Miss utalii Tanzania 2013, Hadija Mswaga (kushoto) akiingia kwenye
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam jana, kuelekea Equatorial Guinea kuiwakilisha Tanzania katika
mashindano ya Dunia ya Miss Tourisim World 2013, pembeni ni mshindi wa
tatu, Teresia Kimolo. aliyemsindikiza (Picha na Hosea Joseph)
BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), limempa karipio kali Mwenyekiti wa
shindano la Miss Utalii, Gideon Chipungahelo kwa kosa la kudhalilisha
baadhi ya washiriki na malalamiko kufanyiwa kazi na Baraza hilo.
Karipio hilo lilitolewa baada ya Basata kupitia tathmini iliyohusisha
vipande vya matukio yaliyorekodiwa (clips) na kujionea namna wasichana
wanavyofanyiwa vitendo vya udhalilishaji na Chipungahelo kwa kipindi cha
kambi ya miezi mitatu.
Katika hafla ya upitiaji wa clips hizo uliofanyika mwishoni mwa wiki
katika Ukumbi wa Basata, Ilala, jijini Dar es Salaam mbele ya
Chipungahelo, ilionekana wazi wasichana kukosa uangalizi walipokuwa
kambini, hivyo kuwepo kwa matukio mbalimbali yasiyofaa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa kitengo cha Sanaa wa Basata,
Nsao Shaluwa alisema baada ya kupata malalamiko kuwa wasichana
wanafanyiwa mambo yasiyofaa wakiwa kambini, waliamua kuutafuta ukweli na
kujiridhisha shindano hilo lina ukakasi mwingi.
Alisema baada ya kukusanya baadhi ya matukio katika kuthibitisha hali
halisi iliyopo kwenye shindanohilo, watapeleka vielelezo kwa Waziri wa
Wizara ya Habari, Vijana Michezo na Utamaduni ili Chipungahelo ajadiliwe
kwa kosa la kudhalilisha warembo wa shindano hilo.
Alisema kwa kukosa matroni, yaelezwa warembo walikuwa wakizurula kutwa
nzima hadi usiku kwenye gari huku kukiwa hakuna ratiba ya chakula ya
kueleweka huku wakifanyishwa mazoezi muda mrefu.
Mbali ya muda mrefu kuanzia saa 2 usiku hadi 9, pia walikuwa wakivaa
viatu virefu, hivyo miguu kuvimba na wakati mwingine walikuwa wakichapwa
makofi na kulazimishwa mapenzi.
Aidha, Chipungahelo anakabiliwa na shutuma ya kuwaweka mabini washiriki
kwa muda wa miezi mitatu tofauti na alivyoeleza Basata kuwa kambi ni ya
wiki tatu.
Zaidi ya hapo, Chipungahelo alishindwa kutoa zawadi kwa washindi wala
kifuta jasho kwa washiriki wengine huku mshindi wa mwaka 2013, akidaiwa
kubebwa kwa hila.
Shaluwa alisema baada ya malalamiko hayo kufikishwa kwao, waliamua
kunyatia katika kambi yake iliyokuwa na warembo saba ambayo pia
Chipungahelo aliwaficha.
Baada ya kuwahoji washiriki, walikiri kwamba walikuwa wakilala warembo
saba, wengine watano katika chumba kimoja na wengine wakilala chini huku
wakila mlo mmoja tena katika muda usiofaa.
“Warembo wengi wamekiri walikuwa wakifanyishwa mazoezi kwa muda mrefu huku wakiwa wamevaa viatu virefu,“Tulikuwa tukifanyishwa mazoezi kuanzia saa mbili usiku hadi saa tisa,
tuna njaa na tulipolalamika, baba alitutukana matuzi ya nguoni na
kukashifu tupu zetu” mmoja wsa warembo alisema katika CD ya Basata.
Shaluwa anasema walipofika Ikondolelo ambako kulikuwa na kambi ya awali,
walizungumza na warembo hao, lakini wakishindwa kusema ukweli mbele ya
Chipungahelo.
Alisema walipowapa karatasi kuandika kero zao, kila mtu aliandika jina
na kusaini ambapo walieleza mengi yaliyorekodiwa na wadau kuoneshwa
mwishoni mwa wiki mbele ya mwanasheria Ashura Mzava kutoka TAWLA.
Mzava alisema wazi kwa madudu yaliyopo kwenye shindano hilo, Chipungahelo anapaswa kushtakiwa kwa udhalilishaji.
Kashfa nyingine ni kitendo cha Chipungahelo kutumia kiasi cha sh 200,000
ambazo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya Tanga Mjini, Halima Dendego ili
washiriki waende saloon kabla ya fainali.
“Baba ametunyanyasa sana hadi, ametumia pesa tuliyopewa na mama Halima
Dendego, lakini hapohapo amekuwa akimpendelea mshiriki mwenzetu (jina
tunalo), kwa vile alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi,” alisema mmoja
wa washiriki na kuongeza:
“Hata siku ile ya fainali, alipokuja mpambaji kutoka Sofia Record,
alimuita na kumvalisha nguo nzuri pamoja na kumpamba tofauti na
alivyovalisha washiriki wengine” wamesema washiriki hao.
Wakati huohuo Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa kutoka Wizarani, Leah
Kihimbi alisema atalifikisha kwa usahihi suala hilo katika ngazi ya juu
akimtaka Chipungahelo ajitayarishe kwa maamuzi yoyote.
Mshiriki pekee wa Miss Utalii 2013 aliyefika kwenye tahmini hiyo, ni
Glory John aliyesema wazi shutuma zote zilizoelezwa na wenzake dhidi ya
Cipungahelo ni kweli.
“Tulipokuwa tunakwenda Mikumi , tulilala Morogoro, Baba (Chipungahelo)
aliniita akaniambia nipande juu katika chumba kimojawapo, nilipokwenda
na kufungua mlango, nikakutana na moshi wa ajabu nikashindwa kuvumilia
nikatoka.
Akanifuata akinitaka nirudi chmbani mle, nikagoma, nilipowaeleza
wenzangu, walinieleza nilielekea kunaswa kwenye mtego wake,” alisema
Glory.
Naye Katibu Mtendaji BASATA Godfrey Mngereza alisema, hilo ni suala
nyeti linalogusa jinsia ya kike, hivyo ni hatari kwa ustawi wa jamii.
Kupitia tathmini hiyo ya aina yake, Basata itachunguza mazingira ya
ushindi wa Miss Utalii mwaka 2013, ikibainika hakustahili, atavuliwa
taji hilo ili iwe fundisho.
“Tabia hizi chafu zinatuchafua hata sisi BASATA tunaonekana hatufanyi
kazi sasa ndio tutaanza na Miss Utalii na ikibidi kusiwe na shindano la
aina yeyote kama mambo yenyewe ni kudhalilishana,” alisema Mngereza.
Wadau wengine waliohudhuria tathmini hiyo ni kutoka TAMWA,
TAWLA,TGNP,THAWE, Polisi Jamii, Polisi kutoka kituo cha Pangani Ilala,
Dar es Salaam, Shirikisho la Sanaa na Ufundi, Binti Leo na wengineo.
Shaluwa alisema suala hilo litapelekwa ngazi za juu na vielelezo
kuonesha wasichana wakieleza yanayotokea kambini pamoja na maoni ya
wadau yaliyorekodiwa.
Akizungumnzia tuhuma dhidi yake, Chipungahelo alisema ni majungu
yaliyopikwa na maadui zake ambao walimpandikizia makahaba kwa lengo la
kuchafua taswira ya shindano hilo ili kummaliza, lakini aliomba radhi kwa dosari na mapungufu yaliyojitokeza na kuahidi kuwa hazitajirudia tena.
No comments:
Post a Comment