Friday, May 17, 2013


JAMHURI YA MUNGANO WA TANZANIA
   

    WIZARA YA MAJI 






                   
                                       TAARIFA KWA UMMA

Katika gazeti la Nipashe la Jumapili tarehe 12 Mei 2013 mwandishi Mshaka Mgeta aliandika makala yenye kichwa cha habari “Aibu kwa Profesa Maghembe na dharau kwa wataalamu wa Wizara” na kuwa, Wizara ya Maji imejiwekea rekodi chafu kwa bajeti yake kurejeshwa kabla ya kupitishwa na Bunge na wataalamuwa wa Wizara ya Maji wamekuwa miongoni mwa wasiosikilizwa na kupuuzwa suala hilo si la kweli.
Mnamo tarehe 24 na 25 Aprili, 2013, Waziri wa Maji Mhe. Prof. Jumanne  Abdallah Maghembe (MB) aliwasilisha Bungeni Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2013/2014. Bajeti hiyo iliwasilishwa na mjadala uliendelea kwa muda wa Siku mbili. Mjadala mkubwa ulikuwa Bungeni baada ya kuwasilisha maoni ya Kamati ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa Bajeti ya Wizara ya Maji haitoshi.
Mjadala ulihairishwa na Mhe. Spika chini ya Kanuni ya Bunge 67(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kama Ibara ya 89(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sura ya 2 Toleo la 2002.
Wakati huo, Bunge halikuulizwa kama linakubali au kukataa Bajeti ya Wizara ya Maji. Mhe. Spika alisitisha mjadala wa Bunge ili kupata nafasi kwa Wizara kukaa pamoja na Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Wizara ya Fedha kuona ni jinsi gani Wizara ya Maji itaongezwa fedha kama iliyopendekezwa na Kamati ya Bunge.
Baada ya Bunge kukutana tena tarehe 29 Mei, 2013, Waziri wa Fedha alitoa taarifa Bungeni kuwa, Wizara ya fedha imekubali kuiongezea Wizara ya Maji fedha za nyongeza jumla ya Shilingi bilioni 184.5 kama ulivyopendekezwa na Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji. 
Huu ulikuwa ni ushindi mkubwa kwa Wizara pamoja na Kamati na wala sio kosa au aibu kama alivyoandika Bwana Mashaka Mgeta katika Makala yake ya gazeti la Nipashe tarehe 12 Mei 2013.
Mjadala uliendelea kuhusu namna fedha zilizoongezwa zinaingizwaje katika vifun gu vya matumizi ili Wizara ya Maji iweze kutumia kwa maombi hayo mahususi.  Spika wa Bunge alisitisha majadiliano kwa masaa ili Wizara ya Maji ikutane na wataalamu wa Wizara ya fedha pamoja na Kamati ili kuweka vifungu vya matumizi.
Fedha zilizoongezwa ziliingizwa kwenye mafungu na kuwasilishwa Bungeni. Mhe. Waziri wa Maji alikaribishwa Bungeni na kufanya majumuisho na Bunge kupitisha Bajeti yote kifungu kwa kifungu pamoja na fedha zilizoongezwa kufikia Shilingi bilioni 582,895,874,000 badala ya Shilingi bilioni 398,395,874,000 zilizokuwa zimepangwa awali.

Hii ni mara ya kwanza kwa Wizara kuongezewa fedha zaidi shilingi 184.5 bilioni. Kwa sababu ilikuwa ni mara ya kwanza, Wabunge walikuwa makini kuhakikisha kuwa jambo hili linafanywa kwa umakini mkubwa.Hivyo, sio kweli kuwa Bajeti ya Wizara ya Maji ilikataliwa na Bunge kama Bwana Mashaka Mgeta alivyoandika.Angekuwa ametafiti angeelewa wazi kuwa nyongeza hiyo ni ushindi na wala sio aibu kama alivyoandika yeye kwenye makala yake.

Kuhusu dharau kwa Wataalamu wa Wizara kama alivyoandika, sio kweli kwani Bajeti iliyopitishwa na Bunge pamoja na nyongeza yake ilitengenezwa na wataalamu hao hao wa Wizara kuzingatia vipaumbele vilivyopo.

Tungeshauri atupe maoni yake ambayo Wizara inaweza kuyatumia na angeeleza wanadharauliwa kwa kitu gani?

CV ya Mh.Waziri Prof. Maghembe kuwa amezaliwa mwaka 1970 tunashangaa kuona Mashaka Mgeta anaangalia tovuti moja tu ya Bunge na angekuwa mwangalifu asingeandika hilo maana katika tovuti hiyo, imeonyesha wazi kuwa Prof. Jumanne Abdallah Maghembe alianza Shule ya Msingi mwaka 1961 na mwaka 1970 alikuwa Kidato cha Sita ambako mwaka 1975 alitunukiwa Shahada ya BSc. na 1977 alipata MSc. na baadaye Phd. mwaka 1981.

Sasa kwa historia yake ya kielimu angewezaje kuzaliwa mwaka 1970?  Rais wa China marehemu Mao Tse Tung aliwahi kusema kuwa ” mtu ambaye hajafanya utafiti wa jambo hafai kulizungumzia” kama alivyofanya Bwana Mashaka Mgeta katika makala yake ya tarehe 12 Mei 2013.

Tunaheshimu sana na kujali kazi za Waandishi wa Habari lakini tunashauri kiandikwacho kiwe na ukweli vinginevyo wananchi wanapotoshwa bure na taarifa kama hizi.

         Imetolewa na

                                KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
                                                        WIZARA YA MAJI

17  Mei 2013

No comments: