Saturday, March 2, 2013



UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
Academic Staff Assembly
 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 2/3/2013


Utangulizi

Wapendwa waandishi wa habari. Tunaomba kupitia ninyi tuweze kuongea na watanzania wenzetu kuhusu hali ya amani ilivyo nchini mwetu kufuatia kila aina ya dalili ya watanzania kukosa uvumilivu wa kidini. Tunatambua kuwa serikali yetu imefanya mambo mazuri mengi tu nchini, hilo hatuna mashaka nalo; hata hivyo kama watanzania tunadhani kuna baadhi ya mambo hayaendi sawa. Hivyo basi, tunaomba kuchukua nafasi hii kuelezea wasiwasi wetu kuhusu migogoro hii ya kidini inayozidi kukua nchini.

Migogoro hii ilianza kuvuka kama moshi lakini sasa inaanza kulipuka na kusambaa zaidi. Tumeshuhudia uchomaji moto wa kanisa kule Mbagala, kumwagiwa tindikali shekhe mmoja kule Zanzibar na Shekhe mwingine kuuawawa, kuchomwa makanisa Zanzibar, kupigwa risasi viongozi wa kikristo kule Zanzibar na pia mgogoro wa kuchinja huko Geita ambako tumeshuhudia mchungaji mmoja akiuawa.

Mbali na hayo, kuna matukio kadhaa kwenye shule zetu za sekondari yakihusisha migogoro ya kidini kati ya wakristo na waislamu. Haya tumeshahudia yakitokea sekondari za Bagamoyo, Ndanda, Kibiti, Ilboru na kwingineko. Pia yapo malalamiko yasiyo rasmi kuhusu udini kwenye sehemu za kazi na kwenye taasisi mbalimbali za serikali. Wapo wanaodai kuwa baadhi ya taasisi binafsi, za kidini na hata za serikali zinazohudumia watanzania wengi zimekuwa zikiajiri wafanyakazi kwa misingi ya kupendelea dini fulani fulani. Jambo hili hata kama ni la kuzungumzwa tu, ni vema likafanyiwa kazi maana hisia hizi zikipanuka hujenga chuki na kusababisha watanzania wasielewane.

Kwanini haya yanatokea?

Sisi wanajumuiya ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tunaamini, kama taifa, kuna mahali tumechepuka na kuacha misingi tuliyoachiwa na Baba wa Taifa katika ujenzi wa taifa imara na lenye umoja. Kuna sababu kadhaa zilizotufikisha hapa tulipo, nazo ni:

1)      Wanasiasa na watanzania wengi tunafuata dini zetu kwa hisia zaidi pasipo kufikiri kwa kina kuhusu yale tunayoyafanya. Tumesahau kabisa kuwa dini ni kwaajili ya kutuhusianisha na ulimwengu ujao tusioujua. Tunapaswa kumheshimu na kumthamini kila binadamu aliyeko hapa duniani. Kwa bahati mbaya baadhi yetu tunadhani kuwa ulimwengu huu umeumbwa kwaajili ya dini fulani na binadamu wengine hawana haki ya kufurahia maisha yao hapa duniani. Tunataka kutumia dini zetu kumiliki utawala wa dunia hii.

Dini zetu zimekuwa mtaji kwa baadhi ya wanasiasa na vyama vyao. Inasikitisha kuwa hakuna jitihada za kutosha zilizofanyika kuzuia wanasiasa kutumia dini kama sera au ajenda ya katika kupata kura. Baadhi ya wanasiasa wameingia madarakani kwa kutumia udini na ukabila na hivyo hali inapofikia watanzania kuanza kuchukiana kwa misingi ya dini wanakosa nguvu na ujasiri wa kukemea na kuzuia haya kwakuwa nao wamepitia njia hiyo.

2)      Sababu ya pili ni kwamba hivi sasa umaskini nchini umekuwa wa kiwango cha juu. Kila mtu anatafuta jawabu la umaskini wake kwa kudhani kuwa umesababishwa na mfumo ulio nje ya maisha yake na ya serikali. Katika hali hii wamejitokeza watanzania wenzetu wanaotafuta majibu mepesi kwa kusingizia kuwa wamekuwa maskini kwasababu ya dini nyingine. Hali hii imesababishwa na ukosefu wa elimu kiasi kwamba watanzania wengi wanashindwa kuwa na uwezo wa kuchambua mambo kimantiki na badala yake wanaamini bila kuchuja lolote wanaloambiwa na viongozi wa dini au mwanasiasa au mwanaharakati. Ni vema watanzania wakajua kuwa ajenda ya udini si ya dini fulani bali ni ya makundi machache ndani ya taasisi zetu za dini. Tusibebeshe lawama za udini kwa dini fulani bali tuelewe kuwa udini umekuwa ni mtazamo ya watu wachache ndani ya dini zetu.

3)      Tatu, watanzania tumeanza kupoteza uelewa kuhusu madui wetu wa asili ambao ni ujinga, umaskini na maradhi, na tumeongeza adui mwingine ambaye ni imani ya mwingine. Tumeacha kuelekeza nguvu zetu katika kupambana na maadui hao watatu na tunaelekeza nguvu zetu kupambana na dini nyingine ambazo kimsingi haziwezi kuwa sababu ya matatizo yetu ya kila siku.  

Kwa bahati mbaya tunashindwa kuelewa kuwa dini hizi kuu mbili za kikristo na kiislamu ni dini zilizozaliwa sehemu mmoja baadaye zikasambaa sehemu tofauti na kuchukua utamaduni tofauti. Hatimaye tunachokiona sasa, ndugu wa ukoo na hata kabila moja waliotokana na historia moja, utamaduni mmoja na lugha moja wamefanywa maadui kwasababu wanafuata dini tofauti. 

4)      Jambo la nne, nchi yetu imeruhusu uhuru wa kuanzisha taasisi za dini pasipo kuwa na usimamizi wa karibu. Taasisi nyingi za kidini zimeibuka nchini na zimekuwa chanzo kikubwa cha kuwagawa watanzania kwa misingi ya kidini. Umoja wetu unapotea kwasababu baadhi ya taasisi za kidini zilizopo zinawagawanya watanzania kwa misingi ya dini. Taasisi nyingi za dini zinafundisha mbinu na namna ya kuwakabili waumini wa dini nyingine badala ya kuhimiza upendo na mshikamano miongoni mwa watanzania.

Baadhi ya viongozi wa taasisi hizo wamewafanya watanzania mtaji wao kwa kuwachochea wafuasi wao kuwachukia wengine kwa lengo la kutimiza haja zao binafsi. Watanzania tunapaswa kuzinduka na kuchukua tahadhari dhidi ya watu wanaotuchonganisha. Tukumbuke kuwa kiongozi wa dini anayekuambia kuwa dini fulani ni ya kishenzi na wafuasi wake ni wa kishenzi basi mtu huyo si mtumishi wa Mungu bali anatumikia maslahi yake.

Tufanyeje? 

Baada ya kueleza sababu zilizotufanya tufikie hapa tulipo sasa, sisi wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tunapendekeza mambo yafuatayo:

1)      Serikali isimamie na kudhibiti vyombo vya habari vya kidini vinavyochochea chuki za kidini. Inasikitisha kuwa serikali iliyosheheni wataalamu wa kila aina inashindwa kutambua madhara ya uchochezi wa vyombo vya habari. Watanzania tunapaswa kujifunza kuwa hata mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda hayakuanza siku moja, yalichochewa na vyombo vya habari kwa muda mrefu na vyombo hivyo vilihamasisha pia mauaji hayo.

Hata hapa nchini kwetu, serikali isipokuwa tayari kukemea na kufungia vyombo vya habari vinavyotumia udini kuleta uchochezi, ipo siku watanzania watauana sana na nchi itapoteza heshima yake ya kuwa taifa la amani na tutakuwa wakimbizi. Tunaishangaa serikali inaweza kuyafungia magazeti yanayoikosoa lakini haiko tayari kuyafungia magazeti yanawachochea watanzania.

Tungependa ujasiri unaotumika na vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata wanaoandika ujumbe wa vitisho kwa viongozi wa kisiasa nchini utumike pia kuwakamata wanaochochea uvunjifu wa amani. Kama tunaweza kuwalinda viongozi dhidi ya vitisho kwa maisha yao binafsi kwanini tushindwe kulilinda taifa letu kwa kutumia nguvu hizo hizo za kuwatumikia wanasiasa?

2)      Pia tunatoa wito kwa wanasiasa na watanzania kwa ujumla kuwakataa wale wanaotafuta vyeo mahali popote pale, iwe kwenye vyama vya siasa au taasisi, kwa kutumia udini kama kigezo cha kutaka kuchaguliwa. Ni wakati muafaka sasa kuhuisha yale yote yatakayoleta mtangamano wa kitaifa. Kama taifa tumeacha misingi mizuri ya ujenzi wa taifa tuliloachiwa na waasisi wa taifa hili.

3)      Jambo jingine ni kuhamasisha na kusimamia sera ya elimu sawa kwa wote. Elimu yetu ya sasa imejenga matabaka makubwa miongoni mwa watanzania na matokeo yake matabaka haya yanajitokeza zaidi katika sura ya udini. Kutokana na hali hii watanzania wengi waliokosa elimu wanadhani kuwa wenzao wa dini nyingine wanafanikiwa kwasababu ya upendeleo wa kidini. Kwa kusisitiza katika elimu, itakuwa rahisi kwa watanzania kuelimishwa kuwa chuki za kidini si msingi wa dini zetu tofauti na ilivyo sasa ambapo ukosefu wa elimu unawafanya wengi kuwa waathirika wa mafundisho potofu.

4)      Pia tunaisihi serikali iwachunguze viongozi wa baadhi ya taasisi za kidini zinazowahamasiha wafuasi wake kufanya vitendo vya uhalifu. Ni vigumu sana kuwadhibiti wafuasi wa taasisi ya kidini ambao wameshakuwa na nguvu ya kuungana na kufanya jambo lolote baya. Tuna wasiwasi kuwa baadhi ya viongozi wa taasisi hizo wanatumika na watu wa nje kuvuruga amani yetu. Kwa bahati mbaya viongozi hawa wanajua wazi kuwa amani ikivurugika nchini wao wanazo sehemu za kukimbilia wakati ndugu zetu wakiendelea kuuana.


Wito wetu kwa watanzania wenzetu ni kwamba wajue kuwa viongozi wa kidini wanaowachochea kuwachukia wengine hawana nia njema na taifa na maisha yao. Watatuacha tukiliangamiza taifa huku wao wakiwa salama. Ni vema watanzania wakajua kuwa sababu ya umaskini na matatizo ya kimaisha hayajasababishwa na waumini wa dini nyingine bali mfumo wetu mbovu wa utawala unaoacha kukua kwa matabaka ya kijamii. Tukishirikiana sote kupambana na umaskini hakutakuwa na sababu ya kuchukiana. Pia, ni muhimu sasa, kila dini iendeshe maswala yake bila kutaka kubebwa na serikali.



Asanteni sana

3 comments:

Anonymous said...

It should be signed to prove its authenticity.UDSM is very high reputable institution.

Anonymous said...

nimeupenda mstari unaosema kuhakikisha dini hazibebwi na serekali kuendesha mambo yake! tuondoe ruzuku kwenye shughuli zote zinazoendeshwa na taasisi za dini,inashangaza kuona serikali inaweza kutoa ruzuku ila haiwezi kuendesha shughuli za kijamii za wananchi wake!! je,ni sawa kwenye taasisi za serikali watu kufungulia redio/miziki au mahubiri yanayohusu imani zao sehemu za kazi??hatuoni kuwa inaweza kuwa njia mojawapo ya kusambaza udini?? tunapaswa kufikiri zaidi na sio kuishia hapo mlipoishia kama wasomi..matatizo haya yanahitaji mjadala wa kina na sio kama mlivyoainisha katika waraka wenu kwani tuna mengi ya kujadili juu ya hili kama taifa.

Anonymous said...

Masikitiko yangu ni kuwa tuna wasomi wanasema nadharia zinazozungumzwa mitaani bila data.

Na tatizo hata mapendekezo yako hayatekelezeki kiserikali kwani yataleta matatizo zaidi. Kuishauri serikali kunyima vyombo vya habari uhuru hakudumishi amani. Kumbuka uhuru ni kuweza kusema lolote hata kama linamuudhi mtu almuradi si tusi. Na kila mtu ajuwe kila amtu ana uhuru wa kusema mawazo yake hata kama ni mabaya.

Angalia mi msomi suluhisho langu sasa:

Pamekuwepo na manung'unukio ya udini kwa miaka mingi. Data zimekuwa ni idadi ya waajiriwa serikalini inaonyesha dini fulani imejaa. Pia elimu ya juu (wahadhiri na wanafunzi) wengi ni dini fulani.

Kimsingi malalamiko ni ya msingi lakini kiini cha tatizo kimekuwa kikipuuziwa. Matatizo yanasababishwa na vyanzo vya ndani (ya waumini) na vyanzo vya nje.

Tatizo walalamikaji hawakubali vyanzo vya ndani vya tatizo na hueleza vyanzo vya nje tuu (yaani udini). Tatizo sambamba pia ni watatuaji wa tatizo hawakubali kutatua matatizo ya vyanzo vya nje wanataka vyanzo vya ndani tuu (kama vile ubaguzi haupo na hawapendi shule). Mtazamo wangu ni kwamba vyanzo vyote vya tatizo ni halisia.

Zao la tatizo limekuwa kukomaa kwa tatizo kwani halitatuliwi. Hakuna kiongozi mkubwa anayetaka kulitatua kitaalamu na wala hakuna mwongozo wa kikatiba wa kutatua udini. Bila mwongozo bali utatuzi utakuwa na tatizo zaidi. Mfano, utatuzi wa udini si kupata raisi wa dini fulani kutumia madaraka yake vibaya kuwapendelea wanaodhani kuonewa. Hilo litafanya raisi wa dini nyengine kuonea pia na nchi itakuwa jalala. ufumbuzi unatakiwa uwe kikatiba na kisheria kivitendo.

Kama udini upo basi usipewe majibu rahisi. Sitarajii kama kuna kiongozi mdini atakubali upo. Na pia tafsiri ya neno udini iko chali, wengi wamaanisha kusali saana badala na siyo kumbagua mtu kwa misingi ya dini.

Serikali, badala ya tuu kulaani ubaguzi, inatakiwa ianzishe sheria ya kuwaadhibu wadini katika sekta za serikali. Laana ni maneno matupu hayavunji mfupa. Laana hizi zinafanya udini uendelee kukuwa zaidi ya sasa. Na unaweza kukuta hamna hata mmoja katoa wazo hili kwa katiba mpya. Nani atoe? Tumezoea mtu akisema kuna udini nasi twamzomea yeye mdini. Nani anataka kuzomewa? Hapa hakuna kiungo cha kutolea maoni huru.

Tumejitolea hadi damu kukomesha ukaburu nje lakini tumeshindwa hata kukubali kuwepo ukaburu ndani ya nchi. Kwa nini, tunadhani kukubali upo ndo kuukuza badala ya kuwa ni hatua ya mwanzo kuuondoa. Mficha ugonjwa mauti yalimuumbua.