Monday, May 6, 2013

EU yaahidi kusaidia Bajeti ya Tanzania Dola milioni 562


Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Mh. Filiberto Sebregondi (katikati) akiwaeleza waandishi wa habari(hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam juu ya Wiki ya Umoja wa Ulaya itakayoadhimishwa nchini na kuhusisha shughuli mbalimbali za kijamii. Wengine katika picha ni Balozi wa Hispani nchini Mh. Luis Cuesta Civis(wa kwanza kushoto) , Balozi wa Ireland nchini Mh. Fionnula Gilsenan na ,Balozi wa Nethrland nchini Mh. Dkt. Ad Koekkoek Emmanuel . Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO_Dar es salaam

UMOJA wa Nchi za Ulaya (EU) umeahidi kuendelea kusaidia Tanzania katika miradi ya maendeleo, ambapo kwa mwaka ujao wa fedha wa 2013/2014 itaipatia Tanzania zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 562.

Kauli hiyo imetolewa leo na Balozi wa EU nchini Tanzania Mh. Filiberto Sebregondi jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya Wiki ya Umoja wa Ulaya itakayoadhimishwa nchini na kuhusisha shughuli mbalimbali za kijamii.

Mh. Sebregondi alisema kuwa fedha hizo zitatolewa na nchi washirika wa maendeleo zikiwemo nchi zilizoko nje ya bara la Ulaya na kwamba zitatolewa kwa ajili ya kusaidia bajeti ya Tanzania.

Balozi Sebregondi alizitaja shughuli zitakazofanyika katika kuadhimisha wiki hiyo kuwa ni pamoja na kutiliana saini makubaliano ya mkataba kati ya EU na Wizara ya Fedha kwa niaba ya serikali ya Tanzania.

Shughuli ngingine zitakazofanyika ni semina kwa waandishi wa habari kuhusu haki za binadamu, siku ya utamaduni wa nchi za umoja ulaya, ambapo shughuli zote zinalenga kuimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Nchi za Ulaya.

Balozi huyo aliendelea kusema kuwa mkataba utakaosainiwa utaiwezesha Tanzania kupata fedha kwa ajili ya kusaidia sekta ya kilimo cha miwa, chai na kahawa kinachotekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Naye Balozi wa Dernmark nchini Mh.John Flento alibainisha kuwa uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Nchi za Ulaya ni mzuri na lengo kubwa la umoja huo ni kusaidia juhudi za serikali za kuondoa umasikini,hivyo jambo la muhimu ni uhusiano uliopo kuimarishwa zaidi.

Aliongeza kuwa serikali ya Tanzania ina mikakati mizuri katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake na umoja huo umekuwa ukiunga mkono juhudi hizo kwa kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali katika kufanikisha miradi mbalimbali inayofadhiliwa na umoja huo nchini.

Kwa upande wake Muambata wa Kijeshi wa Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Ulaya (CDR) Benjamin Chauvet ,anayesimamia Jeshi la Maji kanda ya Tanzania na Kenya, amesema kuwa matukio ya uharamia yamepungua kutoka matukio 200 kwa mwaka 2012 hadi chini ya 10 kwa mwaka 2013.

Aliongeza kuwa juhudi zaidi zinahitajika ili kupambana na Uharamia katika eneo la pembe ya Afrika ambapo umoja wa ulaya umejikita katika kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama kwa kuondoa kabisa tatizo hilo.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukifadhili miradi mbali mbali nchini katika huduma za kijamii na kiuchumi katika sekta za Miundombinu ya usafiri ikiwemo ujenzi wa viwanjwa vya ndege vya mikoa ya Kigoma, Tabora, na Shinyanga. Sekya nyingine ni Afya ambapo EU ilichangia ujenzi wa hospitali 3,000, vituo vya afya, zahanati na nyumba wafanyakazi wa vituo hivyo kutoka mwaka 2009 hadi mwaka 2012.

EU pia ilichangia fedha za kuwawezesha zaidi ya watu milioni 1.5 kupata maji safi na salama katika maeneo ya mijini na vijijini, huku ikiisaidia Tanzania katika kuboresha sekta za Elimu, Kilimo na Utawala bora.

Umoja huo una nchi wanachama 27 ambapo kati ya hizo nchi 11 zina balozi zake nchini Tanzania ambazo baadhi yake ni Ufaransa ,Italia, Finland, Ujeruman i, Uingereza ,Sweden, Hispania, Ireland na Uholanzi.

No comments: