Tuesday, May 7, 2013

TANZANIA YAHADHARISHA WACHACHE KUAMUA KWA NIABA YA WENGI

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,Balozi Tuvako Manongi.

Na Mwandishi Maalum

Tanzania imesisitiza na kutamka bayana kwamba, majadiliano yoyote yanayohusu maslahi ya wengi ni lazima yajadiliwe kwa uwazi, ukweli na yawe shirikishi ili kuepusha misuguano na migongano isiyokuwa ya lazima.

Kauli hiyo imetolewa siku ya jumatatu na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi, alipokuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya mkutano wa Kamati ya Tano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, inayosimamia masuala ya Utawala na Bajeti.

Kamati hiyo ya Tano inajadili pamoja na mambo mengine, bajeti za Misheni za kulinda Amani za Umoja wa Mataifa inayokadiriwa kuwa takribani dola za kimarekani Bilioni 8. Bajeti hiyo ni kwa kipindi cha Julai 2013 hadi June 2014.

Balozi Manongi ameeleza wasi wasi wake kuhusu tabia inayotaka kujengeka kwa baadhi ya nchi chache kuamua kukutana kivyao vyao na kupitisha maamuzi na kuzilazimisha nchi nyingine zikubaliane na maaamuzi hayo.

Akabainisha kwamba mwenendo huo ni kinyume na taratibu za Umoja wa Mataifa zinazotaka na kusisitiza majadiliano ya kiserikali baina ya nchi wanachama katika kila suala muhimu linalogusa maslahi ya wengi.

Akasema Manongi, “ Ujumbe wangu unaungana na unapenda kurejea kauli iliyotolewa na Kundi ya Nchi za Afrika kuja kwako Mwenyekiti na kupitia kwako kwenda kwa Bureau. Kwamba, majadiliano na upitishaji wa maamuzi ni lazima yafanyike katika misingi ya uwazi na yawe shirikishi”

Na kuongeza “ Ujumbe wangu unapenda kutahadharisha kuhusu maamuzi yanayofikiwa kupitia kikundi kidogo. Tabia hii imeonyesha udhaifu na wakati mwingine imesababisha mkanganyiko na kutoaminiana miongoni mwa wanachama.”

Akasisitiza kwamba ifike mahali ambapo wajumbe waachane na mazoea yoyote yenye mwelekeo wa kudhoofisha asili na kiini cha mikachato ya kiserikali inayosimamia majadiliano.

Akizungumzia ajenda ambazo zipo mbele ya Kamati hiyo, Balozi Tuvako Manongi, amesema Tanzania itafuatilia kwa karibu majadiliano ya ajenda zote muhimu zilizo mbele ya Kamati hiyo.

Ajenda ambazo ujumbe wa Tanzania utazipa kipaumbele ni Ripoti wa Bodi ya Wakaguzi, Upanuzi wa dhamana na mamlaka ya Misheni ya Kutuliza Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO), Utoaji wa fedha kwa Misheni ya Umoja wa Mataifa katika Somalia, (AMISOMI), Misheni ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika inayolinda Amani katika jimbo la Darfur ( UNAMID), na ujio wa Misheni mpya ya kulinda amani huko Mali ( MINUSMA).

Akizungumzia kuhusu operesheni za kulinda Amani, Mwakilishi huyo, amesema uaminifu wa Umoja wa Mataifa, unategemea pamoja na mambo mengine, uwezo wake katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwa ni pamoja na uwezeshwaji wa wale waliodhaminiwa kutekeleza operesheni za ulinzi wa Amani.

Akasema haitoshi kuwataka walinzi wa amani kuwajibika kwa mujibu wa dhamana za Misheni zao ili hali hawawezeshwi kutekeleza wajibu wao kwa ukamilifu.

Na kwa sababu hiyo na hasa katika mazingira ya sasa ambapo kumekuwapo na upungufu mkubwa wa rasilimali, ni vema jitihada zaidi zikafanyika za kuziongezea rasilimali Misheni za kulinda amani badala ya kuzipunguzia.

No comments: