Pichani ni walinzi wa Amani wakiwa katika moja ya doria kwenye mitaa ya mji wa Goma, mwanzoni mwa wiki hii kumetokea mapingano katika eneo la vilima vya Kibati Magharibi ya Kivu ambapo kundi la waasi la M23 lilishambulia walinzi wa amani wa Misheni ya Kutuliza Amani katika DRC ( MONUSCO) waliokuwa katika Operesheni ya kulinda raia wakishirikiana na Majeshi ya Serikali ya DRC. Shambulio hilo limesababisha mwanajeshi Mtanzania kupoteza maisha na wengine 10 wakiwamo wanajeshi wa Afrika ya Kusini wamejeruhiwa. Tukio la kushambuliwa kwa walinzi hao limelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ban Ki Moon na Baraza Kuu wametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na familia za wale waliojeruhiwa na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika ya Kusini. Aidha Baraza Kuu limesisitiza kwamba vitendo vinavyolenga kudhoofisha mamlaka ya MONUSCO havitavumiliwa.
Na Mwandishi Maalum
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amelaani kuuawa kwa Mlinzi wa Amani kutoka Tanzania ambapo wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya kushambuliwa na kundi la waasi la M23 katika katika eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaii wa Katibu Mkuu , inaeleza kwamba. “ Katibu Mkuu analaani kwa nguvu zote mauaji ya mlinzi huyo na kujeruhiwa kwa walinzi wengine 10 na anatoa salamu zake za rambirambi kwa familia za walinzi hao na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika ya kusini”.
Mashambulizi dhidi ya walinzi hao wa Amani yametokea siku ya jumatano katika Vilima vya Kibati Magharibi ya Kivu ambako Misheni ya kutuliza Amani ya Umoja wa Mataifa katika DRC ( MONUSCO) ilikuwa ikisaidiana na majeshi ya serikali ya DRC kuwalinda raia katika eneo la Goma ambalo lina idadi kubwa ya watu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, MONUSCO ilijibu mashambulizi hayo kwa kutumia zana mbalimbali za kivita yakiwamo makombora, mizinga na helkopta za kivita wakati majeshi ya DRC yalitumia askari wa ardhini, vifaru na helkopta za kivita na kwamba operesheni hiyo bado inaendelea.
Taarifa inaeleza zaidi kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kuwajibika na kuhakikisha inachukua hatua zote muhimu kwa kuzingatia Azimio namba 2094 ( 2013) la Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linasisitiza ulinzi wa raia katika eneo hilo la Mashariki ya Kongo.
Wakati huo huo , wakati mapigano yakiendelea, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika kikao chake kilichofanyika siku ya Alhamisi nalo limetoa tamko la kulaani vikali tukio la kuuawa kwa mlinzi wa Amani wa Tanzania, na kutoa salamu zako za pole kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na familia ya marehemu pamja na wale waliojeruhiwa.
Tamko la Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limetolewa taarifa hiyo baada ya Baraza hilo kupokea taarifa rasmi iliyowasilishwa na Naibu Mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani, Bw. Edmond Mulet kuhusu kinachoendelea katika DRC.
Baraza pia limelaani kwa nvugu zote dhidi ya kujirudia rudia kwa matukio yanayofanywa na M23 yanayolenga MONUSCO na rais yakuwalenga raia na MONUSCO.
Na kwa sababu hiyo Baraza Kuu la Usalama limetaka mamlaka ya DRC kuchunguza tukio la kuuawa kwa mlinzi huyo wa Amani na kisha kuwafikisha mbele ya sheria watakaobainika kuhusika na tukio hilo.
Aidha Baraza Kuu limerejea tena tamko lake la kuitaka M23 na makundi mengine yenye silaha katika DRC kuacha aina zote za machafuko na kuweka chini silaha zao. Na kwamba, halitasita kupitisha vikwazo vya nyongeza kwa yeyeyote yule ambaye atabainika kujihusisha na fujo na machafuko na kwamba vikwazo hivyo vitahusu pia silaha.
Aidha wajumbe 15 wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limeipongeza MONUSCO kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza mamlaka yake na hususani ya kuwalinda raia na limeitaka na kuihimiza MONUSCO kuendelea na wajibu wake huo huku lilikisisitiza kwamba Baraza Kuu la Usalama halitavumilia kitendo chochote kinacholenga kudhoofisha mamlaka ya MONUSCO.
Vilevile Baraza limeitaka Expanded Joint Verification Mechanism ( EJVM) kuchunguza madai ya kuwapo kwa vitendo vya urushwaji wa makombora kuelekea nchi ya jirani ya Rwanda
Katika hatua nyingine , Muwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu katika DRC. Bw. Martin Koble naye ameelezea kusikitishwa kwake na tukio hilo la kuuawa kwa mlinzi wa Amani wa Tanzania.
Akielezea masikitiko yake, Bw. Martin Koble anasema, “ mlinzi huyo wa Amani ameyatoa muhanga maisha yake ili kuwalinda wananchi wa Goma. Ninaungana na familia ya marehemu na walinzi wenzake katika kombania yake katika kipindi hiki cha majonzi na wakati mgumu”.
Katika mwaka mmoja uliopita, kundi la waasi la M23 pamoja na makundi mengine yenye silaha mara kwa mara yamekuwa yakipambana na Jeshi la Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( FARD). Ambapo Mwezi Novemba mwaka jana kundi hilo la M23 lilichukua kwa muda mji wa Goma.
Machi 28 mwaka huu , Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha azimio la kuanzishwa kwa Brigedi Maalum ( FIB) iliyopewa mamlaka ya kuyadhibiti makundi ya waasi yenye silaha yenyewe kama FIB na au kwa kushirikiana na Majeshi ya serikali ya DRC ( FARD).
Kupitia azimio hilo Baraza Kuu la Usalama lilitoa wito kwa kundi la M23 kusitisha mara moja aina zote za machafuko ikiwa ni pamoja na kuweka chini silaha zao.
Aidha kwa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuimarisha mamlaka ya MONUSCO pamoja na kuundwa kwa FIB kumelenga katika kusaidia utekelezaji wa malengo ya Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa kuhusu Amani, usalama na maendeleo katika DRC na eneo la Maziwa Makuu.
No comments:
Post a Comment