Monday, October 21, 2013

TTCL yapania kupambana na uhalifu kupitia mitandao.

 
 Afisa Mtendaji  Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Dkt. Kamugisha Kazaura akizungumza katika warsha ya saba ya mwaka ya Taasisi ya Mawasiliano ya Kusini Mwaafrika (SATA), ambapo wajumbe 60 walishiriki kujadilia mbinu zinazoweza kusaidia kuzuia wizi na udanganyifu unaofanywa mitandaoni jijini Dar es Salaam hivi karibuni
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Patrick Makungu (kushoto) akimsikiliza kwa makini  Afisa Mtendaji  Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Dkt. Kamugisha Kazaura mara baada ya kufungua warsha ya mwaka ya Taasisi ya Mawasiliano Kusini mwa Afrika (SATA) jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Patrick Makungu (kulia) akizungumza na Afisa Mtendaji  Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Dkt. Kamugisha Kazaura (katikati) mara baada ya kufungua warsha ya mwaka ya Taasisi ya Mawasiliano Kusini mwa Afrika (SATA). kushoto ni Ofisa Mkuu wa Ufundi TTCL, Bw. Jotham Lujara. Mkutano huo ulifanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
=======  =======  ==========
TTCL yapania kupambana na uhalifu kupitia mitandao.

Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) imejidhatiti  kupambana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao ili kuwakikishia wateja wake huduma bora na pia kukuza uchumi wa nchi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Dkt. Kamugisha Kazaura ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa warsha ya watalaamu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)iliyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni.

Dr Kamuzora alisema kuwa TTCL ina vifaa vya kisasa kwa ajili ya ulinzi na mbinu za kukabiliana na wizi na udanganyifu katika mitandao hivyo kuwakikishia wateja wake huduma zenye bora.

“Tunalazimika kuwa na mbinu za ziada hata kama wahalifu wanaweza kuwa na utaalamu zaidi yetu”, alisema Dr. Kazura. Aliongeza kusema kuwa tatizo la wizi na udanganyifu kwa njia ya mtandao ni kubwa na linahitaji kuwepo kwa sera ya udhibiti ya matumizi ya mtandao wa ndani, nje na hata katika ngazi ya kimataifa. 

“Uhalifu wa mtandao ikiwemo wizi na udanganyifu ni tatizo ambalo hatupaswi kilidhrau, ni kama ugonjwa unaohitaji tiba”, alisema Dr. Kazaura. Alisema kuwa mkutano huo ulilenga kuja na mapendekezo ya kudhibiti tatizo hilo katika jumuiya. “Tumekutana kuzungumzia wizi na udanganyifu wa mitandaoni na usalama wa mitandao hii,” na mapendekezo yatakayo tolewa yatafikishwa kwenye mkutano wa Mawaziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknoloji wa jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

TTCL ni moja ya taasisi zinazotakiwa kuhakikisha tatizo hilo linapungua na kuisha kabisa kutokana na jukumu lake kubwa la kusimamia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa ambao kupitia kwake huduma za kimtandao zimeshaanza kutolewa ndani na nje ya nchi.  Alisema kuwa nchini Tanzania Mkongo wa Taifa umeboresha huduma za mawasiliano  na kusaidia kuboresha huduma za mawasiliano kwa kutumia mitandao mbalimbali ikiwemo ya intaneti.

Kupitia mitandoa hiyo watu hutuma na kupokea fedha,  pia hupata taarifa mbalimbali, sasa baadhi ya watu hutumia fursa ya kukua kwa tehama kufanya wizi na udanganifu huo mitandaoni. Kwa upande Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Patrick Makungu alisema kuwa warsha ya watalaamu hao ni muhimu na imekuja wakati muafaka na itasaidia kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo linalorudisha nyuma maendeleo katika sekta nyingi.

“Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika nchi za SADC na duniani kwa ujumla kuna tatizo la wizi na udanyanyifu unaofanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao”, alisema Profesa Makungu. Watalaamu hao walikutana chini ya Taasisi ya Mawasiliano Kusini mwa Afrika (SATA) katika warsha yake ya saba ambapo walijadili usalama wa mitandao dhidi ya wizi na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao.

Takwimu zinaonyesha kuwa watoa huduma za mawasiliano duniani kote wanapata hasara ya asilimia  8 hadi 13 ya mapato kutokana na wizi na udanganyifu huo. “Serikali ya Tanzania imeanza kuifanyia marekebisho sera ya mwaka 2003 ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano ili kuwa na sera itakayo saidia kuweka mifumo itakayozuia hali hiyo,”alisema Profesa Makungu.

Aliongeza kusema kuwa serikali itayapokea mapendekezo yatatolewa na mkutano huo na kuyafanyia kazi ili ya kuboresha sera hiyo ili kuwa na mifumo thabiti ya kuzuia watu kutumia vibaya mitandao. Akitoa mfano, alisema kwa sasa mitandao yetu ina picha na taarifa mbalimbali ambazo husababisha watoto kutokuwa na maadili yanayokubalika katika jamii zetu na kongeza kuwa wazazi washiriki kudhibiti watoto wao kutotumia mitandao vibaya ili wakue katika maadili mema.

Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Mtandao TTCL, Mhandisi Priscilla Chilipweli alisema tatizo la wizi na uganganyifu wa mtandaoni ni la siku nyingi tangu enzi za simu za mezani, hivyo kwa sasa hakuna budi kuwa na mifumo ya kuzuia na kuthibit tatizo hilo. “Kutokana na ukubwa wa tatizo hili hasa katika kipindi hiki ambacho sayansi na teknolojia imekua sana, nchi zetu hizi ikiwemo Tanzania tuwe na sera itakayo saidia kuweka mifumo bora zaidi ya kulikabili,” alisema Mhandisi Chilipweli. Akitoa mfano alisema nchini Tanzania mtu akikamatwa amefanya wizi au udanganyifu huwezi kumstaki kutokana na kukosekana kwa sheria maalumu ya kudhibiti jambo hilo.

Alisisitiza kuwa wataalamu katika idara na vitengo mbalimbali vya sekta ya umma na binafsi wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya kubaini kuwepo kwa matukio kama hayo ili wahusika wachukuliwe hatua. Warsha hiyo ya siku tatu ilihudhuriwa na wajumbe 60 wa jumuiya hiyo ya SADC na wawezeshaji kutoka Bara la Ulaya.

No comments: