia toka kwa Mkurugenzi Mkuu Bwana Sanga
kuhusu maendeleo ya LAPF kwa mwaka 2012/2013. Nawapongeza sana kwa mafanikio makubwa mliyopata
na nasema jitihada hizo ziongezeke ili wanachama wenu na wananchi wengine
waweze kunufaika zaidi.
Ndugu Washiriki, mkutano huu ni muhimu sana kwani ndio mkutano pekee katika mwaka
unaowakutanisha ninyi na hivyo kuwapa fursa ya kujadili hoja mbalimbali toka
LAPF. Ni fursa pia kwenu kuweza kuueleza
uongozi mambo ambayo mngependa Mfuko ufanye kwa manufaa yenu na wananchi kwa
ujumla. Hivyo tutumie vizuri sana siku
hizi mbili za mkutano kuibua maazimio ambayo ninyi pamoja na Mfumo mtaenda
kuyafanyia kazi.
Tumeambiwa kuwa kauli mbiu yetu ni Kutosheleza
kwa mafao ya Kustaafu: Changamoto na Njia za Kuboresha. Kauli mbiu hii ni muhimu sana ikajadiliwa kwa
kina kwa matokeo ya mjadala wake itatupa mwelekeo wa nini kifanyike kuboresha
zaidi mafao ya wanachama wa Mfuko. Ni
kweli kabisa wapo wastaafu wetu wamepata fedha nyingi sana lakini ndani ya
mwaka mmoja au miwili fedha hizo zinakuwa zimekwisha na hakuna jambo la msingi
walilofanya.
Inaonyesha dhahiri kuwa nidhamu ya utunzaji fedha kwa watumishi na
wastaafu wengi ni tatizo. Ni vizuri eneo
hili likajadiliwa kwa kina na mkaondoka hapa na maazimio ya kurekebisha dosari
hii. Najua kuwa uongozi wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii uko hapa. Naomba
mtumie nafasi hii kuona namna ambavyo mnaweza kuboresha sekta hii ili
iwanufaishe walengwa zaidi.
Nimeambiwa pia kuwa ipo mada kwa ajili ya mbinu za ujasiriamali. Tupende tusipende ujasiriamali haukwepeki kama
tunataka kumaliza sehemu yetu ya maisha kwa furaha na amani. Kila shughuli utakayoifanya baada ya kumaliza
utumishi wako ni ujasiriamali na shughuli hiyo itakuwa na manufaa kwako endapo
utakuwa umeifanyia maandalizi ukiwa bado kazini. Wale wanaokimbilia kujifunza biashara kwa
mfano ya daladala baada ya kustaafu
kimsingi wanajitafutia matatizo. Sio biashara
nyepesi kama wanavyofikiri ila ni rahisi endapo imefanyiwa utafiti wa kutosha juu
ya namna ya kuisimamia. Hivyo naona
Mfuko umefanya jambo la msingi sana kuleta mada hii hapa. Aidha, nashauri isiishie hapa ila nanyi
mhakikishie kuwa watumshi wengine walio kule maofisi wanapata taaluma hiyo japo
kwa uchache.
Ndugu Washiriki, katika sekta hii ya hifadhi ya jamii huduma bora ni jambo muhimu mno.
Wastaafu wengi wanasumbuka kupata mafao yao wanakuwa wamestaafu. Leo nafurahi kusikia na kuona kuwa LAPF sasa
inaweza kulipa wanachama wake kabla au katika siku ya kustaafu. Hili ni jambo zuri nami nashauri waajiri
mlichukue kwa umuhimu wake kwa kuhakikisha wale wanaokaribia kustaafu maombi
yao yanawasilishwa LAPF angalau miezi mitatu minne kabla ya tarehe ya kustaafu
ili Mfuko uweze kufanya malipo kama tulivyoona leo hapa. Huduma bora ni kivutio kikubwa cha wanachama
hivyo mkiendelea na kasi hiyo hakika mtapata wanachama wengi zaidi.
Ndugu Washiriki, nitoe rai kwa Mfuko wa LAPF kufanya kazi moja. Angalieni uwezekano wa kutoa “Guarantee” kwa
wanachama wenu ili wapewe mikopo na mabenki.
Hii itasaidia kukuza mitaji yao na kuzalisha zaidi, hivyo kua na uwezo
wa kuchangia zaidi katika mfuko. Ni
matumaini yangi likifanyiwa kazi jambo hili linaweza likawa ni fursa kwa Mfuko
na wanachama pia.
Mwaka jana tulizungumza kuhusu uwezekano wa kutoa mikopo ya elimu kwa
wanachama wa Mfuko. Leo mmesema kuwa
jambo hili sasa liko kwa mtathmini wa Mfuko. Naomba liharakishwe kwani nina uhakika
wanachama wenu wanalisubiri kwa hamu kubwa sana.
Ndugu Washiriki, nikirudi sasa kwenu, nawaomba sana mtimize wajibu wenu kwa kuwasilisha
michango kwa wakati. Michango hii inahitaji
kuwekezwa kwa wakati ili kuujengea Mfuko uwezo wa kuboresha zaidi mafao ya
wanachama wenu. Sasa inapocheleweshwa ni
hatari mfuko kupoteza mapato na hivyo uwezo wa kuboresha zaidi mafao.
Ndugu Washiriki, Sheria ya Mamlaka imetoa uhuru wa watumishi wapya kuamua Mfuko
wanaoupenda, hii ni njia nzuri ya kujenga mazingira ya ushindani na kuhakikisha
kila mfuko unaboresha huduma zake na mafao yanayotolewa ili kuweza kupata
wanachama zaidi. Waajiri mnapaswa kutoa
fursa kwa mifuko kujieleza mbele ya watumishi wapya kila mnapowaajiri ili
wafanye maamuzi sahihi kuhusu mfuko wanaotaka. Naomba kusiwe na upendeleo au mizengwe ya aina
yoyote katika eneo hili.
Aidha, wanachama mnaofaidi na mikopo ya LAPF kupita SACCOS zenu
muendelee kurejesha fedha husika kwa wakati na pia muwe na mipango madhubuti ya
kuitumia mikopo hiyo ili ionekane kuwa na manufaa kwenu na kuwaletea maendeleo.
Nashauri LAPF na Mifuko mingine muwaelimishe wanachama wenu jinsi ya kusimamia
mikopo hiyo ili iwe na tija kwao.
Mwisho napenda kuwashukuru tena kwa kunipa heshima hii na kuipongeza kwa
dhati Bodi ya Wadhamini na Uongozi wa LAPF kwa kazi yenu nzuri. Nasema endeleeni na kazi hiyo kwa manufaa ya
wanachama na Taifa kwa ujumla. Baada ya
kusema hayo machache sasa natamka kuwa mkutano wa sita wa Wadau wa LAPF mwaka
2013 umefunguliwa rasmi.
ASANTENI SANA
No comments:
Post a Comment