Thursday, August 1, 2013

MAMA SALMA KIKWETE AHUDHURIA NA KUFUNGA RASMI MKUTANO WA HIGH LEVEL GROUP HUKO BOTSWANA

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akikaribishwa rasmi kwenye mkutano wa "High Level Group" na Dr. Sheila Tlou, Mkurugenzi wa UNAIDS Regional Support Team kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika katika siku ya pili ya mkutano huo unaofanyika jijini Gaberone nchini Botswana tarehe 31.7.2013.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano wakisoma jarida linalochapishwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, huku wakiendelea na mkutano.
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo Mama Salma Kikwete akifunga rasmi mkutano wa High Level Group uliokuwa unafanyika kwenye hoteli ya Lasmore nchini Botswana tarehe 31.7.2013.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifanya mazungumzo na Profesa Alaphia Wright, Mwakilishi wa UNESCO kwenye nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika mwishoni mwa mkutano wa siku mbli wa High Level Group ulikuwa ukifanyika jijini Gaberone nchini Botswana tarehe 31.7.2013.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimsikiliza kwa makini Dr. Patricia Machawira, Mshauri wa HIV na AIDS kwa nchi za ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika mwishoni mwa mkutano wa siku mbili uliokuwa unafanyika nchini Botswana. Dr. Machawira alikuwa akimshukuru Mama Salma kwa ushiriki wake kwenye mkutano huo uliofanyika tarehe 30.7 hadi 31.7.3013.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akihojiwa na na MS Sandra Chuma kutoka kwenye sekretarieti ya High Level Group, kuhusu masuala mbalimbali yanayowakabili wanafunzi yanayohusiana na elimu na afya, mwishoni mwa mkutano.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiagwa rasmi na Mwakilishi wa UNESCO wa Kanda ya Kusini mwa Afrika Profesa Alaphia Wright nje ya hoteli ya Lasmore huko Gaberone nchini Botswana ulikofanyika mkutano wa siku mbili wa High Level Group kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kuhusiana na elimu na afya kwa vijana. PICHA NA JOHN LUKUWI.

Na Anna Nkinda- Gaborone, Botswana

Imeelezwa kuwa watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za udhalilishaji na unyanyasaji wa jinsia, ukosefu wa elimu, utaalamu na huduma zitakazowasaidia kukaa shuleni , kujikinga na mimba za utotoni ,ugonjwa wa Ukimwi na virusi vinavyosababisha kansa ya shingo ya kizazi.

Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifunga mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika Hoteli ya Lansmore Masa Square iliyopo mjini Gabarone nchini Botswana.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema ingawa upatikanaji wa huduma na mahitaji ya vijana ni madogo katika nchi nyingi za kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika bado kuna tofauti kubwa ya utolewaji wa huduma hizo kwa vijana wa kike ukilinganisha na wa kiume ambao wao wanapata zaidi.

Alisema kwa kufanya kazi kwa pamoja kati ya mashirika yanayofanya kazi chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika ya kijamii wanaweza kutambua mahitaji na changamoto zinazowakabili vijana na kuwaomba wakati wanakusanya maoni wawashirikishe viongozi na jamii nzima.

“Tunachotakiwa kufanya kama wanakamati ni kutumia muda tuliopewa kusoma ripoti yote na kuielewa kisha kuwashirika wadau mbalimbali wa wa maendeleo ili waweze kujadili ripoti hii na kutoa maoni yao”, alisema Mama Kikwete.

Akimkaribisha Mama Kikwete kufunga mkutano huo Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) Prof. Sheila Tlou alimshukuru kwa kukubali kwake kuwa mmoja wa wanakamati kwani yeye ni kinara kati ya wake wa marais wa Afrika katika suala zima la kupambana na ugonjwa wa Ukimwi na kumsadia mtoto wa kike.

Alisema kuwa miaka ya nyuma Umoja wa Mataifa (UN) ilikuwa inafanya kazi na kila mtu aliyekuwa na mamalaka lakini hivi mashirika yote yaliyopo chini ya UN yanafanya kazi kwa ushirikiano na hivyo kuzisaidia nchi husika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“Kwangu mimi hii ni historia kwani mpango kazi wa Maputo (Maputo Plan of Action) na makubaliano haya ya leo yatasaidia kushughulikia utolewaji wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kwani jambo hili linatakiwa kuangaliwa kwa umakini zaidi hakika tutafanya kitu katika jamii yetu kwakuwa vijana wanakabiliwa na matatizo mengi ndani ya nchi zetu”, alisema Prof. Tlou.

Akisoma taarifa ya makubaliano ya kamati hiyo Afisa Programu kutoka UNESCO Dhianaraj Chetty alisema kuwa kabla ya kuandaa ripoti hiyo walikusanya mawazo ya wadau mbalimbali kutoka nchi 21na kuandika ripoti kuhusu Vijana wa leo wako tayari kwa kesho? na kuangalia matatizo yanayowakabili na kugundua mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa upatikanaji wa elimu.

Pia katika ripoti hiyo kamati iliangalia kiwango cha uelewa wa maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi kwa baadhi ya nchi wanachama na faida za utoaji wa huduma kwa vijana wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).

“Uelewa wa ugonjwa wa Ukimwi kwa vijana ni chini ya asilimia 40, wasichana wanahangaika kupata na kumaliza elimu ya Sekondari, na kati ya wasichana 52 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 wanapata maambukizi mapya ya Ukimwi kwa kila saa moja katika kanda.

Kuna idadi kubwa ya upatikanaji wa mimba zisizohitajika na utoaji mimba usio salama, hii ni changamoto ya dharula ambayo inatufanya sote kuangalia jinsi gani tutapata nafasi ili tuweze kubadilisha na hali hii leo na siku za baadaye”, alisema Chetty.

Makubaliano hayo yanaangalia kazi ambazo wanachama wa SADC na EAC wanafanya ili kuangalia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana yatapelekwa kwa wadau wote, vijana na mawaziri wa wizara za Afya na Elimu na kutoa mawazo yao kuanzia mwezi wa nane hadi wa kumi mwaka huu.

Mwezi wa kumi na mbili kamati hiyo itakutana kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa ya zinaa ambao utafanyika mjini Cape town nchini Afrika ya Kusini na kupitisha makubaliano hayo (document) kisha yatasainiwa na mawaziri husika katika mkutano huo ambayo itakuwa ni sehemu ya utekelezaji kwa nchi.

Mkutano huo wa siku mbili uliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) , UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lengo kuu likiwa ni kuhakikisha kuwa vijana wote wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia jambo ambalo litawasaidia waweze kufahamu zaidi ugonjwa Ukimwi.

No comments: