[Limetolewa kwa mujibu wa Kanuni 53(1) na (2) ya
Kanuni
za
Kudumu za Bunge 2013]
_____________
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 17 - 27 Julai, 2013 ulifanyika Mkutano wa 44 wa Chama cha
Mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola Afrika [Commonwealth Parliamentary Association (CPA)] uliofanyika Windhoek,
Namibia na Bunge letu liliwakilishwa na Wabunge wafuatao:-
1.
Mhe. Anne Semamba Makinda, Mb, - Spika;
2.
Mhe. Mussa Azzan Zungu, Mb. - Mwenyekiti wa CPA Tawi la Tanzania;
3.
Mhe. Beatrice Matumbo Shellukindo, Mb - Makamu Mwenyekiti wa CWP Kanda
ya Afrika Mashariki;
4.
Mhe. Kabwe Zubeir Zitto, Mb. – Mwakilishi wa Tawi na Mjumbe Kamati ya
Mipango na Fedha;
5.
Mhe. Magalle John Shibuda, Mb;
6.
Mhe. Dkt Maua Abeid Daftari, Mb;
7.
Mhe. Magdalena Hamis Sakaya, Mb; na
8.
Mhe. Mhonga Said Ruhwanya, Mb.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine, katika Mkutano huo ambao lengo lake kuu
lilikuwa ni kujadiliana na kuona namna gani nchi wanachama wanaweza kutumia
umoja wao katika kutatua migogoro, pamoja na kustawisha maendeleo ya kiuchumi
Barani Afrika, [Utilizing our
Commonwealth partnership to promote Conflict Resolution and Econimic
Development on the African Continent] kulikuwa na jukumu kubwa na zito la
kumchagua Rais wa chama hiki atakayekuwa kiongozi wa nchi 19 na matawi 45 ya Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua uwezo na sifa za viongozi wa Tanzania, Tawi la CPA
Tanzania lilipendekeza jina na Mheshimiwa Anne S. Makinda (Mb), Spika kuwa
mgombea wa nafasi hii, kwa kuamini kuwa ni mwadilifu, mwenye uzoefu wa
kutosha na mchapakazi, na hivyo kuwa na sifa stahiki za
kugombea nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada mbalimbali zinazofanywa siku zote na Rais wetu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho kikwete za kuitangaza nchi yetu
kimataifa, zilisaidia sana katika mchakato wa kumnadi mgombea wetu kwa wajumbe
wa mkutano ambao ndio walikuwa wapiga kura katika uchaguzi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika uchaguzi huo Mhe Anne Semamba Makinda, Mb alichaguliwa kwa
kishindo kuwa Rais wa CPA Kanda ya
Afrika kwa muda wa mwaka mmoja, jambo ambalo limeiletea nchi yetu
heshima na sifa kubwa kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua jambo hili, natumia
fursa hii kuliomba Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi kuridhia Azimio
la Kumpongeza Mhe Spika kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa CPA Kanda ya Afrika kama
ifuatavyo:-
KWA KUWA, Bunge la Tanzania ni
Mwanachana wa Umoja wa Kibunge wa Jumuiya ya Madola [the Commonwealth Parliamentary Association] kwa muda mrefu sasa na
imekuwa ikishiriki kikamilifu shughuli za Umoja huo na kutoa fursa sawa za
uwakilishi kwa raia wake wote bila
kujali jinsia jambo ambalo limewezesha wanawake wengi kushika nyadhifa
mbalimbali za uongozi Kitaifa na Kimataifa;
NA KWA KUWA, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonyesha jitihada mbalimbali
za kuitangaza nchi nyetu kimataifa jambo ambalo limewezesha fursa nyingi
kupatikana;
NA KWA KUWA, katika Mkutano wa 44 wa CPA- Afrika uliofanyika Windhoek, Namibia, Mhe.
Anne S. Makinda (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
alichaguliwa kuwa Rais wa CPA Kanda ya Afrika;
NA KWA KUWA, Mheshimiwa Spika, ana uzoefu wa kutosha katika medani za siasa na
uongozi kwa zaidi ya miaka 37, kwa kushika nyadhifa mbalimbali kama vile kuwa
Naibu Spika na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Ardhi , Maliasili na Mazingira, Mwenyekiti wa Bunge, Waziri
katika Wizara Mbalimbali, Makamu mwenyekiti wa SADC-PF nk jambo ambalo
linaondoa shaka ya aina yoyote juu ya uwezo wake;
HIVYO BASI, Bunge hili katika Mkutano wake wa Kumi na Mbili linaazimia kumpongeza
Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne
Semamba Makinda (Mb) kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mabunge ya nchi wanachama
wa Jumuiya ya Madola, (Commonwealth
Parliamentary Association) kanda ya Afrika, na kwamba linamtakia kila la
kheri Mheshimiwa Spika katika kutekeleza majukumu yake haya mapya na mazito kwa
kuongoza nchi 19 na matawi 45 Afrika nzima.
Naomba
kutoa hoja.
Mussa Azzan Zungu, MB.
MWENYEKITI
WA CPA - TANZANIA
No comments:
Post a Comment