Ndugu Wananchi;
Namshukuru
Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza
mwezi Septemba salama na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo kwa
sababu nilikuwa safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013. Awali nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho
wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada ya
kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee
baadhi ya mambo huenda itasaidia.
Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya mambo siyo kwa kuyapuuza, bali kwa
kuepuka hotuba kuwa ndefu mno.
Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.
Uhusiano
na Rwanda
Ndugu Wananchi;
Katika
hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai, nilizungumzia hali ya uhusiano wetu
na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la ujambazi na wahamiaji haramu katika Mikoa
ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi
kusema kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia moyo.
Tarehe
5 Septemba, 2013, nilikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Kampala .
Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu katika Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu
kuzungumzia uhusiano baina yetu na nchi zetu.
Mazungumzo yalikuwa mazuri na sote tulikubaliana kuwa yaliyopita si
ndwele tugange yajayo. Kwa sababu hiyo
tulielewana kuwa tutengeneze mazingira yatakayosaidia kutuliza hali na
kurudisha nchi zetu katika uhusiano mwema kama ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan wanasiasa, watumishi
wa umma, wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog na wananchi kwa ujumla
tusaidie kuimarisha uhusiano mwema baina ya Rwanda na Tanzania na watu wake.
Majambazi
na Wahamiaji Haramu
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba
hiyo pia nilisema kuwa tutachukua hatua thabiti dhidi ya majambazi na wageni wanaoishi
nchini bila ya kuzingatia taratibu zinazohusika. Niliwataka majambazi wajisalimishe wao na
silaha zao kwa hiari. Wale wanaoishi
nchini bila ya kuwa na kibali halali wahalalishe ukaazi wao au warejee
makwao. Nilitoa siku 14 kuanzia tarehe 29 Agosti, 2013 wafanye hivyo kwani baada ya
hapo tungeanzisha operesheni maalum ya kushughulika na watu wa makundi yote
mawili.
Ndugu Wananchi;
Kumekuwepo
na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande
wa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng’ombe 8,000 waliondolewa na silaha 102 zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza tarehe 6
Septemba, 2013 na kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013, wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa makwao na
watuhumiwa 279 wa unyang’anyi wa
kutumia silaha walikamatwa. Aidha,
mabomu 10 ya kutupa kwa mkono
(offensive hand grenades), silaha 80,
risasi 780 na mitambo 2 ya kutengeneza magobole
vilikamatwa. Pia, ng’ombe 8,226 walikamatwa wakichungwa katika
mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao
ya misitu, mbao 2,105 zilikamatwa
pamoja na nyara mbalimbali za Serikali.
Ndugu Wananchi;
Agizo
la kuwataka watu wanaoishi nchini isivyo halali wahalalishe ukaazi wao au
waondoke kwa hiari au wataondolewa lilipotoshwa hasa na vyombo vya habari vya
nje ya Tanzania. Walikuwa wanadai eti Tanzania
ilikuwa inafukuza wakimbizi. Madai hayo si
ya kweli hata kidogo. Hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2013
wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye
Kambi ya Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna
mkimbizi ye yote aliyetakiwa kuondoka.
Ukweli ni kwamba hakuna mtu ye yote kati ya wale watu walioondoka kwa
hiari au kusaidiwa kuondoka wakati wa operesheni ambaye ni mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza kulalamika
wangekuwa wenzetu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri jambo hilo halikutokea.
Ndugu Wananchi;
Yalikuwepo
pia madai kwamba tunawaonea na kuwatesa watu walioishi nchini miaka mingi. Ati iweje sasa ndiyo waambiwe kuwa siyo
raia. Siku zote Serikali ilikuwa wapi? Uraia
haupatikani kwa kuishi nchi ya kigeni kwa miaka mingi. Unapatikana kwa kutimiza masharti ya kuomba
na kupewa uraia. Kama mtu hakufanya
hivyo anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au walikotoka wazazi wake. Ipo mifano ya watu mashuhuri ambao
walilazimika kuachia nyadhifa zao baada ya kugundulika kuwa siyo raia. Hawakuwa wanaonewa, ndiyo matakwa ya Katiba
na Sheria za nchi yetu.
Ndugu Wananchi;
Katika
kutekeleza operesheni hii niliagiza kuwa wale watu ambao wameishi hapa nchini miaka
mingi ambao wana nyumba, mashamba au mali mbalimbali au wameoa au kuolewa na wana
watoto au hata wajukuu waelekezwe kuhalalisha ukaazi wao. Iwapo watakataa kufanya hivyo basi wasaidiwe
kurejea kwao. Pia niliagiza watu
wasiporwe mali zao wala kudhulumiwa. Sijapata
taarifa ya kufanyika kinyume na maelekezo yangu. Lakini kama wapo watu waliotendewa tofauti,
taarifa itolewe kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili hatua
zipasazo zichukuliwe. Hatutaki watu
wadhulumiwe au kuonewa.
Napenda
kutumia nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Shamsi Vuai
Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi kwa uongozi
wao mzuri katika zoezi hili. Pia, nawapongeza
Makamanda na askari wa JWTZ na Polisi pamoja na maafisa wa Idara ya Uhamiaji,
Idara ya Mifugo, Idara ya Wanyamapori, Idara ya Misitu na Idara nyinginezo za
Serikali kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya.
Najua awamu ya kwanza imeisha tarehe 20 Septemba, 2013 na kama
nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa endelevu, muda si mrefu awamu ya
pili itafuata. Nawaomba waendelee
kuchapa kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu ya hali ya juu.
Ziara
ya Canada na Marekani
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe
17 na 28 Septemba, 2013 nilifanya ziara ya kikazi katika nchi za Canada
na Marekani. Nchini Canada nilitembelea
Chuo Kikuu cha Guelph ambapo nilitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu kwa
kutambua jitihada zetu tuzifanyazo kujiletea maendeleo na mafanikio ya kutia
moyo tunayoendelea kupata licha ya changamoto zinazotukabili. Katika mazungumzo yangu na uongozi wa chuo
hicho wamekubali kuwa na ushirikiano wa karibu na Wizara zinazohusika na Elimu,
Kilimo na Mifugo pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara hizo na
viongozi wa vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa.
Ndugu Wananchi;
Nchini
Marekani nilikutana na kuzungumza na maafisa na viongozi mbalimbali wa Serikali
ya nchi hiyo wakiwemo Rais Barack Obama na baadhi ya Wabunge wa Bunge la
Marekani. Mazungumzo yetu yalilenga
kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zetu na mambo yalienda vizuri. Wote walituhakikishia kuwa mambo
tuliyoyazungumza na kukubaliana na Rais Barack Obama wakati wa ziara yake
nchini yanaendelea kufanyiwa kazi.
Miongoni mwa hayo maombi yetu ya kupatiwa vitabu milioni 2.4 vya sayansi na hisabati yamekubaliwa na utekelezaji
umeanza. Upatikanaji wa vitabu hivyo utamwezesha
kila mwanafunzi wa sekondari kuwa na kitabu chake.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine kubwa
na la faraja kwetu ni kuwa mapendekezo yetu ya miradi ya umeme na barabara za
vijijini za kugharamiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lao la
Changamoto za Milenia yamepokelewa vizuri.
Kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa na Bodi ya MCC na kiasi gani
cha fedha kitatengwa na Bunge la Marekani kwa ajili hiyo.
Tuzo ya Uhifadhi
Jambo lingine
muhimu katika safari yangu ya Marekani ni kutunukiwa tuzo na “International
Congressional Conservation Foundation” kwa kutambua juhudi zetu katika
kuhifadhi wanyama pori
na mafanikio tuliyoyapata. Licha ya
changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo, tuzo hii imetupa moyo wa kuongeza
nguvu katika jitihada tunazozifanya sasa kupambana na ujangili na matatizo
mengine ya uhifadhi wa wanyama na misitu.
Ndugu Wananchi;
Kilichotupa
moyo zaidi ni kauli za utayari wa kutusaidia katika mapambano hayo zilizotolewa
wakati wa kupewa tuzo na katika mkutano wa mfuko wa Maendeleo wa Clinton na
katika mkutano maalum wa kupambana na ujangili na biashara ya meno ya tembo
duniani.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Ndugu Wananchi;
Shabaha kuu ya
safari yangu ya Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa 68 wa Umoja wa Mataifa unaoendelea
jijini New York mpaka Desemba, 2013.
Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu ni kuandaa agenda ya maendeleo baada ya
mwaka 2015 yaani: Post 2015 Development
Agenda: Setting the Stage. Kama
mtakavyokumbuka Malengo ya Milenia yaliyoamuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa mwaka 2000, yanafikia ukomo wa utekelezaji wake mwaka 2015.
Katika Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu mjadala umehusu nini kifanyike baada ya mwaka
2015. Hata hivyo, mjadala huo unaanza
kwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa yale Malengo Manane ya Milenia ya mwaka
2000 umefikia wapi mpaka sasa na utafikia wapi mwaka 2015 kwa kila nchi na kwa
dunia kwa ujumla. Tathmini ya jumla
inaonesha kuwa kumekuwepo na jitihada kubwa ya kutekeleza malengo haya katika
kila nchi. Yapo malengo ambayo
utekelezaji wake umefikia shabaha hivi sasa na yapo ambayo upo uwezekano wa
shabaha kufikiwa ifikapo mwaka 2015.
Vile vile yapo ambayo shabaha haitafikiwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande
wetu, Tanzania, tumefikia shabaha katika mambo yafuatayo:
(1)
Lengo la Milenia namba 2 kuhusu uandikishaji
wa watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;
(2)
Lengo la Milenia
namba 3 hasa kuhusu usawa wa kijinsia katika Shule za Msingi na Sekondari. Ukweli ni kwamba, wasichana wanaanza kuwa
wengi kuliko wavulana. Hatujafikia shabaha
kwa upande wa usawa wa kijinsia katika elimu ya juu na ni vigumu kulifikia
ifikapo 2015. Pia hatujafikia lengo kwa
upande wa usawa wa Wabunge wanawake na wanaume.
Hata hivyo, kwa kutumia mchakato wa Katiba unaoendelea sasa tunaweza
kufikia lengo katika uchaguzi wa 2015 iwapo tutaamua iwe hivyo;
(3)
Lengo la Milenia namba
4 kuhusu kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri chini
ya miaka mitano;
(4)
Tumefikia shabaha kwa
Lengo la Milenia Namba 6 kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na
(5)
Kwa upande wa lengo namba 7 kuhusu mazingira, tumefikia shabaha kwa upande wa
upatikanaji wa maji mijini. Bado tuko
nyuma kwa maji vijijini ingawaje tunaweza kufikia lengo ifikapo mwaka 2015 kama
tutaendeleza uwekezaji tulioamua kufanya katika bajeti ya mwaka huu. Lakini, hatutaweza kufikia shabaha kwa upande
wa usafi wa mazingira mijini na vijijini ifikapo mwaka 2015. Safari bado ndefu sana.
Ndugu Wananchi;
Malengo ya
Milenia namba 1 na namba 5 ambayo bado tuko nyuma sana ya shabaha hatutafikia
lengo ifikapo 2015. Tumeendelea
kutekeleza lengo la Milenia namba 1
kuhusu kupunguza umaskini na njaa kwa zaidi ya nusu kutoka kiwango cha mwaka
2000. Hatua tunazochukua kuleta mageuzi
katika kilimo zina lengo la kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza mapato
ya wakulima. Mafanikio yanaanza
kuonekana lakini si ya kiwango cha kutufikisha kwenye lengo ifikapo mwaka 2015. Tunao, pia, mpango wa kupanua programu ya
TASAF ya Conditional Cash Transfer
ili tuwafikie watu wengi maskini. Hata
kama tutafanikiwa kuutekeleza mapema mpango huu utatusogeza sana mbele lakini bado
tutakuwa chini ya lengo kwa upande wa kupunguza umaskini ifikapo 2015.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Lengo la Milenia namba 5, kuhusu afya ya kina mama
wajawazito bado tuko nyuma katika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na
kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungua chini ya uangalizi wa wataalamu wa
afya. Hatutaweza kufikia shabaha ifikapo
mwaka 2015. Mpango wa Maendeleo ya Afya
ya Msingi (2007 – 2017) una nia ya kukabiliana na matatizo haya. Tumeongeza ujenzi wa zahanati, vituo vya afya
na hospitali, tumeboresha upatikanaji wa dawa na tumepanua sana mafunzo ya
madaktari, wauguzi na wakunga mambo ambayo yamesaidia kutufikisha hatua
tuliyopiga mpaka sasa. Naamini juhudi zetu tukiziendeleza zitatusogeza mbele
zaidi ingawaje bado tutakuwa chini ya lengo.
Miaka michache ijayo, tatizo hili nalo litakuwa historia.
Ndugu Wananchi;
Lengo la
Milenia namba 8 linazihusu nchi tajiri kuongeza michango yao kusaidia nchi
zinazoendelea kutekeleza Malengo ya Milenia.
Bahati mbaya sana
mataifa tajiri hayajafikia viwango wanavyotarajiwa kutoa na hata vile
wanavyoahidi wenyewe kutoa katika majukwaa mbalimbali. Kama wangetimiza ahadi zao, sura ya
utekelezaji wa Malengo ya Milenia ingekuwa tofauti kabisa.
Ndugu Wananchi;
Hiyo ndiyo
hali ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia hapa nchini. Hakuna nchi ye yote duniani
iliyofanikiwa kutekeleza shabaha za malengo yote kwa ukamilifu. Ushauri wa viongozi wote waliozungumza
ulitaka mataifa yaliyoendelea yatimize ahadi zao za kuchangia utekelezaji wa
Malengo ya Milenia. Ilionekana suala la
upatikanaji wa fedha halina budi kuangaliwa kwa makini sasa na baada ya mwaka 2015. Bila ya hivyo ufanisi utakuwa mdogo katika kuongeza
kasi ya utekelezaji kwa pale paliposalia kufikia malengo ya 2015 na hata kwa
Malengo ya baada ya mwaka 2015.
Mashambulizi
ya Kigaidi ya Westgate, Nairobi
Ndugu Wananchi;
Wakati nikiwa
safarini, tarehe 21 Septemba, 2013
kulitokea shambulilizi la kigaidi katika Jengo la Biashara la Westgate, huko
Nairobi, Kenya. Watu 67 walipoteza maisha na zaidi ya 200 walijeruhiwa. Nilituma salamu za pole na rambirambi kwa Mheshimiwa
Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wa Kenya na kuwahakikishia kuwa tupo pamoja nao
katika wakati huu wa majonzi.
Nafahamu kuwa
baada ya tukio hilo watu wengi hapa nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama
wetu. Ni hofu ya msingi kwani tarehe 8
Agosti, 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu
zetu 11 wasio na hatia walipoteza
maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwafahamisha
kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, Serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo
vyetu vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali. Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku
hadi siku. JWTZ, Polisi na Idara ya
Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe
salama hadi sasa.
Baada ya tukio
la Kenya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Pamoja na kujizatiti kwetu huko hatuwezi
kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini. Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na
tajiri yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni
kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.
Hali kadhalika,
tumewataka watu wote wenye shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka,
maofisi, mahoteli, migahawa n.k. waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo
yao. Pia waangalie uwezekano wa kuweka
vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays).
Najua watu wanaweza kulalamikia usumbufu au gharama, lakini gharama na
hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.
Ndugu Wananchi;
Nawaomba
muendelee kufanya shughuli zenu bila ya hofu ingawaje msiache kuwa makini na
kuchukua tahadhari. Watu watoe taarifa
kwa vyombo vya usalama wanapoona mtu au watu au kitu cha kutilia shaka. Ni muhimu kwa usalama wake, wa kila mtu, jamii
na taifa. Maafisa husika wa vyombo vya
ulinzi na usalama wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za
tahadhari za kuchukua. Sisi Serikalini
tumejipanga kuchukua hatua zaidi kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu na
watu wake.
Mchakato
wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wananchi;
Baada ya Bunge
la Novemba, 2011 kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kulikuwepo na madai
ya kutaka sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya
upinzani na Chama tawala. Majadiliano
yalifanyika baina ya Serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho la asasi za kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho
yafanyike kwa awamu. Awamu ya kwanza
ihusishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho
yanayohusu Bunge Maalum na mwisho Kura ya Maoni.
Kama
ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, safari hii
nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao.
Yalifanyika mazungumzo kati yao na Serikali na maelewano kufikiwa kuhusu
maeneo ya kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha rasimu ya Muswada na
kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi;
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa
mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa
wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar.
Pili walishauri kwamba kama Bunge
Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90.
Maeneo mengine ya Muswada waliafikiana nayo.
Ndugu Wananchi;
Kwa
kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali ilifikisha Muswada kwa Spika wa
Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na
Utawala. Kama ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya
vikao na wadau na kupokea maoni yao kuhusu Muswada. Nimeambiwa kulikuwa na mjadala wa kina na
mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau. Kisha
hapo Wajumbe wa Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada walikuwepo pia Wabunge
ambao si Wajumbe wa Kamati walioshiriki kwa vile Kanuni zinaruhusu. Nimeambiwa pia kwamba mjadala ulikuwa mpana
na wa kina zaidi. Mapendekezo kadhaa
yalitolewa na Wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya Muswada.
Ndugu Wananchi;
Nimefahamishwa
kuwa Wabunge wa vyama vyote walichangia na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa
ugumu mawazo mazuri ya baadhi ya Wabunge wa upinzani yalisaidia kupata
ufumbuzi. Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe
wa Kamati na upande wa Serikali walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa
machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke Bungeni ili Wabunge nao wayajadili
na kuyapatia ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias
Chikawe aliwasilisha Muswada Bungeni.
Akafuatiwa na Mheshimiwa Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati.
Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa maoni yake.
Ndugu Zangu;
Baada ya watu
hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa Wabunge wangeanza kujadili
Muswada. Naambiwa mambo hayakuwa
hivyo. Badala yake kukazuka malumbano baina
ya Spika na baadhi ya Wabunge wa Upinzani wakitaka Muswada usijadiliwe. Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe
kwa kura ambapo ilishindwa. Katika hali
isiyotarajiwa, Wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa wawili. Kitendo hicho kimewanyima Wabunge wengi wa
upinzani fursa ya kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa
Kambi ya Upinzani. Pia wamejinyima
nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Wabunge
waliokuwepo waliendelea kuujadili Muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya
kuuboresha. Walifanya hivyo wakati wa
mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na
mengine yalikataliwa. Miongoni mwa
yaliyokubaliwa na Wabunge, kwa mfano, ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa
Mwenyekiti wa Bunge Maalum na lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Ndugu Wananchi;
Kwa maoni
yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza
kukubalika kama Wabunge wake wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa
kujadili na kupitisha Miswada Bungeni. Bahati
mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo yao. Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka
kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana. Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo
hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo. Kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za
kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe anavyotaka,
hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii. Naamini na wao
wanautambua ukweli huo.
Ndugu Wananchi;
Kuna msemo wa
wahenga kuwa “historia hujirudia”.
Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na
zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012. Kulipotokea mazingira kama haya pande zote
zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini
kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya
kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza
mzozo.
Ndugu Wananchi;
Kufanya
kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu. Tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa
ya lazima. Tukikataa kufanya hayo
Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu
sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna
dhamira nyingine iliyojificha?
Kama dhamira
yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria, ushauri wangu
na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na
mipango ya maandamano na kufanya ghasia.
Badala yake watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria
kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya taifa. Sisi katika Serikali tuko tayari.
Ndugu Wananchi;
Napenda pia
kuzisemea baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani. Kwanza
kabisa nasema kuwa nimesikitishwa sana na madai na tuhuma za uongo eti katika
uteuzi wa Tume ya Katiba sikuheshimu mapendekezo ya TEC, CCT na walemavu.
Ndugu Zangu,
Watanzania Wenzangu;
Siyo tu kauli hiyo
ya Mheshimiwa Tundu Lissu ni uzushi na uongo mtupu bali pia ni ya unafiki,
fitina na uzandiki wa hali ya juu.
Nasema hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema
yale kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya. Amesema yale kwa makusudi mazima ya kupotosha
ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wale Wajumbe 166 wa Bunge Maalum.
Napenda ieleweke
kuwa siishabikii kazi hiyo, lakini kwa kutimiza wajibu na maslahi ya taifa nikiagizwa
na Sheria za nchi nitafanya. Nasema
hivyo kwa sababu nafahamu ni kazi ngumu.
Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe 30
wa Tume haikuwa rahisi hata kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa ngumu zaidi. Ile
ya Tume ilikuwa ngumu kwa namna mbili. Kwanza,
kwamba taasisi zilizoomba na waombaji walikuwa wengi mno kuliko nafasi za
kujaza yaani 15 Zanzibar na 15 Bara. Zanzibar ziliomba taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa zaidi ya 200 wakati Bara kulikuwa na taasisi
zaidi ya 170 zikiwa na waombaji
zaidi ya 500. Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi
hicho si mtihani mdogo. Pili kwamba tulitakiwa
kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani watu wa nchi yetu kwa maeneo, vyama
vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu, wafanyakazi, wasomi, Wabunge,
Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara, wakulima, asasi za kiraia n.k.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na
changamoto hizo, lakini tulifanikiwa kuunda Tume iliyopokelewa vizuri na jamii
na kufanya watu wengi hata wale ambao hawakuteuliwa wahisi kuwakilishwa. Tulifanyaje? Kwanza kabisa tulihakikisha kuwa
tunapata wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye wawakilishi Bungeni na kwenye
Baraza la Wawakilishi na tunapata wawakilishi wa mashirika ya dini zetu kubwa yaani,
TEC, CCT na BAKWATA. Ndiyo maana
nikasema kuwa kwa Mheshimiwa Tundu Lisu kudai kuwa mapendekezo ya TEC na CCT
hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana usiokuwa na kichwa wala miguu.
Baada ya hapo
ndipo tukaangalia waombaji wa makundi na taasisi nyingine. Tulijitahidi sana kupata watu ambao
wanawakilisha kundi zaidi ya moja. Tulifikiria
hivyo kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si kila taasisi iliyoomba itapata mwakilishi
kwani hata tungependa iwe hivyo nafasi hazikuwepo. Kwa kutumia utaratibu huu makundi mengi yamepata
uwakilishi kutokana na watu waliopendekezwa na makundi mengi. Tumefanya kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo
na makundi ya maslahi mbalimbali nchini.
Ndiyo
maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana
na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa Bunge Maalum. Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu
ingefaa sana kama kungekuwepo na nafasi za kutosha kila kundi nchini. Hilo haliwezekani, labda tuwe na Bunge Maalum
lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
Ndugu Wananchi;
Mimi na Rais
wa Zanzibar tumekuwa tunajiuliza baada ya kazi ngumu na nzuri tuliyoifanya na iliyopongezwa
na wengi ya kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba nini kilichoharibika sasa hata tuonekane
hatuaminiki kuteua hawa 166? Kama ni kwa sababu za Mheshimiwa Tundu Lissu,
nimeshasema hazina ukweli wowote. Ninapojiuliza
kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu linaloingia akilini. Wakati mwingine nafikiria kuwa ni hiana. Lakini nadhani ni hila za kisiasa zenye nia ya
kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama chake. Kama hiyo ndiyo shabaha basi amekosea
sana.
Ndugu Zangu,
Watanzania Wenzangu;
Hatutengenezi Katiba
ya Chama fulani bali Katiba ya nchi, Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa
na vyama ambao ndiyo wengi kuliko wote. Lazima
tuongozwe na ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote. Lazima tukumbuke kuwa si watu wote
wanaostahili au kuwa na sifa ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa Wajumbe, hivyo
wale wachache watakao bahatika lazima wawasemee wote. Wanatakiwa kusikiliza na kuwakilisha mawazo
ya wote hata wale wasiokuwa wa Chama chao au kundi lao.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri hii
ndiyo sifa kubwa iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya
kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya
watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa ajili
hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki.
Tunataka watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalum nao waige mfano huu mzuri. Wajali maslahi mapana ya taifa letu na watu
wake badala ya kujali yale ya taasisi zao au makundi yao .
Ndugu Wanachi;
Nimeambiwa pia
kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo. Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika
Muswada. Hivyo basi napata tabu
kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi
wake nini! Labda kuna kitu sikuambiwa!
Nimeulizia
kuhusu hoja ya Kamati kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa
Zanzibar. Nimeambiwa kuwa Kanuni za
Bunge hazina sharti hilo hivyo Kamati haistahili kulaumiwa. Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili
lirudishwe Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo
watu wataendelea kulauminiana isivyostahili.
Hivyo basi, kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au
kususia vikao vya Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa.
Ndugu Wananchi;
Nimeambiwa pia
kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya Wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sababu ya idadi ya Wajumbe wa Tume kuwa sawa
inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi.
Ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili sauti za
pande zote zisikike sawia. Bunge Maalum lina
sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande
kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
Hivyo basi, katika Bunge Maalum nguvu si
uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu sawa wa
kura za kila upande peke yake. Huu ndiyo
msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa
lengo la kulinda maslahi ya Zanzibar.
Zanzibar ina Majimbo 50 ya
uchaguzi na Tanzania Bara ina Majimbo 189,
hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari watashindwa. Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao kutaka
kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa
na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja. Msingi unaotumika ni kutoa nguvu sawa
za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua masuala ya Katiba. Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako
sawa. Hakuna mdogo kumezwa na
mkubwa. Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika
kwenye Bunge Maalum hivyo hakuna kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe kutokukulingana. Nadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama Wabunge wataamua waongeze idadi itakuwa
kwa sababu nyingine siyo hii ya mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Katika
orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa Tume ya
Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi
rasimu ya pili kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa
mchakato. Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na
mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala. Limetokana na pendekezo la Mbunge
katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na Wabunge wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja
hii.
Nami
naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia
kufafanua mapendekezo ya Tume. Je
ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza
kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Naomba
nimalizie kwa kuwasihi viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kuongozwa na
hekima iliyotumika wakati tulipokuwa na tatizo linalofana na hili kuhusu Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Mimi naamini kama iliwezekana kufanikisha mambo wakati
ule inaweza kufanya hivyo hata safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka
salama salimini bila maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani. Kupanga ni kuchagua, naomba sote, mmoja mmoja
na kwa umoja wetu tuchague njia ya mazungumzo na maelewano kwani itaihakikishia
nchi yetu amani, usalama na utulivu. Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa
wema.
Mungu Ibariki Tanzania .
Nawashukuru
sana kwa
kunisikiliza.
4 comments:
Well said, Amani kwanza
hotuba ya mkuu wa nchi inapendeza na nzuri ya2pasa kuyafata maelekezo aliyoyyatoa kwa vyama vya sisa na makundi mengine ndani ya jamii
Mheshimiwa Rais umenena busara tupu. Wenye masikio watasikia. Mungu ibariki nchi yetu. Mungu dumisha amani ya nchi yetu.
Shukran Rais wetu kwa hotuba nzuri yenye busara na kuvutia,Allah akujaalie kila la kheri katika uongozi wako na ninamwomba Allah aijaalie amani nchi yetu.
Ameen.
Post a Comment